Atuhumiwa kuwalawiti wanafunzi 18

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mkazi wa kijiji cha Komela, wilayani Moshi mkoani hapa, Shukuru Nguma kwa tuhuma za kuwalawiti kwa nyakati tofauti wanafunzi 18 wa shule tofauti za msingi kijijini hapo.

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mkazi wa kijiji cha Komela, wilayani Moshi mkoani hapa, Shukuru Nguma kwa tuhuma za kuwalawiti kwa nyakati tofauti wanafunzi 18 wa shule tofauti za msingi kijijini hapo.

Nguma anadaiwa kuwalawiti wanafunzi hao wa kiume ambao ni kuanzia darasa la kwanza hadi la tano kwa kuwapa pipi na fedha.

Akizungumzia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda alisema kijana huyo alikamatwa Januari 21, baada ya kuzagaa kwa taarifa hizo ambapo timu ya uchunguzi ilitumwa kijijini hapo kujiridhisha na kubaini ukweli wa tuhuma hizo.

“Huyu mtuhumiwa tayari tunaye, tumefuatilia tumebaini ni kweli baada ya kutuma timu yetu kuchunguza na Serikali tayari imeshachukua hatua, ikiwemo kumkamata, kwa ngazi ya wilaya tumeshakamilisha taratibu zote ili tumfikishe mahakamani,” alisema.

Kayanda alisema kijana huyo sio mara yake ya kwanza. Akiwa na miaka 17 aliwahi kukamatwa na kuhukumiwa kifungo cha nje.

“Yeyote atakayebainika kufanya vitendo vya namna hiyo kwa watoto wetu wa shule, iwe chekechea, shule ya msingi au sekondari hatutamwacha, tutamkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, ili tukomeshe tabia za namna hii ambazo hazifai katika jamii yetu,” alisema.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa aliungana na mkuu huyo wa mkoa akisema kuna taratibu zinaendelea ikiwemo kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo.

“Ni kweli mtuhumiwa huyo anashikiliwa katika kituo cha Polisi Himo na taratibu za kisheria zitakapokamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Maigwa.

Mmoja wa walimu wa shule hizo, (kimaadili hakutaka jina lake liandikwe gazetini) alisema huwa kila siku wana utaratibu wanafunzi wakiwa mstarini kabla ya kuingia darasani wanazungumza na wanafunzi kama kuna aliyefanyiwa kitendo kibaya ajieleze.

“Huwa tunatoa elimu kila siku kuhusu mambo ya ulawiti wakiwa mstarini kabla ya kuingia darasani, tunaongea nao na kama kuna mtoto aliyewahi kufanyiwa kitendo kama hicho ajitokeze, ghafla mmoja akaanza kunyoosha kidole na kutaja wenzake na akasema anafanyiwa na mtu fulani,” alisema.

“Baada ya hapo tukaita wazazi wao tukawaeleza na inaonekana ni kitu ambacho kilishawahi kutokea tena hapo nyuma na kwa baadhi ya wazazi wanafahamu, tulikaa na wazazi tukawaeleza madhara ya hivyo vitendo kwa hao watoto, wakasema wanachukua hatua za kisheria na wakaondoka na sisi tukaendelea na majukumu mengine,” alisema mwalimu huyo ambaye shuleni kwake wanafunzi sita wameshafanyiwa vitendo hivyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa vitendo hivyo, walikiri kuwapo kwa matukio hayo.

“Kama mzazi nimeumia sana kwa sababu mara nyingi niko karibu sana na mwanangu, lakini cha kushangaza wakati anafanyiwa kitendo kama hicho hasemi, baada ya walimu kutuita shuleni nilimuita mwanangu na kumuuliza ilikuwaje, akasema kijana huyo akishawafanyia kitendo hicho huwatishia wasiwaambie wazazi wao na kuwapa fedha na wakati mwingine pipi.

“Tunaomba huyu kijana awajibishwe kwa namna yoyote ile maana anatumalizia watoto wetu jamani, hii dunia tunaenda wapi maana huu ukatili ni mkubwa na ni wa kinyama katika jamii,” alisema mzazi huyo, ambaye jina lake limehifadhiwa.Mzazi mwingine wa kijiji hicho, alisema kuwa licha ya kuwa karibu sana na watoto wake anashangaa tukio kama hilo kufanyika, na hawajui ni mbinu gani mtuhumiwa anazotumia kuwafanyia ukatili watoto wao.

Mzazi mwingine ambaye pia jina lake limehifadhiwa kimaadili, alisema kuwa taarifa zilizopo kijana huyo amekuwa akifanya vitendo hivyo mara kwa mara.

Alisema kuna taarifa aliwahi kufungwa kifungo cha nje kwa kufanya vitendo kama hivyo. “Naona sasa wakati umefika mtuhumiwa kuchukuliwa hatua stahiki, maana inaonekana ameshazoea na atawaumiza wengi asipochukuliwa hatua kali,” alisema mzazi huyo.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Komela, Anord Mtui alikiri kuwepo kwa matukio kama hayo katika kijiji hicho na kusema kuwa kijana huyo amekuwa ni tishio kutokana na matukio anayoyafanya.

“Huyu kijana hapa kijiji kwetu kwa sasa hivi inaonekana amelawiti watoto 18 na hata alipokamatwa juzi alikiri yeye mwenyewe kwa kinywa chake kwamba amekuwa akifanya matukio hayo, na sio mara ya kwanza kufanya hivyo,” alisema.