Prime
Mahakama yawaachia huru makada wa ACT Wazalendo walioshitakiwa kwa mauaji
Muktasari:
- Uamuzi huo umetolewa Julai 10, 2026 na Jaji Augustine Rwizile wakati akitoa uamuzi wa kama washtakiwa walikuwa na kesi ya kujibu.
Kigoma. Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma imewaachia huru makada watatu wa Chama cha ACT-Wazalendo waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la mauaji bila kukusudia ya kada mwenzao, Jinasa Manabi, baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha unaowahusisha na tukio hilo.
Walioachiwa huru ni pamoja na Julius Yotham Mpwehuka, aliyekuwa mgombea udiwani wa ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Daniel Gize na Stanlaus Ngadigadi.
Uamuzi huo umetolewa Julai 10, 2026 na Jaji Augustine Rwizile wakati akitoa uamuzi wa kama washtakiwa walikuwa na kesi ya kujibu.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Manabi alifariki dunia Oktoba 29, 2025 baada ya kudaiwa kushambuliwa katika makazi ya Mpwehuka yaliyopo Kijiji cha Asante Nyerere, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa siku ya tukio, wanachama hao wa ACT-Wazalendo walikuwa wamekusanyika nyumbani kwa Mpwehuka kwa ajili ya kuwateua mawakala wa vituo vya kupigia kura kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Ilidaiwa kuwa wakati wa mkutano huo, Manabi alituhumiwa na baadhi ya wajumbe kuwa alikuwa akitoa taarifa za chama kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Baada ya tuhuma hizo, alisimama na kujaribu kuondoka, lakini inadaiwa alishambuliwa kwa kupigwa na kusukumwa hadi akaanguka na kushindwa kusimama tena.
Mahakama ilielezwa kuwa baadaye ofisa mtendaji wa kata alipata taarifa kuhusu tukio hilo na kuwasiliana na polisi, ambao walifika eneo la tukio na kuwakuta watu kadhaa wakiwa ndani ya nyumba hiyo, pamoja na Manabi akiwa amejeruhiwa vibaya.
Alipelekwa hospitali kwa matibabu baada ya kupewa fomu ya PF3, lakini baadaye alifariki dunia.
Uchunguzi wa mwili uliofanywa ulionesha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa jeraha kubwa la kichwani lililosababisha uharibifu wa ubongo.
Katika ushahidi wake, daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili alithibitisha kuwa majeraha ya kichwa ndiyo yaliyosababisha kifo cha Manabi.
Shahidi mwingine wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi Charles Mwanjoba, aliiambia Mahakama kuwa alipokea taarifa kutoka kwa ofisa mtendaji wa kata kuhusu vurugu zilizokuwa zikitokea nyumbani kwa Mpwehuka.
Alisema yeye na askari wenzake walipofika eneo hilo walilazimika kutumia mabomu ya machozi baada ya mlango wa nyumba hiyo kushindwa kufunguliwa.
Walipoingia, walimkuta Manabi amelala chini akiwa katika hali mbaya, huku watu wengine waliokuwa ndani ya nyumba hiyo wakikamatwa kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, watu waliokuwa eneo la tukio walidai kuwa marehemu alishambuliwa baada ya kutuhumiwa kuwa mtoa taarifa wa CCM.
Shahidi wa tatu, Koplo Malogo, aliyekuwa mpelelezi wa kesi hiyo, aliiambia Mahakama kuwa awali watu 10 walikamatwa kuhusiana na tukio hilo, lakini baada ya uchunguzi, watano walifikishwa mahakamani na baadaye watatu pekee ndio waliendelea kushtakiwa.
Alisema uamuzi wa kuwafungulia mashtaka washtakiwa hao ulitokana na maelezo ya mashahidi wawili waliodaiwa kushuhudia tukio hilo, Damas Charles na Hamisi Athman.
Hata hivyo, Mahakama ilielezwa kuwa mashahidi hao muhimu hawakufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa, na wakati wa usikilizwaji wa kesi, mahali walipokuwa hapakujulikana.
Akitoa uamuzi wake, Jaji Rwizile alisema hakuna ubishi kuwa Manabi alifariki dunia kutokana na jeraha kubwa la kichwani, kama ilivyobainishwa katika ripoti ya uchunguzi wa mwili.
Hata hivyo, alisema suala muhimu lililopaswa kuamuliwa na Mahakama lilikuwa kama kulikuwa na ushahidi wa kuaminika unaowahusisha washtakiwa na shambulio lililosababisha kifo hicho.
Jaji alisema hakuna shahidi aliyeshuhudia tukio hilo aliyefika mahakamani kutoa ushahidi wa moja kwa moja dhidi ya washtakiwa.
Alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi wa polisi ulitokana na taarifa walizopewa na watu wengine ambao hawakufika mahakamani, hivyo ulikuwa ushahidi wa kusikia (hearsay), ambao haukubaliki kisheria kuthibitisha hatia ya mtu.
Aidha, alisema upande wa mashtaka pia haukumwita ofisa mtendaji wa kata aliyepokea taarifa za awali kuhusu tukio hilo, hivyo Mahakama haikujiridhisha kuhusu chanzo cha taarifa hizo.
"Ni kanuni ya sheria kwamba pale upande wa mashtaka unaposhindwa kuwaita mashahidi muhimu ambao ushahidi wao ni wa lazima kuthibitisha shtaka, Mahakama inaweza kufikia hitimisho kwamba ushahidi huo usingeuunga mkono upande wa mashtaka," alisema Jaji Rwizile.
Aliongeza kuwa hitimisho la mpelelezi wa kesi lilitokana na maelezo ya mashahidi ambao hawakutoa ushahidi mahakamani, hivyo halikuweza kuthibitisha ushiriki wa washtakiwa katika kosa walilokuwa wakikabiliwa nalo.
Kutokana na upungufu huo, Mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuanzisha kesi dhidi ya washtakiwa.
"Kwa msingi huo, Mahakama inaamua kuwa washtakiwa wote hawana kesi ya kujibu na wanaachiwa huru," alisema Jaji Rwizile katika hukumu yake.