Auawa kwa tuhuma za kumpa ujauzito mke wa mtu

Saturday November 13 2021
auapic

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Marrison Mwakyoma

By Joseph Lyimo

Simanjiro. Daktari wa mifugo wa kijiji cha Loiborsoit A wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, Malipe Ole Kisota ameuawa kwa kukatwa mapanga na watu waliomtuhumu kumpa ujauzito mke wa ndugu yao.

Imeelezwa kuwa alikatwa na sime sehemu mbalimbali mwilini na ndugu watatu, Lazaro,  Mamei na Supek Mamei, wakimtuhumu kumpa ujauzito mke wa ndugu yao Kinaruu Mamei.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Marrison Mwakyoma akizungumza Novemba 13,2021 ameieleza Mwananchi Digital kwa njia ya simu kuwa mauaji hayo yametokea Novemba 11,2021.

Kamanda Mwakyoma amesema chanzo cha kifo hicho ni wivu wa mapenzi, akidai marehemu alikuwa akituhumiwa kutembea na mke wa mtu na alikuwa anatafutwa akawa anajificha na siku ya tukio walimkibiza, kumkamata na kufanya mauaji hayo.

"Mwanamke alipohojiwa alikubali kuwa na mimba ya mtu mwingine ndipo mume wake akachukua uamuzi wa kikatili wa kumuua  akishirikiana na ndugu zake," amesema kamanda Mwakyoma.

Kamanda Mwakyoma amesema watuhumiwa hao watatu walitoroka kusikojulikana mara baada ya mauaji hayo ila wanaendelea kuwatafuta ili wawafikishe mahakamani.

Advertisement

"Natoa wito mtu anapobaini mwanamke ameolewa kisha amepewa mimba na mwanaume mwingine ni bora waachane au kusuluhisha kuliko kufanya mauaji," amesema kamanda Mwakyoma.

Mmoja kati ya mashuhuda wa tukio hilo, Alais Sasinee amesema Ole Kisota (mume wa mwanamke anayedaiwa kupewa ujauzito) aliuawa na ndugu hao kwa kucharangwa sime baada ya kutoka kuangalia mpira wa miguu baina ya timu ya Taifa ya Tanzania  na DRC-Congo.

Advertisement