Babu atuhumiwa kuwaua wajukuu zake kwa kuwaponda vichwa

Songwe. Polisi mkoani Songwe limemkamata, Aloyce Nyabwanzo (53), Mkazi wa Kitongoji cha Kikamba, Kijiji cha Kapalala wilayani, Songwe kwa tuhuma za kuwaua wajukuu zake wawili kwa kuwapasua mafuvu ya kichwa na mchi wa kutwangia hadi ubongo kumwagika.

 Kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya amesema tukio hilo lilitokea Aprili 30, 2023 majira ya saa 5:00 alfajiri na kwamba jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kujua sababu za mtuhumiwa kutenda tukio hilo.

Amesema mtuhumiwa alitumia mbinu ya kuwavizia wajukuu zake hao wakati wanatoka chumbani kwao kumfuata bibi yao sebuleni aliyekuwa anajaribu kuzuia mlango usivunjwe na mtuhumiwa huyo baada ya kuanzisha vurugu nyakati hizo za usiku.

“Marehemu wamefanyiwa uchunguzi na daktari na kubaini kuwa vifo vyao vimesababishwa na kupasuka kwa mafuvu ya vichwa baada ya kupigwa na kitu kizito hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi na ubongo kutoka nje,” amesema Kamanda Mallya.

Amewataja marehemu hao kuwa ni Jackson Chacha (2) na George Chacha (5) wote wakazi wa kitongoji cha Iwindu- Kikamba katika Kijiji cha Kapalala na walikuwa wakilelewa na mtuhumiwa.

Hata hivyo, Kamanda Mallya amesema wakati uchunguzi wa kujua sababu zilizosababisha mtuhumiwa kutenda tukio hilo, mtuhumiwa atapelekwa hospitali ili kupimwa afya ya akili.

Wakati huohuo kufuatia tukio la kufyekewa shamba la kahawa la Mariamu Kalupande, watu Tisa (9) wanashikiliwa na polisi.

Kamanda Mallya amesema mali iliyoharibiwa ina thamani ya zaidi ya Sh.63.5milioni

Amesema waliokamatwa ni walinzi sita na watumishi wengine 3, inadaiwa eneo hilo lina mgogoro kati ya familia ya Kalupande na Shirika la Akina Mama na watoto.

Katika tukio lingine mtu mmoja amekamatwa katika mpaka wa Tunduma akiwa anasafirisha madawa ya kulevya aina ya Bangi yenye uzito wa gramu 80.34.

Kamanda Mallya amesema mtuhumiwa huyo ni kondakta wa basi ambalo lilikuwa lilitokea nchini Zimbabwe.