Askofu Nyaisonga awaomba wadau kusaidia wanafunzi wenye uhitaji
Askofu Mkuu Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga akimshukuru mdau wa elimu na Mkurugenzi wa Shule za Paradise na Patrick Mission, Ndele Mwaselela kwa kutoa udhamini wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi sita.Picha na Hawa Mathias.
Muktasari:
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Gervas Nyaisonga amewataka wakuu wa vyuo vishiriki vya kanisa kupaza sauti kwa wadau kueleza changamoto za wanafunzi wenye uhitaji ambao wamekosa udhamini na mikopo ya elimu ya juu kwa lengo la kupata misaada kuendelezwa na kutimiza ndoto zao.
Mbeya. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Gervas Nyaisonga amewataka wakuu wa vyuo vishiriki vya kanisa kupaza sauti kwa wadau kueleza changamoto za wanafunzi wenye uhitaji ambao wamekosa udhamini na mikopo ya elimu ya juu kwa lengo la kupata misaada kuendelezwa na kutimiza ndoto zao.
Nyaisonga ambaye ni Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Mkuu wa Vyuo Vikuu vya Vishiriki vya Katoliki (SAUTI) amesema hayo leo Jumanne Aprili 26,2022 wakati wa uzinduzi wa mfuko wa udhamini wa elimu ya juu kwa wanafunzi sita wa Chuo hicho ulioanzishwa na mdau wa elimu na Mkurugenzi wa Shule za Paradise na Patrick Mission, Ndele Mwaselela.
Amesema kuwa kumekuwepo na changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi wanapata fursa ya elimu ya ya juu lakini wanakosa mikopo serikalini jambo ambalo linalowafaya kughairi masomo kwa mwaka husika.
''Kuna jumla ya wanafunzi 40 walikwama kuendelea na masomo kutokana na kukosa mikopo ya elimu ya juu hivyo kitendo cha mdau wa elimu kujitolea kusomesha ni sadaka kwa Mungu na Ishara kubwa Mbinguni kwa kuliona kundi hilo.'' amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule za Paradise na Patrick Mission ambaye ni mdau wa maendeleo Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amesema kuwa ameguswa kusaidia watoto hao kutokana na kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike.
''Kwa kipindi cha mwaka jana mpaka sasa jumla ya wanafunzi 400 wa elimu ya juu nimewafadhili katika vyuo mbalimbali nchini na sasa nimeanza kwa Chuo kikuu Kishiriki cha Katoliki Mbeya (CUCOM ''amesema.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT, Profesa Coster Ricky Mahalu amesema kutokana na changamoto hiyo wameweka mikakati ya kuanzisha mfuko wa elimu kwa ajili ya kuendeleza wanafunzi wenye uhitaji.
Amesema kwa upande wa SAUT jijini Mwanza asilimia 75 ya wanafunzi wa elimu ya juu ndio wamepata mkopo serikalini huku idadi kubwa wakiwa wamekosa na kukata tamaa na kuendelea kupata.
Mwanafunzi aliyepata udhamini wa masomo, Grady Sanga amesema wamekuwa wakikata tamaa kutokana na kukosa mikopo ya elimu ya juu na kwamba fursa hiyo waliyoipata itakuwa chachu kwao kusoma kwa bidii