Baba adaiwa kufukua mwili wa mwanaye ukafanyiwe maombi afufuke

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa  Katavi limesema mtuhumiwa alipofanyiwa uchunguzi alibainika kuwa na tatizo la afya ya akili

Katavi.  Mkazi wa Mtaa wa Kapalangao Manispaa ya Mpanda, Fransis Nilanga amedaiwa kufukua kaburi la mwanaye kisha kubeba jeneza lenye mwili huo kwenda nalo nyumbani kufanya maombi ili afufuke.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumanne Januari 30, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amesema tukio hilo limetokea Januari 28 saa saba usiku.

"Mtoto wake alifariki na kuzikwa Julai mwaka jana katika makaburi ya Kazima akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu. Sisi tulipata taarifa kutoka kwa dereva wa bajaji aliyejitambulisha kwa jina la Alex, akisema wakati anapita eneo hilo alimuona amebeba jeneza alimuomba amsaidie kubeba kwenda nyumbani," amesema Kamanda Ngonyani.

Pia,  amesema baada ya kupata taarifa walimkamata na alipofikishwa Kituo cha Polisi Mpanda kufanyiwa uchunguzi, walibaini mtuhumiwa huyo ana ugonjwa wa afya ya akili.

"Tuliwasiliana na uongozi wa eneo hilo, baba wa mtuhumiwa alipatikana alikiri mwanaye ana tatizo hilo, tukamuachia huru akaondoka na baba yake," amesema Kamanda Ngonyani.

"Nilipata taarifa usiku, kutoka polisi nilimfahamu huyo kijana kwasababu ni jirani nilimtaarifu baba yake kisha tukaenda polisi."

"Baada ya kufika tulishuhudia ni yeye na mwili wa mtoto, tulitoa maelezo polisi waliamuru tukauzike mwili kwenye kaburi la awali," amesema Feruzi.

Anna John mkazi wa Mpanda amesema wazazi na walezo wanatakiwa kuwa makini na watoto wao wanaokabiliwa na magonjwa ya afya ya akili.

"Wanatakiwa kuwalinda usiku na mchama hili tukio ni la kusikitisha sana licha ya kuwa mtuhumiwa alikuwa mgonjwa," amesema Anna.