Alichokibaini CAG ndege za ATCL

Muktasari:

  • Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yam waka 2021/22 imewasilishwa bungeni ikionesha upungufu kwa baadhi ya maeneo ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Moshi. Nini kinalitafuna Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hili ndio swali kuu linalotawala vichwa vya Watanzania, baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kubainisha upungufu kibao.

 Katika ripoti hiyo ya ukaguzi kwa mwaka 2021/2022 iliyowasilishwa bungeni leo Alhamisi, Aprili 6, 2023, CAG licha ya kueleza kuwa shirika hilo limepata hasara kwa miaka mitano mfululizo, pia amebaini madudu katika uendeshaji wa ndege hizo.

CAG anasema katika ukaguzi wake, alibaini ndege mbili za Airbus A220-300 (5H-TCH & 5H-TCI) na Bombardier Q400 zilikuwa hazifanyi kazi kwa muda wa siku 2 mpaka 220 kuanzia Julai 1,2021 hadi 30 Juni 2022.

“Hii ni kwa sababu ya utendaji duni wa ndege ya Airbus A220-300 na huduma dhaifu za baada ya mauzo za kuhakikisha ndege inafanya kazi kama vile huduma za kwenye injini,”inasema taarifa hiyo ya CAG Charles Kichere.

Kwa mujibu wa CAG, uchambuzi wa kifedha umeonesha kuwa ndege zisizotumika zimesababisha kampuni kuingia gharama zisizobadilika kutokana na kukodi na bima jumla ya Sh5.27 bilioni na kukosa mapato ya SH 20.35 bilioni.

“Mapato hayo yangeweza kupatikana endapo ndege ingefanya kazi kwa mwaka mmoja tangu 1 Julai 2021 hadi 30 Juni 2022. Hali hii imeathiri sana ukwasi na sifa ya kampuni, pia kuongezeka kwa idadi ya ratiba za safari za ndege zilizofutwa,” amesema

Katika ukaguzi huo pia, CAG alibaini ndege ya Boeing 787-8 ilizalisha mapato ya Sh45.67 bilioni na kuwa na gharama ya Sh70.57 bilioni ambayo ilisababisha hasara ya Sh24.9.bilioni, hali inayozidi kuibua maswali kuhusu ufanisi wa Shirika.

Ukaguzi ulibaini ndege hizo zilisababisha gharama zisizobadilika za shilingi bilioni 5.06 kama gharama za matengenezo ambazo hazikuwa na mapato yanayolingana kutokana na kutofikia masaa ya ndege yanayoweza kutozwa kiwango cha chini.

Mbali na madudu hayo, gharama za ziada za Sh19.11 bilioni zilizotumiwa na ATCL kutokana na Wakala wa Ndege za Serikali Tanzania kutotekeleza majukumu ya kimkataba, na hii ni kwa mujibu wa taarifa hiyo ya CAG Kichere.

Ndani ya mwaka 2021/22, ATCL ilikodi ndege 11 kutoka kwa Wakala wa Ndege za Serikali ya Tanzania, hivyo kutozwa gharama za matengenezo za dola za Marekani 496 kwa saa moja kwa utendaji kazi wa injini.

Pia, ilitozwa dola za Marekani 360 kwa maisha ya injini ya mzunguko wa ndege, na kwa mwaka 2021/22 zilifikia Sh25.39 bilioni, kiasi hicho kinakusudiwa kwa matengenezo ya ndege wakati zinaharabika kulingana na mkataba.

Kampuni hiyo pia iliingia gharama ya Sh19.11 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya ndege katika mwaka huo, ambayo ni sehemu ya akiba ya matengenezo chini ya mkataba wa Wakala wa Ndege wa Serikali ya Tanzania.

Ndege za abiria za ATCL zimebainika kuchelewa kuondoka kwa wastani wa asilimia 25 kati ya lengo lililowekwa chini ya mpango mkakati wa Kampuni ya Ndege Tanzania ni kufikia kiwango cha asilimia 92 cha ndege kuondoka.

Asilimia 96 ya tiketi za ndege za ATCL zilibatilishwa au kufutwa na ATCL au mawakala nilibainika kulikuwa na tiketi 38,455 zilizofutwa mwaka 2021/22, ambapo asilimia 4 zilifanywa na ATCL na asilimia 96 zilifanywa na mawakala.

Pia CAG alibaini kulikuwa na tiketi 479 zilizofutwa baada ya tarehe ya kutumika tiketi hiyo kinyume na ilivyoelezwa katika Miongozo ya Shirikisho la Kimataifa la Usafiri wa Anga.

“Nina mashaka dadi kubwa ya tiketi zilizofutwa zinapelekea kupoteza mapato kwa sababu wakati mwingine wateja hawawezi kupata tiketi kwani mfumo huonesha ndege zimejaa wakati kiuhallisia ndege zinakuwa bado zina nafasi.

“Ninapendekeza kuwa Kampuni ya Ndege Tanzania iboreshe mifumo ya udhibiti ya ndani kuhusu utaratibu wa kufuta tiketi ikiwa ni pamoja na kuweka masharti na ukomo wa kufuta tiketi kwa mawakala wa safari.” amependekeza CAG.