Baba anayedaiwa kuzaa na bintiye afikishwa mahakamani, arudishwa tena polisi

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoa wa Kipolisi Rufiji mkoani Pwani leo limemfikisha mahakamani baba anayedaiwa kuzaa na mtoto wake lakini baadaye amerejeshwa tena Polisi akisubiri kurejeshwa tena mahakamani kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka yake.

Rufiji.  Baada ya kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoa wa Rufiji mkoani Pwani, baba anayedaiwa kuzaa na binti yake watoto watatu amefikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka.

Mtuhumiwa huyo, Mabula Jiumbi, mkazi wa Kitongoji cha Mbambe, kijiji cha Mbunju-Mvuleni, kata ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, amefikishwa mahakamani, katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji, leo Jumanne, Oktoba 24, 2023.

Mabula amefikishwa mahakamani hapo saa 4:09 asubuhi akiwa ndani ya gari ya Polisi aina ya Toyota Landcruiser Pickup, rangi ya Samawati akiwa pamoja na watuhumiwa wengine.

Baada ya kufikishwa mahakamani hapa yeye pamoja na watuhumiwa wenzake wengine wameshushwa na kuingizwa katika mahabusu ya mahakama hiyo wakiwa wamefungwa pingu wawili wawili, ili kusubiri taratibu za kusajiliwa kwa kesi zao kisha wapandishwe kizimbani kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Hata hivyo baada ya dakika 51, yaani saa 5:00 asubuhi mtuhumiwa huyo na wenzake hao wamechukuliwa kutoka mahabusu na kupakizwa ndani ya gari hilo la Polisi lililowafikisha mahakamani hapo na kisha kuondoka nao.

Mmoja wa askari Polisi mahakamani hapo ameieleza Mwananchi Digital kuwa watuhumiwa hao wamerejeshwa Polisi Utete kwa ajili ya kukamilisha taratibu fulani na kwamba watarudishwa mahakamani hapo saa nane mchana kwa ajili ya kusomewa mashtaka.

Hata hivyo baadaye, saa 5:52, imetolewa taarifa ya kwa kesi zote mpya ambazo zilikuwa bado hazijasajiliwa mahakamani hapo wakiwemo watuhumiwa waliotoka Ikwiriri ambao walikuwa wamepelekwa Polisi (akiwemo mtuhumiwa Mabula) zimeahirishwa.

Tarifa hiyo iliyotolewa na mmoja wa watu waliokuwemo mahakamani wakifuatilia kesi  ya ndugu yake  amesema kuwa kwa  mujibu wa taarifa aliyopewa na askari Polisi, watuhumiwa hao waliokuwa wamepelekwa Polisi hawataletwa tena leo na kwamba badala yake SAS awataletwa kesho.

Hivyo akinukuu taarifa hiyo aliyoipata Kwa Polisi amesema kuwa ndugu wa watuhumiwa hao wanapaswa kuondoka na kurejea kesho, isipokuwa wale ambao tayari kesi zao zimeshasajiliwa mahakamani hapo.

Askari Polisi mmoja kutoka kituo hicho cha Polisi walikopelekwa amelieza Mwananchi kuwa kweli watuhumiwa wengine waliopelekwa kituoni hapo hawataletwa tena leo mahakamani mpaka kesho isipokuwa Mabula tu ndio ataletwa kusomewa mashtaka yake.

Hivyo mpaka sasa mtuhumiwa huyo yuko kituo cha Polisi akisubiri taratibu kukamilika kabla ya kuletwa tena mahakamani kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Atasomewa mashtaka gani na baada ya kusomewa atajibu nini? Je, atakubali au atakana? Hayo yote yatakulikana baadaye atakapoletwa tena na kupandishwa kizimbani.