Prime
KESI YA MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA: Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa- 7

Muktasari:
- Wakati, baadhi ya washtakiwa wakijitetea walitoa utetezi ambao katika lugha ya kisheria unaitwa ‘Alibi’ ni kutetezi unaoeleza kuwa, siku na tukio hakuwepo eneo husika.
Dar es Salaam. Baada ya Jamhuri kufanya uchambuzi wa ushahidi wake na kuthibitisha viini vyote vitatu vya kosa la mauaji, sasa inahitimisha hoja zake kwa kuchambua udhaifu wa utetezi wa washtakiwa katika kesi hii.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) na Nicholous Kisinza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Marco Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi, John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi )na Salim Mbalu alikuwa Koplo.
Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara.
Wakati, baadhi ya washtakiwa wakijitetea walitoa utetezi ambao katika lugha ya kisheria unaitwa ‘Alibi’ ni kutetezi unaoeleza kuwa, siku na tukio hakuwepo eneo husika.
Jamhuri ilivyokosoa utetezi wa ‘Alibi’
Jamhuri katika hoja zake za mwisho baada ya pande zote kukamilisha ushahidi wake, iliupinga utetezi wa ‘Alibi’ na kubainisha udhaifu wake unaufanya usiwe na maana.
Hivi ndivyo Jamhuri ilivyowasilisha hoja hizo:
“Mheshimiwa Jaji, utetezi wa ‘Alibi’ uliowasilishwa na washtakiwa kwa heshima kubwa, tunawasilisha kuwa ni dhaifu kwa sababu zifuatazo, mosi, washtakiwa hawakudai kuwa mbali na eneo la tukio.
“Mheshimiwa Jaji, Mahakama ya Rufani katika kesi ya Msafiri Benjamin dhidi ya Jamhuri ambayo ni rufaa ya jinai namba 549 ya 2020, iliyoamuliwa Agosti 27, 2021 ilifafanua maana ya ‘Alibi’ kuwa:
“Alibi ni neno la Kilatini linalomaanisha mahali pengine au sehemu nyingine; hivyo, iwapo mshtakiwa atadai hakuwepo mahali kosa lilipotendeka na alikuwa sehemu nyingine mbali kiasi kwamba asingeweza kuwa na hatia, basi atakuwa ameweka ‘Alibi.’
“Januari 5, 2022 haipingiki kwamba washtakiwa wote walikuwa Wilaya ya Mtwara na wanapinga tu kuwa hawakuwa Kituo cha Polisi Mitengo.
“Aidha, mchana wa tarehe hiyo mshtakiwa wa kwanza, Kalanje anadai alikuwa Kituo cha Polisi Nanyamba na mshtakiwa wa pili, Onyango anadai alikuwa katika Kituo cha Polisi Mtwara, maeneo ambayo si mbali na Kituo cha Polisi Mitengo ambako kosa lilitendeka.”
Washtakiwa walitambuliwa
Hoja ya pili ya Jamhuri ni kwamba washtakiwa walitambuliwa eneo la tukio.
“Mheshimiwa Jaji, utetezi wa ‘Alibi’ uliotegemewa na shahidi wa kwanza wa utetezi, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, Kalanje na shahidi wa pili wa utetezi ambaye ni mshtakiwa wa pili, Onyango hauna maana yoyote.
“Hii ni kwa sababu walitambuliwa vyema eneo la tukio na mashahidi namba 5,23 na 25 wa upande wa mashtaka na shahidi wa tano wa utetezi ambaye ni mshtakiwa wa tano, Mkaguzi wa Polisi Msuya.
“Mahakama ya Rufani katika kesi ya Denis Frank Tarimo maarufu kwa jina la Novat na mwingine dhidi ya Jamhuri katika rufaa ya jinai namba 140 ya 2021 iliyoamuliwa Juni 11, 2024) ilisema kama ifuatavyo:
“Sasa, katika sheria, hitimisho ni kwamba washtakiwa walitambuliwa vyema eneo la tukio linavunja utetezi wa ‘Alibi’ na kubaki ni hali ya ubatili mtupu, mwisho wa kunukuu sehemu ya uamuzi huo wa Mahakama.”
‘Alibi’ haikusemwa mapema
“Mheshimiwa Jaji, ‘Alibi’ ya washtakiwa haikuwekwa wazi awali kwa ofisa aliyefanya uchunguzi wa kesi hii na jina la sehemu walizodai kuwepo halikuoneshwa mapema kwa upande wa mashtaka au Mahakama kabla ya usikilizaji kuanza.
“Bali ‘Alibi’ hiyo imewekwa baadaye kwa mara ya kwanza mahakamani kama ilivyowekwa katika kesi ya Kubezya John dhidi ya Jamhuri, rufaa ya kinai Na. 488 ya 2015 ikinukuu uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Uganda katika kesi ya Kibale dhidi ya Uganda [1999] 1 EA 148 ambapo Mahakama ilisema:
“Alibi ya kweli, bila shaka, inatarajiwa kufichuliwa kwa polisi wanaochunguza kesi au upande wa mashtaka kabla ya usikilizaji.
“Ni pale tu inapofanyika hivyo, ndipo polisi au upande wa mashtaka watakapopata fursa ya kuthibitisha Alibi hiyo,” ilieleza Jamhuri.
“Alibi iliyowekwa kwa mara ya kwanza wakati wa usikilizaji na mshtakiwa kuna uwezekano mkubwa ni wazo lililobuniwa tu baadaye baada ya tukio.”
‘Alibi’ haikuthibitishwa
Katika hoja yake ya nne, Jamhuri iliegemea hoja kuwa ‘Alibi’ haikuthibitishwa.
Katika utetezi wake, mshtakiwa wa kwanza, Kalanje, alidai kuwa siku na wakati wa tukio alikuwa Kituo cha Polisi Nanyamba wakati kosa likitendeka na alikuwa na polisi wakifundishwa jinsi ya kushughulikia dharura.
“Lakini hakufanya jitihada yoyote ya kuwaita mashahidi waliokuwa Nanyamba kuthibitisha madai hayo,”ilieleza Jamhuri katika wasilisho lake.
“Mshtakiwa wa pili, Onyango pia alidai kuwa alikuwa Kituo cha Polisi Mtwara akitekeleza majukumu yake lakini hakufanya jitihada ya kuwaita mashahidi waliokuwepo kuthibitisha madai hayo.
“Mheshimiwa Jaji, katika kesi ya Maramo Slaa Hofu na wengine watatu dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 246 ya 2011, Mahakama ilinukuu kesi ya Makala Kiula dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai N2 ya 1983 ikisema:
“Iwapo mtu aliyeshtakiwa kwa kosa kubwa anadai kwamba wakati kosa hilo likitendeka alikuwa sehemu nyingine, anafahamika vyema na bado hafanyi jitihada kuthibitisha ukweli huo, ambao kama ni kweli ungethibitishwa kwa urahisi, basi Mahakama italazimika kutilia uzito mdogo madai hayo.”
‘Alibi’ kutokufuata utaratibu
“Mheshimiwa Jaji, tunakiri kwamba mshtakiwa wa kwanza, Kalanje na wa pili, Onyango walitoa taarifa ya kutumia utetezi wa vAlibi wakati wa usikilizwaji wa awali, lakini kwa heshima kubwa tunawasilisha taarifa ya mdomo iliyotolewa, kwamba haikuonesha sehemu wanayodai walikuwepo.
“Hivyo, tunaona hawakutii matakwa ya lazima ya kisheria yaliyoainishwa katika kifungu cha 194(4)(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya 2022, kinachotaka utetezi utoe taarifa au maelezo ya Alibi,” ilieleza Jamhuri.
“Kushindwa kufuata matakwa hayo ya lazima kisheria, Mahakama hii chini ya kifungu cha 194(6) cha sheria hiyo ina mamlaka ya kutoupa uzito wowote.
“Katika kesi ya Mkurugenzi wa Mashtaka dhidi ya Nyangeta Somba na wengine 12 [1993] T.L.R 69, Mahakama pamoja na mambo mengine ilisema lazima taarifa hiyo itoe maelezo ya kutosha ya Alibi ili kuiwezesha Jamhuri kuhakiki ukweli wa maelezo hayo na ikiwezekana kuandaa ushahidi wa kupinga.
“Kwa kuwa taarifa hiyo haikutoa maelezo ya kutosha ya Alibi tunawasilisha kwa heshima kwamba taarifa hiyo haikukidhi matakwa ya kisheria, wameeleza.
“Mheshimiwa Jaji, hata kama utachagua kutumia mamlaka yako chini ya kifungu cha 194(6) cha Sheria hiyo kuikubali, Alibi iliyowekwa, haikufikia kiwango cha kisheria na haikuungwa mkono na mashahidi wengine,”ilieleza Jamhuri.
Jamhuri ilihitimisha hoja zake kwa kuiomba Mahakama iwatie hatiani washtakiwa wote kwa mashtaka ya kuua kwa kukusudia.
Usikose kesho sehemu inayofuata kujua Mahakama ilichokisema