Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Warundi 25 watupwa jela mwaka mmoja kwa kuishi nchini bila vibali

Muktasari:

  • Warundi hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 29, 2025 katika maeneo ya Karume na Jangwani yaliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu raia 25 wa Burundi  kulipa faini ya Sh250,000 kila mmoja au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kupatikana na hatia kuwepo nchini Tanzania kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao ni Manirambona Atanasi, Igirinya Yolevis, Ndiyokubaya Jamali, Manario Ezekiel, Ndereimana Levis na wenzao 20.

Uamuzi huo umetolewa leo Julai 4, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, baada ya washtakiwa hao kukiri shitaka lao.

Hata hivyo washtakiwa hao wameshindwa kulipa faini hiyo na hivyo wataanza kutumikia kifungo hicho.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Lyamuya amesema washtakiwa wametiwa hatiani kama walivyoshtakiwa hivyo kila mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh250,000 na kama akishindwa kulipa faini hiyo, atatumikia kifungo cha mwaka moja gerezani.

Awali, wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Raphael Mpuya akisaidiana na Mohamed Mlumba waliomba Mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao kwa kuwa vitendo walivyofanya ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, washtakiwa walipopewa nafasi na mahakama hiyo ya kujitetea, waliiomba iwapunguzie adhabu kwa kuwa wao ni wakosaji wa mara ya kwanza na hawatarudia kutenda kosa hilo

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai ya mwaka 2025 yenye shitaka moja la kuwepo nchini Tanzania kinyume cha sheria.

Walitenda makosa hayo Mei 29, 2025 katika maeneo ya Karume na Jangwani, Jiji la Dar es Salaam.

Washtakiwa hao siku hiyo ya tukio,  walikamatwa na maofisa wa uhamiaji kwa kosa la kuwepo nchini bila kuwa kibali, wakati wakijua kuwa ni kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.