KKKT yatoa pole maafa Hanang, apongeza juhudi za uokozi

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo
Muktasari:
- Maafa yaliyotokana na maporomoko katika Mlima Hanang, yalisababishwa na miamba dhoofu ya mlima huo kunyonya maji, na hivyo kusababisha mgandamizo huku sehemu ya mlima huo ikishindwa kuhimili, na hivyo kumegeka na kutengeneza tope lililoporomoka.
Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo ametoa pole kwa Serikali na wananchi, kufuatia maafa yaliyotokea katika Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara, ambapo watu 65 wameripotiwa kupoteza maisha na wengine 117 kujeruhiwa.
Maafa hayo yanafuatia maporomoko ya tope, mawe na maji yaliyotoka katika mlima Hanang baada ya miamba dhoofu ya mlima huo kunyonya maji na kusababisha mgandamizo, huku sehemu ya mlima huo ikishindwa kuhimili na kumeguka na hivyo kutengeza tope lililoporomoka.
Dk Shoo ametoa pole hizo leo, Desemba 5, 2023, wakati akizungumza kwenye ibada maalumu ya kuuaga mwili wa Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo, Dk Erasto Kweka ambapo amesema Kanisa linafarijika na juhudi mbalimbali zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali kusaidia waathirika wa maafa hayo.
"Nitoe pole nyingi kwa Serikali na Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa maafa makubwa yaliyotokea kule wilayani Hanang ambako kumetokea maporomoko na ndugu zetu wengi wamepoteza maisha," amesema Dk Shoo na kuongeza kuwa;
"Tunajua Serikali imewekeza nguvu kubwa kule kuwasaidia ndugu zetu waliopata maafa na tunapenda kushukuru maana tangu kumetokea yametokea tumeona kinachofanyika,”amesema.
Aidha Dk Shoo amesema Kanisa limefarijika pia kuona Serikali inawakimbilia tangu kulipotokea msiba wa Dk Kweka hadi leo wakati wa ibada maalumu ya kuuaga mwili wake, ambapo Serikali imewakilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko.
Akizungumzia maafa hayo, Dk Biteko amesema Serikali inaendelea kufuatilia miili ya watu wengine kuendelea kutoa huduma kwa wale waliopata majanga.
“Tumepata majanga makubwa kama alivyosema baba Askofu. Wamefariki wengi bado tunaendelea kutafuta miili ya watu wengine. Tunaendelea kutoa huduma kwa wale waliopata majanga,” amesema Dk Biteko.
Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kidini, kisiasa na serikali.
Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, Mwenyekiti wa Cham Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi.
Dk Kweka ambaye amekuwa kiongozi wa Dayosisi ya Kaskazini toka mwaka 1976 mpaka 2004 alipostaafu, alifariki dunia, Novemba 25,2023, katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa kesho, Desemba 6,2023, katika Kijiji cha Uswaa, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa historia, Askofu Dk Kweka alikuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu, na ametibiwa katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Novemba 7, 2023 akiwa nyumbani kwake hali yake ilibadilika ghafla, akapelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambapo baada ya matibabu ya kina alipewa rufaa ya kwenda JKCI na Novemba 25 saa 4:00 asubuhi alifariki dunia.