Askofu KKKT ang’olewa Konde, yeye agoma

Muktasari:

  • Mkutano mkuu maalumu wa Dayosisi ya Konde ulioitishwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo umemvua wadhifa wa uaskofu, Askofu wa dayosisi hiyo, Edward Mwaikali na kuibua maswali.


Mbeya/Moshi. Mkutano mkuu maalumu wa Dayosisi ya Konde ulioitishwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo umemvua wadhifa wa uaskofu, Askofu wa dayosisi hiyo, Edward Mwaikali na kuibua maswali.

Wajumbe wa mkutano huo ambao walikuwa ni wale waliohudhuria mkutano mkuu wa dayosisi hiyo mwaka 2017, pia walimchagua kwa kura 2,014, Mchungaji Geofrey Mwakihaba kuwa Askofu mteule wa dayosisi hiyo ya Konde.

Mbali na kumuondoa madarakani Askofu Mwaikali, tume iliyoundwa na mkuu wa kanisa chini ya uenyekiti wa Askofu Alex Malasusa, imerejesha makao makuu ya dayosisi hiyo Tukuyu kutoka Ruanda jijini Mbeya huku utaratibu wa kurudisha kiti cha askofu ukiandaliwa.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Askofu Mwaikali alipinga uamuzi huo akisema utaratibu uliotumika haupo mahali popote pale na kwamba zipo taratibu za kikatiba za kumuondoa askofu lakini hazikufuatwa.

“Mimi sikuhudhuria huo mkutano kwa sababu nilikuwa siutambui na hili nilishalisema tangu mwanzo. Nimesikia tu kwamba maamuzi ni hayo, sijaambiwa rasmi. Wakishaniambia nitakuwa na neno la kusema,” alisema Askofu Mwaikali.

“Kimsingi mkuu wa Kanisa la KKKT amewatwisha laana wana Dayosisi ya Konde kwa sababu amekwepa kuwa mwenyekiti wa mkutano aliouitisha mwenyewe bila kushirikisha Halmashauri Kuu ya KKKT Konde. Amenawa mikono kama alivyofanya Pilato.

“Wajumbe wa huo mkutano hawakuwa halali kwa sababu Katiba ya KKKT Dayosisi ya Konde kanuni ya 06.29.03.01 inasema hakutakuwa na kipindi maalumu cha ujumbe wa mkutano mkuu,” alisema Askofu Mwaikali na kuongeza kuwa:

“Mkuu wa Kanisa katika barua yake aliagiza kwamba wajumbe watakaoshiriki mkutano mkuu ni wale wa mkutano mkuu wa 2017, si sawa hata kidogo,” alisema.

Uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya dayosisi hiyo kutoka Tukuyu kwenda Usharika wa Ruanda jijini Mbeya unaelezwa kupata baraka za mkutano mkuu wa dayosisi ambapo kura 202 ziliafiki uhamisho huo na kura mbili zilikataa.

Hata hivyo, uamuzi huo haukuafikiwa na baadhi ya wachungaji na waumini wa dayosisi hiyo, hususan wa Tukuyu, na hapo ndipo mgogoro ulipoibuka na tume ya Askofu Malasusa iliyoundwa kuchunguza, ilisema uamuzi huo ulikiuka katiba ya Dayosisi ya Konde. Baada ya jitihada za kusuluhisha mgogoro huo kushindikana kwa zaidi ya mwaka, mkuu wa Kanisa aliingilia kati na kuitisha mkutano mkuu maalumu juzi, ambao umemuondoa Askofu Mwaikali.

Jana Mwananchi lilipomtafuta kwa simu Askofu Shoo ili kuzungumzia madai ya Askofu Mwaikali ya kwamba mkutano huo ulikuwa batili kwani wajumbe walikuwa batili, simu yake iliita muda mrefu bila kupokewa.

Kura zamwondoa

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Dk Shoo alisema kura 211 zilipigwa na kati ya hizo, 204 zilimkataa Dk Mwaikali, huku tano pekee zikimkubali. Kura mbili ziliharibika, kisha ukafanyika uchaguzi wa kumpata askofu mpya.

Askofu Shoo alimtangaza Mwakihaba kuwa askofu mteule baada ya kupata kura 149 na mchungaji Dk Meshack Njiga kura 55. Kura sita ziliharibika

Askofu Shoo alisema mchungaji Mwakihaba alipata kura zaidi ya theluthi mbili. Askofu mteule atasaidiana na mchungaji Njiga kama msaidizi wa Askofu.

Akizungumza katika mkutano huo, Askofu Shoo alitoa angalizo kwa washirika kujiepusha na ukabila na kutoa ushirikiano wa viongozi wapya na kufuata mapendekezo ya kamati iliyorudisha makao makuu Tukuyu.

“Tuepuke ukabila, tushirikiane na wateule na kuendeleza mshikamano kwa masilahi ya kanisa ili kazi ya Bwana isonge mbele, lakini pia makao makuu yarudishwe Tukuyu,” alisema Dk Shoo, ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini.

Uchaguzi batili

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano mkoa wa Mbeya, Askofu Oscar Ongere alisema maamuzi ya Askofu Shoo yamekuwa ya haraka na kwamba uchaguzi huo ni batili kwa kuwa haujazingatia katiba ya Dayosisi.

Askofu Ongere alisema Jumuiya ilimtaka Askofu Shoo kusubiri kikao cha maaskofu wa KKKT nchini kinachotarajia kufanyika Jumatatu ili kupata maamuzi ya pamoja ambayo yangeondoa mvutano baina ya viongozi hao.

“Kwanza tuliunda tume huru, ambayo ilibaini kuwapo kwa mgogoro wa kikabila. Uamuzi huo wa Dk Shoo umekuwa wa haraka sana na hatujui ni kwa nini. Kuna mkutano wa maaskofu Machi 28, ambao ungetoa maamuzi,” alisema Ongere. Askofu huyo aliongeza kuwa uchaguzi huo unaongeza zaidi majeraha na maumivu kwa waumini kwa sababu huo mkutano walioufanya ni kuikanyaga katiba ya Dayosisi ya Konde.

Mgogoro wa Dayosisi ya Konde ulifikia hatua mbaya Agosti mwaka jana, ambapo wachungaji 17 walitimuliwa na Desemba 2021 Askofu Mwaikali na wachungaji 85 walitimuliwa katika ibada ya mazishi ya baba mzazi wa Askofu Malasusa.