Tisa wafikishwa kortini wakituhumiwa kubaka wanafunzi 17

Muktasari:

  • Tukio la kubakwa wanafunzi hao wa shule za Boma na Hai Day linadaiwa kutokea siku ya mkesha wa Mwenge wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Septemba 28, 2018 na tayari watuhumiwa hao tisa wamefikishwa mahakamani

Hai. Wakati Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro likiongeza kasi ya uchunguzi wa tukio la kubakwa na kulawitiwa wanafunzi 17 siku ya mkesha wa Mwenge wilayani hapa, watu tisa wamefikishwa kortini kwa tuhuma hizo.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani Ijumaa iliyopita, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Hai, Devotha Msoffe na kukana mashitaka yao na kurudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini, kupanua uchunguzi wao na kugusa shule zote nchini, ili kubaini ukubwa wa tatizo la ubakaji na ulawiti wa wanafunzi.

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo Ijumaa mbele ya hakimu mkazi Msoffe, mwendesha mashtaka wa polisi, Hawa Hamisi alidai watuhumiwa hao ambao ni madereva wa Bodaboda na Bajaji walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti wilayani humo.

Mwendesha mashtaka huyo alidai  kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na dhamana kwa tuhumiwa iko wazi kwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja ambaye ameajiriwa sehemu inayotambulika pamoja na barua ya uthibitisho wa ajira yake ikiambatana na barua kutoka ofisi ya kijiji au mtaa.

Hata hivyo, watuhumiwa wote kwa pamoja wamekana tuhuma hizo na pia walishindwa kukidhi vigezo hivyo vya dhamana na kupelekwa mahabusu hadi Oktoba 16, 2016 wakati kesi hiyo itakapotajwa tena.

Wakati watuhumiwa hao wakifikishwa mahakamani, jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linaendelea kuwasaka washukiwa wengine waliotajwa katika sakata hilo.