Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DPP akwaa kisiki kutaifisha lori la Kenya lililokamatwa na wahamiaji haramu

Moshi. Sasa ni dhahiri imekuwa mfupa mgumu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuitupa rufaa yake kupinga lori la Kenya lililokamatwa likiwa na wahamiaji haramu, lisirejeshwe kwa mmiliki.

Hii ni baada ya jitihada zake kuzuia gari hilo aina ya Mercedes Benz lisirejeshwe kwa mmiliki ambaye ni kampuni ya Almaha Transport and Investment Company Ltd ya Kenya kugonga mwamba.

Uamuzi wa kuitupa rufaa ya DPP namba ya 2024 ulitolewa Juni 30, 2025 na Jaji Lilian Mongella wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi na kuwekwa mtandaoni Julai 2, 2025, akisema sababu za rufaa alizozitoa DPP zilikuwa hazina mashiko.

Jaji alisema katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, kampuni hiyo ilikuwa imewasilisha maombi mawili, ikiomba irejeshewe gari hilo lililokamatwa Juni 19, 2024 eneo la Holili likiwa na wahamiaji haramu watano.


Wahamiaji walivyokamatwa

Kulingana na Jaji, alisema nyaraka za kumbukumbu za rufaa hiyo zinaonyesha siku ya tukio, Tom Muinde Nguli alikuwa akiendesha lori hilo la kusafirisha gesi, akitokea Kenya kuja nchini Tanzania.

Lori hilo lilipofika eneo la Holili wilayani Rombo ambako ni mpaka kati ya Tanzania na Kenya, lilisimamishwa kwa ajili ya ukaguzi na ndipo ilipogundulika chini ya uvungu wa lori kulikuwa na wahamiaji haramu watano kutoka nchini Somalia.

Gari hilo pamoja na wahamiaji hao haramu walipelekwa Moshi ambako raia hao wa Somalia walifikishwa mahakamani kupitia kesi ya Jinai ya 2024 kosa likiwa ni kuingia katika ardhi ya nchi ya Tanzania kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao waliposomewa mashitaka hayo walikiri kosa hilo ambapo walihukumiwa kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kifungo cha mwaka mmoja na ndipo Jamhuri ikaomba gari hilo litaifishwe, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama.

Hata hivyo, kampuni hiyo iliwasilisha maombi mahakamani ikiomba irejeshewe gari lake, maombi ambayo yalipingwa vikali na DPP lakini mahakama baada ya kusikiliza pande zote mbili, ilifuta amri ya kulitaifisha na kurejeshwa kwa wamiliki.


Rufaa ya DPP ilivyokuwa

DPP hakuridhishwa na uamuzi wa kuwarejeshea wamiliki gari hilo, hivyo akakata rufaa Mahakama Kuu akiegemea sababu moja tu kuwa Hakimu alikosea kisheria aliposhindwa kubaini ushahidi uliopo jaladani, hauoani na kiapo cha wamiliki.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa, mrufani ambaye ni DPP aliwakilishwa kortini na wakili wa Serikali, Frank Wambura, wakati wajibu rufaa ambao ni kampuni ya Almaha Transport and Investment Co Ltd ikiwakilishwa na wakili Sikifu Mtikile.

Akijenga hoja ya rufaa hiyo, wakili Wambura alisema taarifa zilizotolewa na mjibu rufaa hasa katika aya ya 4 ya kiapo chake, haioani na ushahidi alioutoa.

Wakili alieleza mjibu rufaa alikuwa ameeleza kuwa Juni 19,2024 saa 3:00 asubuhi, dereva wao aliliendesha lori kutoka Kenya kuja Tanzania kwa ajili ya kupeleka gesi.

Lakini kwa upande mwingine, wakili huyo wa Serikali alisema mjibu rufaa aliwasilisha cheti kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kikionyesha anaruhusiwa kusafirisha kemikali kutoka Tanzania kwenda Kenya.

Kwa mujibu wa wakili huyo, alisema hiyo pekee inaonyesha kuwa mjibu rufaa hana kibali cha kusafirisha kemikali kutoka Kenya kuja Tanzania.

Wakili huyo akasema ni msimamo wa sheria kuwa kiapo chenye taarifa za uongo hakiwezi kuaminiwa na mahakama hivyo akaikosoa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kwa kukubali ombi la kurejeshewa gari kwa kuegemea taarifa ya uongo.

Akijenga hoja zaidi, wakili Wambura aliongeza kusema wakati watuhumiwa wanakamatwa Holili, gari hilo lilikutwa tupu, na kwamba hiyo inadhihirisha mjibu rufaa alifahamu biashara haramu iliyokuwa ikifanywa na dereva wao.

Hivyo aliiomba mahakama ikubali rufaa hiyo na kufuta uamuzi wa awali wa kulirejesha kwa wamiliki, na uamuzi wa kulitaifisha kuwa mali ya Serikali ubakie.


Mmiliki wa gari alivyopambana

Akijibu hoja hizo, wakili Mtikile alianza kwa kurejea msimamo wa kisheria kupitia kesi ya Makubi Dogani dhidi ya Ngodongo Maganga iliyoweka msimamo pale ambapo upande mmoja unashindwa kupinga kupokelewa kwa kielelezo.

Akirejea uamuzi wa kesi hiyo ya rufaa aliyoirejea, wakili Mtikile alisema kielelezo kinachopokelewa na mahakama bila kuwepo kwa pingamizi lolote linathibitishwa ipasavyo kwa sababu ya kutokuwepo kwa pingamizi lolote juu ya kielelezo hicho.

Wakili alipinga hoja za DPP kutokana na kushindwa kuelezea ni kwa kiwango gani aya ya 4 ya kiapo cha mjibu maombi kilivyopingwa na kwamba hiyo inadhihirisha alikubaliana na maelezo yaliyomo, na hicho anachodai ni fikirio tu la baadaye.

Alienda mbali na kueleza kiapo kinaweza kupingwa kwa njia tatu, moja ni kupitia pingamizi la awali, mbili ni kupitia kiapo kinzani na kuweka taarifa zako kinzani na tatu ni wakati maombi yanaposikilizwa kortini.

Ni kwa msingi huo, wakili huyo alisema mleta rufaa (DPP) anazuiwa kutoa ufafanuzi wowote wa maudhui yanayobishaniwa katika hatua ya rufaa.

Alipinga kauli kuwa kibali kilikuwa ni kwa ajili ya kusafirisha bidhaa za kemikali kutoka Tanzania Kwenda Kenya, akisema jambo hilo ni jipya na halikuzungumzwa wakati wa usikilizwaji wa maombi hivyo haliwezi kuletwa katika hatua ya rufaa.

Wakili alisema hoja ambayo mrufani alipaswa kuithibitishia mahakama kuhusiana na gari hilo lililokuwa limeamriwa litaifishwe, ni kama yeye ndio mmiliki halali na hakuwa anafahamu kutendeka kwa kosa hilo la jinai, jambo alilolifanya.


Hukumu ya Jaji

Jaji Mongella alisema amepitia hoja za rufaa na mawasilisho ya mawakili wa pande zote mbili na kwamba ubishi uliopo unahusu uhalali au vinginevyo, wa amri ya kurejesha gari kwa mmiliki iliyotolewa na mahakama iliyosikiliza maombi.

“Wakili Wambura alipinga amri ya marejesho ya gari kwa mmiliki kwa sababu moja tu, kwamba mahakama ya mwanzo ilishindwa kuzingatia ukweli unaokinzana chini ya aya ya 4 ya hati ya kiapo ya mleta maombi,”alisema Jaji.

“Kwa maoni yake, gari hilo lilitumika katika kutenda uhalifu hivyo linastahili kutaifishwa (kuwa mali ya Serikali ya Tanzania). Alishikilia kuwa msimamo huo haukupaswa kubadilishwa na mahakama iliyosikiliza ombi hilo,” alieleza Jaji.

Jaji alirejea misimamo na maamuzi ya mahakama ya juu iliyosema kuwa amri ya kutaifisha haizuii upande mwingine kudai haki ya umiliki wa mali hiyo ilimradi tu anatakiwa afanye hivyo ndani ya miezi sita tangu amri ya kutaifishwa kutolewa.

“Hata kama mali hiyo itakuwa imeuzwa au kuhifadhiwa, upande unaodai ni yake una haki ya kuwasilisha maombi mahakamani kuiomba ichunguze nani ni mmiliki halali, na kurudisha uchunguzi wake ili ufanyiwe maamuzi,”alisema Jaji.


Uhalali wa kurejeshewa gari

“Katika hatua hii, sasa nitakwenda kushughulikia swali nililoliacha kiporo ambalo ni kama maombi (ya kurejeshewa gari) yalitolewa uamuzi kwa usahihi.”

Jaji alisema wakili Wambura aliibua mashaka kuwa maombi hayo yalikubaliwa kwa kuegemea taarifa zinazojikanganya kupitia aya ya 4 ya kiapo cha muombaji na kwamba jaji akasema anaona ni busara kuinukuu aya hiyo kama ilivyo.

“Kwamba Juni 19,2024 saa 3:00 asubuhi, dereva aliyetajwa hapo juu aliendesha gari aina ya Mercedes Benz ikiwa na trailer kutoka Kenya kuja Tanzania kupeleka gesi kwa Manjis Gas Supply Company Limited ya Dar es Salaam,”inaeleza aya hiyo na kuongeza kuwa.

“Nakala ya kibali kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na fomu ya muda ya kuingiza mafuta imeambatanishwa kwa pamoja kama kiambatanisho AL-3 vikifanya kuwa sehemu ya kiapo hiki,”mwisho wa kunukuu.

Jaji akasema aya hiyo haionyeshi siku ya tukio dereva alikuwa akisafirisha bidhaa kutoka Kenya kuja Tanzania wala na hata kibali kinaonyesha kilitolewa kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam kwenda kwa mteja yeyote wa Manjis hapa nchini.

Mbali na kibali hicho, Jaji alisema kuna kibali cha muda cha kuingiza nchini au kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwa njia ya barabara kwa nchi za Afrika Mashariki.

Nyaraka hiyo inaonyesha dereva aitwaye Nguli kama ndiye wakala aliyeidhinishwa na kampuni hiyo ya Kenya ambayo anatajwa kuwa anaishi Kenya na kibali hicho cha muda kinaonyesha kilitolewa Juni 18, 2024, ikiwa ni siku moja kabla ya tukio.

Jaji alisema pamoja na nyaraka hiyo, zipo nyaraka nyingine zilizoonyesha kituo cha kwanza cha kuingia nchini ilikuwa kituo cha forodha cha Tarakea na kuna nyaraka za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zikimtaka alipe ushuru stahiki.

“Kwa kutazama ni kweli taarifa zilizopo katika aya ya 4 zinatofautiana nyaraka zilizoambatanishwa. Hata hivyo, sioni kama hili kwa njia yoyote ile linaonyesha mjibu rufaa alishindwa kuthibitisha madai yake katika maombi,”alisema Jaji.

Kwa mujibu wa Jaji, mjibu rufaa alijaribu kuonyesha yeye ndio mmiliki wa gari na siku ya tukio gari hilo lilikuwa linaendeshwa na dereva ambaye ni mwajiriwa wao, likitokea Kenya kuja Tanzania wakati iliposimamishwa na kukutwa wahamiaji.

“Katika utetezi wake anasema alizingatia sheria zote za Tanzania na hakuwa anafahamu kuhusu matendo ya dereva wao.”

“Nyaraka zote zilizoambatanishwa na maelezo aliyoyatoa kiukweli yanathibitisha kuwa mjibu rufaa hii ndiye mmiliki halali wa gari na gari hili lilihusika katika biashara halali ya usafirishaji wa bidhaa,” alisisitiza Jaji Mongella.

Katika hoja nyingine, Jaji akasema wakili Wambura aliibua madai kuwa kulikuwa na chemba ndani ya gari hilo ambayo iliwezesha kuwahifadhi wahamiaji hao.

“Naona hii ni suala jipya kwa sababu haikuwahi kuibuliwa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo. Nakubaliana na wakili Mtikile kuwa mleta rufaa (DPP) alipaswa kuibua hayo kwenye kiapo kinzani au wakati wa usikilizwaji wa maombi,” alisema.

Jaji alisema anachokiona ni kwamba DPP alishindwa kuthibitisha madai yake kwamba gari lilihusika katika uhalifu na alishindwa kuthibitisha kuwa madai ya mjibu rufaa kuwa hakuwa anafahamu mchezo wa dereva, ilikuwa ni uongo.

Katika hitimisho lake, Jaji akasema mrufani ambaye ni DPP alibishaniwa tu taarifa zilizosemwa na mrufani wa lakini hakwenda mbali kuthibitisha na ndio maana mahakama ilijiridhisha vizuri kuwa mrufani ndiye mmiliki halali wa gari na wala hakuwa anaufahamu wowote wa vitendo vya kihalifu vya dereva wake.

Ni kwa msingi huo, Jaji alisema rufaa ya DPP haina mashiko na inatupiliwa mbali.