Atuhumiwa kumg’oa jino, kumtoboa jicho mpenzi wake Arusha

Jackline Mnkonyi (38), mkazi wa jijini Arusha anayedaiwa kung'olewa jino na kutobolewa jicho na mpenzi wake.

Arusha. Isaack Mnyagi mkazi wa Sombetini jijini Arusha anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumpiga mwenza wake, Jackline Mnkonyi (38) na kisha kumng’oa jino la mbele na kumtoboa jicho.

Tukio hilo limetokea juzi Alhamisi Mei 25, 2023 baada ya kutokea ugomvi ambao unadaiwa kuchangiwa na wivu wa mapenzi baina ya wenza hao.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa wazazi wake eneo la Sinoni ,Daraja Mbili jijini Arusha, Jackline ambaye anamtoto mchanga amesema amepigwa na mumewe baada ya kumtuhumu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mgeni aliyefika nyumbani bila kujua Kama ni mjomba wake.

Amesema Mei 23, 2023 alitembelewa na Mjomba wake, Vicenti Matai kutoka mkoani Simiyu kwa lengo la kumsalimia baada ya kuondoka mgeni huyo mume wake saa 4.45 usiku alianza kumuhoji

Jackline amesema alimweleza Mgeni huyo alikuwa na mjomba wake lakini mumewe alikataa na ndipo alipoanza kumshambulia kwa ngumi, mateke na mkanda na baadaye alichukua Praizi na kumng'oa jino kwa nguvu.

"Nilijitahidi sana kujieleza lakini ilishindikana alianza kunipiga kwa mateke na ngumi na alichukua Praizi na kuniamuru nifungue mdomo na kuning’oa jino moja ambapo damu zilianza kuchuruzika,”amesimulia kwa uchungu huku akilia.

Amesema licha ya kipigo hicho pia alichukua kitu chenye ncha kali na kumtoboa jicho moja ambalo hadi sasa hawezi kuona huku akimwambia maneno mazito na kumtishia kumuua.

Amesema baada ya tukio hilo alimchukua na kumpeleka nyumbani kwa wazazi wake Sinoni Daraja mbili na kumtumpa getini.

Naye baba mzazi wa Jackline, Elimilis Mnkonyi amesema siku ya tukio wakiwa nyumbani  saa saba usiku walipokea simu kutoka kwa mwanaume huyo akiwataka wakachukue mzoga wao hapo nje.

Amesema akiwa na mke wake, walienda getini na kumkuta mtoto wao Jackline akiwa hajitambui na kuamua kumpeleka katika hospital ya Rufaa ya Mount Meru na baadaye alienda kutoa taarifa kituo cha polisi kupitia jalada namba ARS/RB/5416/2023.

"Baada ya kutoa taarifa polisi tulienda kumtafuta mtuhumiwa lakini ametoroka na polisi wanaendelea kumtafuta,"amesema

Mnkonyi amesema mtoto wake huyo alikuwa ameolewa  na mume wa ndoa lakini walitengana na kuamua kuishi na mwanaume huyo wa sasa ambaye ndiye amemfanyia ukatili huo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Justin Masejo amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kumtafuta mtuhumiwa.

"Tunamtafuta aliyefanya uhalifu huu na akipatikana hatua za kisheria zitachukuliwa"amesema.