Ataka Bunge lisitishe shughuli zake kujadili vurugu, watu kupigwa risasi

Mbunge wa Kwela (CCM) Deus Sangu wakati akiomba bunge liahirishwe  leo Jumanne, Novemba 7, 2023 ili kujadili mgogoro kati ya wananchi na taasisi ya Epheta Ministry jimboni kwake ambao umesababisha watu kupigwa risasi. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Bunge limeagiza Wizara ya Ardhi kwenda mara moja katika eneo hilo ili wakaone kinachoendelea na kuwapatia ufumbuzi.

Dodoma. Bunge limeagiza Serikali kwenda haraka katika Jimbo la Kwela mkoani Rukwa kwa ajili ya kusaidia mgogoro kati ya wananchi na Taasisi ya Epheta Ministry ambao umepelekea watu kupigwa risasi.

Agizo hilo limetolewa bungeni leo Junanne Novemba 7, 2023 na Mwenyekiti wa Bunge, Daniel Sillo baada ya mbunge wa Jimbo hilo, Deo Sangu (CCM) kuomba shughuli za bunge zisimame ili wabunge wajadili vurugu za jana katika jimbo hilo ambazo zilipelekea wafugaji watatu kupigwa risasi.

Mbunge huyo amewataka wafugaji waliopigwa risasi ni Eliud Kauzeni, Danson Charle na Festo Kamwaga na wawili kati ya majeruhi hao wapo hospitali za rufaa Mbeya na Sumbawanga kwa matibabu.

Jana katika kipindi cha maswali la majibu mbunge huyo aliuliza swali kuhusu namna ya kutatua mgogoro huo ambapo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa aliahidi Kwenda huko Novemba 17, 2023 kwa ajili ya kuangalia jambo hilo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilisema kuhusu mgogoro huo wa muda mrefu na nikaomba Serikali iingilie kati ambapo Waziri wa Ardhi aliahidi kuja Novemba 17, lakini jana hiyo hiyo kumetokea machafuko kwa wafugaji watatu kupigwa risasi, naomba bunge lako liahirishe shughuli zake ili kujadili jambo hili kwa dharura,” amesema Sangu.

Katika hoja yake ambayo iliungwa mkono na wabunge wengi amesema kabla ya mgogoro wa jana, kuna ubakaji kwa wanawake ambapo 10 walisharipoti wake, wananchi kukatwa masikio na walinzi, mwanamke mjamzito alianguka na kupoteza maisha wakati akiwakimbia walinzi na vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa watu ni vingi.

“Serikali yetu inasifika duniani kwa kuwa na utulivu na amani, lakini vitendo hivi vinaipa doa, je tunataka watu wangapi wafe, watu wangapi wakatwe viungo, watu wangapi wapigwe risasi na watu wangapi waumizwe ndipo ichukue hatua,” amehoji.

Akijibu tuhuma hizo, Naibu Waziri wa Ardhi, Geofrey Pinda amekiri kuwa jambo lilitokea jana na kwamba wanazo taarifa watu wawili walikimbizwa hospitali za rufaa mmoja Mbeya na mwingine hospitali ya rufaa ya Sumbawanga na kwamba hali zao kwa mujibu wa taarifa, zinaendelea vizuri ingawa mmoja wa majeruhi hao hakwenda hata hospitali.

Naibu Waziri ameomba wananchi wa maeneo hayo kuwa watulivu katika kipindi ambacho Serikali inakwenda kutafuta ufumbuzi wa jambo hilo na kutafuta suluhu ya kudumu.