Prime
KESI YA MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA: Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa- 6

Muktasari:
- Washtakiwa saba walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara.
Dar es Salaam. Baada ya kuchambua namna ambavyo ushahidi wake ulivyoweza kuthibitisha viini viwili kati ya vitatu vinavyojenga hatia kwa washtakiwa katika kesi ya mauaji ya muuza madini, sasa Jamhuri inahitimisha na uchambuzi wa ushahidi huo ulivyoweza kuthibitisha kiini cha tatu na cha mwisho.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) na Nicholous Kisinza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Marco Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi, John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi )na Salim Mbalu alikuwa Koplo.
Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara.
Kigezo cha nia ovu
Ili korti imtie hatiani mshtakiwa ni lazima kuwepo na nia ovu ambayo ni kiini cha tatu katika kuthibitisha hatia kwa mshtakiwa wa kesi za mauaji.
Katika kesi hiyo, jamhuri ilieleza Mahakama kuwa ushahidi wake ulithibitisha kiini hicho.
Hivi ndivyo ilivyoanza kujenga msingi kabla ya kuchambua ushahidi huo ulivyothibitisha hilo.
Vigezo au mwongozo wa kutathimini na kubaini nia ya kusababisha kifo viliwekwa wazi na Mahakama ya Rufani katika rufaa ya jinai namba 150 ya mwaka 1994 baina ya Enock Kipela dhidi ya jamhuri iliyotolewa uamuzi Juni 10, 1999, iliposema:
“Kwa kawaida, mshambuliaji hatatangaza nia yake ya kuua au kuleta madhara makubwa. Iwapo alikuwa na nia hiyo, lazima ibainishwe kwa kuzingatia mambo mbalimbali yakiwamo aina na ukubwa wa silaha iliyotumika, nguvu iliyotumika, sehemu za mwili ambazo mashambulizi yalielekezwa, idadi ya mapigo japo pigo moja linaweza kutosha kwa lengo hilo, aina ya majeraha yaliyosababishwa, matamshi ya mshambuliaji kabla au baada ya kuua, na mienendo yake kabla na baada.”
Mauaji yalikuwa na nia ovu
Ilielezwa kuwa, kama ilivyooneshwa na ushahidi ni wazi mauaji yalifanywa kwa nia ovu, kwa kuwa lengo la mauaji lilikuwa kumaliza malalamiko ya marehemu (Mussa) dhidi ya washtakiwa kumpora fedha zake na kuzigawana kama nyara.
Ushahidi wa shahidi wa tano wa utetezi ambaye ni mshtakiwa wa tano, Mkaguzi wa Polisi Msuya, unaonesha mauaji yaliyofanywa na washtakiwa yalitokana na nia mbaya au dhamira ovu.
Matamshi ya baadhi ya washambuliaji kwa Inspekta Msuya kabla ya mauaji na mienendo ya washambuliaji kabla na baada ya mauaji kwa kutupa mwili wa marehemu kichakani, vinaonesha wazi mauaji haya yalifanywa kwa nia ovu.
“Kwa kawaida, kisheria wajibu wa kuthibitisha shtaka ni wa upande wa mashtaka lakini wajibu wa upande wa utetezi ni kutoa ushahidi unaoweza kuibua shaka dhidi ya ushahidi wa jamhuri,” ilieleza jamhuri.
Hivyo, jamhuri katika kesi hii, baada ya kumaliza kuchambua ushahidi wake namna ulivyoweza kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa kwa kujibu viini vyote vitatu vya hatia ya kosa hilo, ulichambua ushahidi wa utetezi kama ulikuwa na uzito.
Katika uchambuzi huo, jamhuri iliupambanisha ushahidi wa utetezi na ushahdi wake kujibu kama uliweza kuutikisa ushahidi wake kwa kuibua shaka au la.
“Mheshimiwa jaji, katika kutathmini kesi ya utetezi, kwa heshima kubwa tunawasilisha kuwa kesi ya utetezi imeshindwa kuibua shaka yoyote katika ushahidi thabiti na wa kuaminika uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka, bali kinyume chake unaoubeba upande wa mashtaka.
“Umejawa utetezi dhaifu wa kutokuwepo eneo la tukio, kutumia Mwongozo wa Utendaji Kazi wa Polisi (PGO) kama kinga, ukwepaji na kukana kwa jumla jumla na uongo kiasi cha kufikia hatua ya kuthibitisha kesi ya upande wa mashtaka
“Mheshimiwa jaji, ni kanuni ya kisheria kwamba iwapo mshtakiwa katika utetezi wake atatoa ushahidi unaoubeba kesi ya mashtaka, basi Mahakama itakuwa na haki ya kuuzingatia ushahidi huo wa mshtakiwa katika kuamua swali la hatia yake.
“Zaidi ya yote, shahidi bora zaidi katika kesi ya jinai ni mshtakiwa anayekiri hatia kwa hiari yake kama ilivyoamuliwa katika kesi ya Hamis Chuma @ Hando Mhoja dhidi ya jamhuri ambayo ni rufaa ya jinai namba 36 ya 2018, iliyoamuliwa na Mahakama ya Rufani Agosti 23, 2021.
“Katika muktadha huu, ushahidi wa mashahidi wa utetezi namba 1,2,3,4,5,6,7 ambao pia ni washtakiwa wa kwanza mpaka wa saba, kwa kiwango kikubwa umeendeleza kesi ya upande wa mashtaka katika shauri hilo la mauaji.
“Haipingiki katika kesi ya utetezi kwamba, Mussa Hamis aliporwa (na washtakiwa) fedha zake, shilingi za Kitanzania na dola za Marekani akiwa Sadina Lodge Mtwara na (kijijni kwao) Luponda, Nachingwea ambazo baadaye washtakiwa walizigawana kama nyara.
“Halikadhalika, haipingiki kwamba, marehemu aliitwa au kuelekezwa (na washtakiwa) kufika kituo cha polisi Mtwara Januari 5 2022 ikiwa ni wito wa kufuata mali zake,”ilieleza jamhuri.
Mshtakiwa aliisaidia jamhuri
Na wala haipingiki kwa ushahidi wa shahidi wa tano wa utetezi kwamba, washtakiwa wenzake walimuua (Mussa) Januari 5, 2022 katika Kituo cha Polisi Mitengo.
Pia, haipingiki tangu alipokamatwa marehemu Sadina Lodge Mtwara Oktoba 20, 2021 hadi Januari 5, 2022 alipouawa katika Kituo cha Polisi Mitengo, kila mshtakiwa alikuwa na jukumu lake la kutekeleza.
Jaji alielezwa kuwa, kwa msingi huo, ushahidi mkubwa ulioletwa na utetezi unathibitisha kesi ya upande wa mashtaka.
Kama ilivyo kisheria kwamba, ushahidi wa kuthibitisha unaweza kuwa wa mazingira na mienendo ya mshtakiwa.
Hili limeleezwa kwenye kesi ya Kitigwa dhidi ya jamhuri [1994] TLR 65, iliyonukuliwa kwa kuidhinishwa katika kesi ya Mboje Mawe na wengine watatu dhidi ya jamhuri, rufaa ya jinai namba 86 ya mwaka 2020.
Vilevile, jamhuri ilijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na washtakiwa katika utetezi wao au katika hoja zao za mwisho zilizowasilishwa na mawakili wao.
Utetezi wa ‘alibi’
Kwenye kesi za jinai, katika hatua ya utetezi kuna aina ya utetezi ambao kwa lugha ya kisheria huitwa alibi (alibai, kwa matamshi).
Alibi ni neno la Kilatini linalomaanisha "mahali pengine" au katika sehemu nyingine".
Tafsiri hiyo imewahi kutolewa na Mahakama ya Rufani katika kesi ya Msafiri Benjamin dhidi ya jamhuri (rufaa ya jinai namba 549 ya 2020, iliyoamuliwa Agosti 27, 2021).
Kwa hiyo huu ni utetezi ambao mshtakiwa hudai kuwa hakuwepo eneo la tukio la uhalifu siku na wakati lilipotendeka, katika harakati za kujinasua kutoka katika tuhuma za uhalifu anazokuwa anakabiliana nazo.
Katika kesi hii, pia baadhi ya washtakiwa walitumia utetezi wa aina hiyo.
Hata hivyo, utetezi wa aina hiyo una kanuni na taratibu zake zinazopaswa kufuatwa ili upokewe mahakamani na kukubalika.
Fuatilia sehemu inayofuata kujua uchambuzi huo wa jamhuri kuhusu udhaifu wa aina hiyo ya utetezi wa washtakiwa, pamoja na hoja nyinginezo zilizoibuliwa na washtakiwa hao.