Baba ahukumiwa miaka 40 jela kwa kuzaa na binti yake

Muktasari:

  • Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, Yudith Lyimo amemhukumu kifungo cha miaka 40 jela, na viboko 12 mkazi wa ‘Kwa Mfipa’ Kibaha, Fadhiri Msham kwa kosa la kufanya mapenzi na mwanawe wa kumzaa na kumpa ujauzito.

Kibaha. Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, Yudith Lyimo amemhukumu kifungo cha miaka 40 jela, na viboko 12 mkazi wa ‘Kwa Mfipa’ Kibaha, Fadhiri Msham kwa kosa la kufanya mapenzi na mwanawe wa kumzaa na kumpa ujauzito.

Mbali na adhabu hiyo pia Msham ambaye ni mtumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kama dereva, atatakiwa kulipa kiasi cha Sh4 milioni kama fidia kwa mwanawe huyo mwenye umri wa miaka 27, kutokana na kitendo alichomfanyia kilichosababisha kushika ujauzito na kupata mtoto.

Hukumu hiyo imetolewa jana Jumatatu Mei 8, 2023 mahakamani hapo baada ya hakimu kuridhishwa na ushahidi uliotolewa wakati wa mwenendo wa kesi hiyo.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa Msham alitenda kosa hilo 2021 huko Kwa Mfipa wakati alipotembelewa na mwanawe huyo aliyekuwa anaishi maeneo mengine na mama yake mzazi.

Kwa mujibu wa mwenendo wa kesi hiyo ya jinai namba 23 ya mwaka 2021, imeelezwa kuwa baada ya kuletwa Mahakamani  kwaajili ya kusikilizwa kipindi hicho; ilibidi iliondolewa ili kusubiri hadi mtoto atakapo zaliwa kwa lengo la kupata uthibitisho wa kipimo cha vinasaba (DNA).

Baada ya kuzaliwa mtoto ndipo shauri hilo lilirudishwa mahakamani kwa mara ya pili ambapo taratibu za kipimo hicho zilifanyika na kubaini kwa asilimia 99.99 kuwa Msham anahusika kumpa ujauzito mwanawe huyo.