Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu KKKT: Acheni kuozesha wasichana kwa mazao

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri  (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo Ole Paul, akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Duniani iliyoandaliwa na Mradi wa Hapana Marefu yasiyo na Mwisho unaotekelezwa na C-Sema, Amani Girls kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya. Picha na Lilian Lucas

Muktasari:

  • Ili wasichana waweze kuendelea na masomo jamii imetakiwa kutowaozesha watoto hao kwa kubadilishana na mazao kwani ni kosa.

Morogoro. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, imeitaka jamii kuacha tabia ya kubadilisha mazao na binadamu kwa lengo la kuozeshwa watoto wa kike na kuwaacha wasome ili watimize ndoto zao.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo Ole Paul, ametoa wito katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Duniani iliyoandaliwa na Mradi wa Hapana Marefu yasiyo na Mwisho unaotekelezwa na C-Sema, Amani Girls kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya.

Askofu Mameo amesema watoto wa kike hawapaswi kuuzwa kama mazao, kwa sababu wana haki ya kupata haki zote ndani ya jamii ikiwemo elimu na kufanya hivyo ataondokana na utegemezi katika kujenga taifa.

Amesema viongozi wa dini wanaungana na Serikali katika mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971, kwani sheria hiyo sio rafiki kwa mazingira ya sasa na ina mnyima haki mtoto wa kike kushindwa kutimiza ndoto zake na kuingia kutengeneza familia wakati muda wake bado haujafika.

“Sisi viongozi wa dini tuko mstari wa mbele katika mabadiliko ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971, ndoa za utotoni hazikubaliki, Serikali endeleeni na mchakato wa mabadiliko ili tuweze tengeneza mazingira rafiki kwa mtoto wa kike kuweza kutimiza ndoto zao.” amesema Askofu Mameo.

Naye Shekhe wa Mkoa wa Morogoro,Twaha Kilango amesema ukatili wa kijinsia umeteketeza jamii kubwa ya Watanzania, hivyo ifikie wakati tuungane pamoja na kuweka nguvu katika kutokomeza ukatili wa kijinsia hususani kupinga ndoa za utotoni katika jamii zetu.

“Tushikamane, tushirikiane na kupaza sauti katika kutokomeza ukatili kwa watoto wetu wa kike, wakati unabadilika na sisi tunapaswa kubalika na tutumie viongozi wa dini katika kuelimisha jamii kwa wazi na kuibadilisha kuondokana na mitazamo ambayo sio sahihi” amesema Shekhe Kilango.

Amesema tuko wakati ambao umma umepotoka na kuporomoka kimaadili, hivyo viongozi wa dini na Serikali watumie nafasi zao ndani ya jamii katika kukemea na kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia unaotokea ndani ya jamii, watoto wa kike wanapaswa kulindwa na kupewa haki zao.

Chifu wa Kabila la Kimasai Kashu Moreto amesema hivi sasa jamii za kifugaji zinabadilika na kuondokana na mila kandamizi na hiyo inatokana na elimu inayotolewa katika makanisani na jamii kuwataka wazazi kukaa karibu na watoto kujua changamoto zao.

Amesema kuna haja ya kuongeza adhabu wanazopewa watu wanaokutwa wamefanya vitendo vya ukatili wa kijinsia ili iwe fundisho zaidi, adhabu zikiongezeka na kutekelezwa ipasavyo itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kiongozi Mkuu wa Mradi wa Hapana Marefu yasio na Mwisho, Patricia Mwaikenda amesema mradi huo umekijita katika kufanya mabadiliko katika mila, desturi potofu ndani ya jamii ambazo zinamkandamiza mtoto wa kike kushindwa kutimiza malengo yake.

Mwaikenda amesema mradi una malengo matatu ambayo ni kuwajengea uwezo watoto wa kike kuweza kujitambua na kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili, elimu kwa viongozi wa dini na utetezi wa mabadiliko ya sera na sheria ikiwemo sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Pia watoto wamesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo Ukatili wa kijinsia majumbani, mashuleni, mitaani, kunyimwa fursa sawa ya kupata elimu na kutimiza ndoto zao, kutothaminiwa hata kufikia hatua ya kulinganishwa thamani na Ng’ombe, watoto wetu wanalazimishwa kuolewa katika umri mdogo ili wazazi waweze kupata mali hususani Ng’ombe.

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 haitoi utetezi wa haki ya mtoto wa kike kwa kuwa inahalalisha mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi.