ATCL wafanye haya kuakisi uwekezaji

Muktasari:

  • Gaudence alisema shirika hilo halina budi kudumisha na kuendeleza rekodi nzuri ya kiusalama kwa sababu tangu wameanza shughuli zao hakujawahi kutokea changamoto kubwa.

Dar es Salaam. Wakati ndege mpya aina ya Boeing 737-9MAX ikitarajia kuingia nchini leo, uwekezaji wa Serikali katika kulifufua Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) unakaribia kufika takribani Sh4 trilioni katika kipindi cha miaka minane ambayo imekuwa na mafanikio na changamoto kadhaa.

Miongoni mwa mafanikio ya ATCL katika kipindi hicho cha karibu muongo mmoja uliopita, ni kufanikiwa kuongeza umiliki wa soko la usafiri wa anga nchini kutoka asilimia 2.5 hadi kufikia karibu asilimia 60 ilionao sasa.

Kuongeza safari za ndani ya nje ya nchi na kuongezeka kwa idadi ya ndege, nayo pia ni miongoni mwa mafanikio yake, licha ya kuwapo kwa malalamiko ya kuahirishwa kwa safari mara kwa mara, huku ufikishaji wa taarifa hizo kwa wasafiri wake na namna wanavyohudumiwa vikitajwa kukwaza utendaji wa shirika hilo.

Mmoja wa abiria wake ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini aliyesafiri na moja ya ndege za shirika hilo, alisema ubadilishwaji wa ratiba hizo unaleta usumbufu kwa abiria.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi

“Awali nilitaka kusafiri saa 7 mchana, lakini wakala aliyetukatia tiketi akasema ratiba imehamishiwa asubuhi saa 12, ikabidi tukubali. Kesho tumefika uwanjani, tukaambiwa na mmoja wa wahudumu wa ATCL kuwa tutapanda ndege ya saa 3 asubuhi, ikabidi tukatae. Baada ya mabishano pale, ndio wakakubali kutupa nafasi ndege ya saa 12 asubuhi,” alisema.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha ubadilishwaji wa ratiba za ndege ni viongozi wa kitaifa kutumia ndege hizo.

Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ambaye ndiye mwenye majukumu ya kusafirisha viongozi, ndiye mmiliki wa ndege zinazoendeshwa na ATCL.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi alisema: “Hii hutokea mara chache iwapo ratiba za safari imezibana ndege zingine za Serikali.

Tatizo si kubwa kiasi hicho na linakwenda kumalizika kutokana hatua zinazochukuliwa ikiwemo kuiongezea ndege ATCL na ikilazimu viongozi hutumia ndege za kukodi. Kwa kweli ATCL inafanya vizuri katika kutoa huduma zake na ni mara chache tu ndiyo hutokea mabadiliko madogo ya safari”

Alisema hadi sasa Serikali imeshanunua ndege 13 na inayoingia leo ni ya 14.

“Kesho (leo) tunaipokea Boeing 737-9MAX na sasa zitakuwa jumla ndege mpya ni 14,” alisema na kuongeza kuwa mbali na ndege hizo kuna Dreamliner moja ambayo bado inachongwa kiwandani ) na nyingine Bombadier Q300 au Dash 8 Q300 iliyopo kwenye matengenezo kisiwani Malta.


Uwekezaji wa Serikali

Ununuzi wa ndege hizo unatajwa kufikia Sh3.63 trilioni kwa kipindi cha miaka minane ikiwa ni juhudi za kuliinua shirika hilo, taarifa zinaonyesha.

Fedha hizo ni zile zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri katika bajeti za kuanzia mwaka 2016/17 hadi mwaka huu. ATCL iliyokuwa na ndege moja aina ya Bombardier Q300 iliyokuwa ikifanya kazi hadi mwaka 2015, imekuwa ikipokea fedha za ruzuku tangu mwaka 2016.

Ununuzi wa ndege mpya hivi karibuni unalifanya shirika hilo kuwa na ndege 14 na inaiweka Tanzania katika ramani ya nchi zenye mashirika ya ndege ya umma duniani yanayotumia ndege za kisasa ikiwemo hiyo ya MAX 9 na ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F.

Uchambuzi uliofanywa kupitia kumbukumbu za vitabu vya bajeti ya Serikali unaonyesha uboreshaji wa shirika hilo ulianza katika mwaka wa fedha wa 2016/17 wakati wa hayati John Magufuli baada ya Serikali kutenga Sh500 bilioni za kununua ndege mpya, kiasi hicho hicho pia kilitengwa mwaka 2017/18.

Mwaka 2018/2019 Serikali ilitenga Sh495.6 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa ndege na Sh500 bilioni za ununuzi wa ndege zilitengwa katika mwaka uliofuata mwaka 2019/2020.

 Mwaka 2020/2021 Sh450 bilioni zilitengwa na mwaka 2021/2022 Serikali ilitenga Sh450 bilioni na Sh468 bilioni zilitengwa kwa ajili ya ATCL kuelekea mwaka 2022/2023, wakati mwaka 2023/2024 Serikali ilitenga Sh271 bilioni kwa ajili ya shirika hilo.


Ijue ndege mpya

Pengine unaweza kujiuliza ndege hiyo ina uwezo gani na sifa zake nyingine ni zipi ikilinganishwa na ndege ambazo tayari zipo katika shirika la ndege la Tanzania (ATCL)?

Uwezo wa Max 9 kupakia abiria ni wastani wa abiria 220 kulingana na mpangilio wa ndani, huku ikisafiri hadi umbali wa kilometa 6,110 bila kulazimika kutua.

Ndege hiyo ambayo toleo lake la kwanza lilitoka mwaka 2017 inatumia injini ya LEAP-1B ambayo inatengenezwa na CFM International ya Marekani. Gharama yake inatajwa kuwa Dola za Marekani milioni 128.9 hadi 135 (Sh323.79 bilioni hadi Sh339.12 bilioni).

Urefu wake ni mita 42.16 na upana wa mabawa yake ni mita 35.9 inaendeshwa na marubani wawili na wahudumu wa ndani ya ndege wanne.


Wasemacho wachambuzi

Mkurugenzi wa Kampuni ya Celebi Tanzania Aviation Services Ltd inayojihusisha na utoaji huduma za ndege, mizigo na abiria, Gaudence Temu alisema ujio wa ndege mpya unaliongezea shirika uwezo wa nafasi nzuri ya kutoa huduma ndani na nje ya nchi.

Alisema shirika hilo linapoimarika wanategemea hata sekta zingine zinazotegemea eneo hilo kama utalii kukua kwa kasi, huku akieleza hata nchi zinazofanya vizuri katika utalii zimekuwa zikifanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya usafiri wa anga unaotajwa ndio salama zaidi.

‘‘Kuwa na ndege nyingi maana yake ni kuwa na uwezo wa kufikia vituo vingi zaidi, hivyo kuchechemua biashara na hivyo kukuza uchumi,” alisema.

Gaudence alisema shirika hilo halina budi kudumisha na kuendeleza rekodi nzuri ya kiusalama kwa sababu tangu wameanza shughuli zao hakujawahi kutokea changamoto kubwa.

“Waendelee kujiimarisha kwenye matengenezo na shirika linapokuwa na ratiba nzuri na za uhakika na kwa mwendelezo, abiria wanajenga imani nalo,” alisema

Alisema iwapo suala la ratiba kama halitazingatiwa na kuwa na mwendelezo, abiria watashindwa kulitumia.

“Usafiri wa ndege ni biashara, ina maana wewe unapojiimarisha, unatangaza vita na washindani wako nao watajizatiti kushindana na wewe, ”alisema.

Katika maelezo yake alisema hata kuchagua njia wanapaswa kuzingatia kwa umakini kwa kujiridhisha kweli kuna uhitaji wa kupeleka abiria na kisha kupata faida.

“Kwa kuwa hii ni biashara lazima wazingatie kuchunga gharama za uendeshaji, lazima ziwe katika kiwango kinachokubalika na kurudisha kile kilichowekezwa na kwenda na matarajio ya Serikali,” alisema.

Mtaalamu na mshauri wa usafiri wa anga kwa zaidi ya miaka 20, Jimi Nangawe alisema ujio wa ndege hiyo, unatarajia kuziba pengo la ndege ambazo zilikuwa hazifanyi kazi na kwenda kuziba njia ambazo zilikuwa zimesimama.

“Nategemea shirika sasa litaanza kupata faida na zile hasara zianze kuondoka na Serikali iwaache wafanye kazi zao kwa uhuru bila kuingiliwa na kuepuka kuingiza mambo ya kisiasa badala ya kibiashara,” alisema Nangawe

Nangawe ambaye amewahi kufanya kazi Precision Air, Rwanda Air na Uganda Air , alisema anachotarajia kukiona kutoka kwa Serikali, ni kulipatia shirika hilo malengo ili lianze kutengeneza faida baada ya muda mrefu.