Aiba Sh19 milioni, ahukumiwa kulipa faini 150,000

Muktasari:

  • Mkazi wa Mabibo Mwinyi Rajabu amehukumiwa kifungo cha miezi jela sita au kulipa faini ya Sh150,000 na Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kwa kukosa la kuiba kiasi cha Sh19 milioni katika benki ya CRDB  tawi la Lumumba ambapo fedha hizo ni za kaka yake Haji Mwinyi.

Dar wa Salaam. Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo imemhukumu mshtakiwa Mwinyi Rahabu kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya Sh150,000 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuiba kiasi cha Sh19 milioni  ambazo fedha hizo ni za kaka yake Haji Mwinyi.

 Hukumu hiyo imesomwa Aprili 28, 2023 na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Clauds Kipande alisema mahakama hiyo imemkuta na hatia kwa kuwa mshtakiwa huyo alienda benki ya CRDB tawi la Lumumba na kisha alitoa kiasi cha Sh19 milioni kwenye akaunti ya  Mwinyi kwa nia ya kuiba.

Kipande alisema kutokana na hilo mahakama hiyo imemtia hatiani na imemuhukumu mshtakiwa huyo kifungo cha miezi sita gerezani au kulipa faini ya Sh150,000 na anaweza kukata rufaa kama hajaridhika na hukumu.

Hata hivyo mshtakiwa huyo ameshindwa kulipa faini hiyo hivyo ameenda gerezani kutumikia kifungo hicho.

Inadaiwa kuwa Desemba 19, 2022 saa 1 usiku mshtakiwa huyo alienda katika benki ya CRDB tawi la Lumumba na kisha alitoa kiasi cha Sh19 milioni kwenye akaunti ya Mwinyi kwa nia ya kuiba.