Atupwa jela maisha kwa kumnajisi mtoto wa miaka minane

Muktasari:

  • Tukio hili lilitokea majira ya jioni na mtoto alikuwa anacheza eneo karibu na kanisa, mshtakiwa alimfuata akiwa ameshika soda na kumpa, kisha akaondoka naye hadi kichakani na kumbaka.

Mufindi. Mahakama ya Wilaya Mufindi imemhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela, mkazi wa Kijiji cha Tambarang’ombe, Kata ya Malangari, Kheri Lutamo (25) baada ya kupatikana na hatia kwa kosa la kumbaka mtoto wenye umri wa miaka minane.

Hukumu hiyo imetolewa Machi 18, 2024 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Sekela Kyungu na nakala yake kupatikana leo Machi 28, 2024.

Mshtakiwa huyo ameshtakiwa kwa kosa moja la ubakaji, kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 rejeo la mwaka 2022.

Akisoma hukumu hiyo, Kyungu amesema ilielezwa mahakamani hapo kwamba Februari 25, 2024 katika Kijiji cha Tambarang’ombe mkoa wa Iringa, mshtakiwa alimbaka mtoto huyo wakati alipokuwa akicheza karibu na eneo la kanisa liliopo kijiji humo.

“Majira ya jioni, mwathirika akiwa anacheza eneo karibu na kanisa, mshtakiwa alimfuata mtoto huyo huku akiwa ameshika soda na kumpa,” amesema hakimu huyo.

Ameongeza kuwa baada ya mshtakiwa kumpa soda mtoto huyo, alimshika mkono na kuondoka naye kwenda kichakani na walipofika huko alimvua nguo kisha kumbaka mtoto huyo,” ameeleza Kyungu.

Mshtakiwa huyo baada ya kumaliza kitendo hicho, alikimbia na mtoto alipoulizwa alimtaja mshtakiwa huyo, kuwa ndiye aliyemfanyia kitendo hicho.

Baadaye alipokamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Malangali.

Amesema Machi 18, 2024 mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa shtaka lake na alikiri kutenda kosa hilo.

Baada ya mshtakiwa kukiri kosa Mahakama ilimkuta na hatia kwa mujibu wa kifungu cha 228(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura 20, rejeo la mwaka 2022.

Hivyo, mahakama imetoa adhabu ya kifungo cha maisha jela chini ya kifungu 131(3) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 rejeo la mwaka 2022.

Awali, mwendesha mashtaka wa polisi, Ahmed Magenda aliomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa jamii kutokana na matukio hayo kukithiri wilayani humo.