Askofu Mlola: Tuvue utu wa kale tuvae mpya, tusameheane

Muktasari:
- Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Askofu Joseph Mlola amewaongoza waumini wa kanisa hilo kuupokea kuuaga mwaka 2022 na kuupokea mwaka mpya 2023 huku akitoa nasaha za kusameheana.
Kigoma. Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Joseph Mlola amewataka waumini wa kanisa hilo kuuvua utu wa kale na kuvaa utu mpya kwa kuacha matendo mabaya waliyokuwa wakifanya mwaka 2022 na kufanya matendo mema kwa mwaka 2023.
Akizungumza wakati akiongoza ibada ya misa takatifu ya kuupokea mwaka mpya 2023, katika Parokia ya Bikira Maria Mshindaji, Askofu Mlola amesema kila muumini atumie nafasi hiyo kutafakari maisha yake aliyoyaishi kwa mwaka 2022 na kuchukua hatua ya mabadiliko.
Askofu Mlola amesema kila mmoja aweze kujiangalia nafsi yake na kutokujihurumia kuacha mambo yote ya ukale ambayo mtu amefanya kwa mwaka 2022 na kujipanga upya kwa kufanya mambo mapya ambapo ni pamoja na kuacha dhambi.
“Kila mmoja kwa nafasi atumie muda huu kujitafakari moyoni mwake na kuona umuhimu wa kuacha mambo ya kale ambayo yalikufanya kushindwa kumsogelea Mungu na kuvaa utu upya kwa kufanya matendo mema kwa mwaka huu mpya wa 2023,” amesema Askofu Mlola.
Askofu Mlola amewataka waumini hao pia katika mwaka mpya kudumisha upendo wa wao kwa wao na katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.
Amesema kila mmoja kwa nafasi yake ampende jirani yake kama nafsi yake, wahurumiane wao kwa wao na kusameheana kama maandiko yanavowataka kufanya hivyo.
“Tuvuke mwaka mpya kwa upendo, tusameheane sisi kwa sisi, mtu usione vibaya kujishusha kama umemkosea mwingine na mwambie mwenzio nimekosa kutoka moyoni huo ndio ukristo,” amesema Askofu Mlola.