Atupwa jela miezi sita kwa shambulio la chupa

Muktasari:

  • Kutokana na mshtakiwa kukiri kosa lake, mahakama hiyo imemkuta na hatia.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Tanzania, imemuhukumu kwenda jela miezi sita Mkazi wa Chang'ombe, Oscar Sanga baada ya kukiri kosa la kumshambulia  kwa chupa na  kumjeruhi kichwani Justa Paskal.

Hukumu hiyo imesomwa leo Jumatano Januari 27, 2021 na Hakimu Mkazi, Amos Rweikiza baada ya mshtakiwa huyo kukiri kosa lake.

Hakimu Rweikiza amesema Desemba 19, 2020 maeneo ya Temeke Sokota, mshtakiwa huyo alimshambulia kwa chupa na kumjeruhi Justa kinyume na kifungu cha 231 cha makosa Sheria namba 16 rejeo ya mwaka 2019.

Amesema kutokana na mshtakiwa kukiri kosa lake, mahakama hiyo imemkuta na hatia.

“Mahakama hii imekukuta na hatia, hivyo inakupa adhabu ya kwenda  jela miezi sita ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo,” amesema Rweikiza.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Doroth Masawe alidai kuwa mshtakiwa huyo licha ya kutokuwa na historia ya mashtaka, lakini ni vema mahakama ikatoa adhabu ili iwe fundisho.