Muuza maziwa jela maisha kwa ubakaji

Muktasari:

  • Alifanya kitendo hicho chini ya mwembe na kumtishia mwanafunzi aliyembaka kuwa akienda kusema atamdhuru.

Kibaha. Mkazi wa Kibaha, mkoani wa Pwani, Said Sadick Said (23) amehukumiwa kwenda jela maisha, baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa shule ya msingi Maendeleo iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, mwenye umri wa miaka (8).

Hukumu hiyo imetolewa jana Jumatatu Januari 8, 2024 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Fahamu Kibona, baada ya mahakama hiyo kujiridhisha na ushahidi uliotolewa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo ya jinai namba 66 ya mwaka 2023.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, mahakama ilimpa mshtakiwa huyo nafasi ya kujitetea kwanini asipewe adhabu kali, nafasi ambayo aliitumia kueleza kuwa kwanza hajui kama ana kesi na pia hajui chochote kuhusu kesi hiyo.

"Mshtakiwa kwanini mahakama isikupe adhabu kali kulingana na kosa hili?" Hakimu aliuza.

"Mheshimiwa mimi sijui kama nina kesi sijui, sijui kabisa, mimi siwezi kufanya kitendo hicho kwakuwa mimi mwenyewe nina familia na nina watoto wa kike," alijitetea mtuhumiwa huyo, ambaye alisindikizwa na mkewe mwenye mtoto mchanga kisha wote kwa pamoja wakaanza kububujikwa na machozi.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu huyo, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kuanzia Januari hadi Septemba mwaka 2023 katika Mpiji – Kibaha na kwamba kwa mujibu wa sheria, anapaswa kwenda jela maisha.

Amesema mama mzazi wa mwanafunzi ndiye aligundua jambo hilo baada ya kukuta haja kubwa kwenye moja ya nguo za ndani za mwanafunzi huyo na akamuuliza kuhusiana na hali hiyo.

"Baada ya mama mzazi kukuta haja kubwa kwenye nguo ya mwanafunzi huyo, alimuuliza kuhusu hali hiyo awali alikanusha na baadaye alimueleza mama yake kuwa hiyo imetokana na kubakwa na muuza maziwa na kutaja jina," amesema.

Amesema kuwa mwanafunzi huyo alisema siku ya kwanza mtuhumiwa alikutana na mwanafunzi huyo aliyekuwa akielekea kwa rafiki yake, ambapo alimshika mkono na kumvutia chini ya mwembe kisha kuanza kumbaka na alipofanikisha unyama huo alimtishia kuwa asiseme kwa mtu yoyote.

Kwa mujibu wa hakimu huyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano ambao ni mwanafunzi aliyeathirika na kitendo hicho, mama wa mwanafunzi huyo, mpelelezi wa kesi, daktari na askari aliyemkamata mtuhumiwa huyo.

Hakimu Kibona alieleza kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili wawili ambao ni Elizabeth Olomi, akisaididana na na Neema Kwayi.

Wakizungumza nje ya mahakama baadhi ya wakazi mkoani humo wamesema kuwa hakumu hiyo itaongeza woga kwa baadhi ya watu wenye tabia hiyo, kwa kuwa kitendo hicho kinaathiri watoto ambao ndio nguvu kazi ya Taifa kwa miaka ijayo.

"Kama ni kweli ametenda kosa hilo mwache aende ni haki yake naamini wengine watajifunza kupitia kwake," amesema Philipo Meshaki ambaye ni mkazi wa Kibaha.