Polisi wamdaka baba anayedaiwa kuzaa na bintiye

Pwani. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni. Ni usemi unaoakisi tukio la baba kudaiwa kumgeuza mwanawe wa kumzaa kuwa mke wake na kuzaa naye watoto watatu.

Tukio hilo la nadra kutokea katika jamii, linadaiwa kutokea katika Kitongoji cha Mbambe, kijijini Mbunju-Mvuleni, Kata ya Mkongo wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Protas Mutayoba, akizungumza na Mwananchi juzi, alisema baba huyo anayetuhumiwa anashikiliwa na polisi.

"Nilituma watu wangu kufanya upelelezi, tumemkamata baba, mtoto na mama tumefanya nao mahojiano ya awali, hivyo Alhamisi (kesho) tunampeleka mtuhumiwa mahakamani," alisema Kamanda Mutayoba.


Ilivyokuwa awali

Baada ya tuhuma hizo kulifikia gazeti hili, lilimtafuta baba huyo azungumzie suala hilo, alisema hapendi kuingiliwa maisha yake na familia yake, huku akiwatupia lawama majirani zake.

"Kwa hiyo wamekupa taarifa za familia yangu ili unifanye nini? Hao ambao wamekwambia hawanijui, na nani kakupa namba zangu? Umekosa kazi ya kufanya na kuniuliza ujinga," alisema kwa ukali na kukata simu.

Kwa mujibu wa habari zilizolifikia gazeti hili, baba huyo ana watoto sita, kati ya hao wa kiume ni wanne na wa kike ni wawili.

Taarifa zaidi zinadai kuwa watoto wote hawajapelekwa shule na badala yake husaidia shughuli za nyumbani.

Mmoja wa watoto wake wa kiume alipozungumza na Mwananchi alisema hakuna aliyekwenda shule kwa kuwa baba yao hataki wasome licha ya kuwa wao wanahitaji elimu.

"Baba hataki kusikia chochote kuhusu elimu, anadai nani atashughulika na masuala ya uchungaji na mambo ya nyumbani, hivyo hajaona umuhimu wa shule na anahisi ni kupoteza muda," alisema.

Anadai ana ndoto za kuwa msanii wa nyimbo za Bongo Fleva na anapenda kuishi mjini, lakini baba yao ni mkali kwenye kila jambo.

"Dada yangu mkubwa ameolewa lakini anaishi nyumbani. Mume wake anaishi mbali na hakuna anayefahamu huko anakoishi," anasema na kuongeza:

"Dada yangu hakutolewa mahari na hachumbiwi tena kwa sababu ameshaolewa. Hata ikitokea mtu anataka kumchumbia hatakubali. Baba naye atakataa kwa sababu ni mke wa mtu.”

Anasema, "Walishakuja watu kutaka kumchumbia alikataa na baba pia, sisi tulitamani aolewe na kuondoka japokuwa amezaa kwa kuwa tungebaki na watoto wake."

Anasema baba yao amempa chumba dada yake na kwamba, "Tunashangaa kumuona dada akiwa na mimba lakini hatumuoni shemeji sababu yupo mbali. Tunashindwa kuuliza kwa sababu hatutakiwi kuongea na dada zetu kitu chochote na tunaacha mambo mengine yaendelee.”


Majirani wafunguka

Baadhi ya majirani wanadai huenda baba huyo ana uhusiano na binti yake ndiyo maana anakataa kumuozesha licha ya wachumba kujitokeza.

Mmoja wao, (jina linahifadhiwa) alisema vijana watatu walijitokeza kwenda kuchumbia lakini wote walikataliwa kwa maelezo kuwa tayari ni mke wa mtu.

"Baada ya kijana wa kwanza kukataliwa walikaa kujadili na kumwambia mwingine aende, alipokwenda alitajiwa mahari kubwa, alikubali lakini cha kushangaza baba mtu alikataa na akamwambia asirudi kwani haozeshi,” alidai.

Anadai watoto wake wa kike hawatakiwi kuchanganyika na wanaume na ikitokea umekwenda nyumbani kwake, hawatakiwi kusogea kwa jambo lolote.

"Huyo binti yake wa pili alitaka kumuozesha kwa kaka yake ambaye wamezaliwa tumbo moja, kwa kuwa kijana wake anajitambua alikataa kumuoa mdogo wake, hivyo alitafutiwa kijana mwingine na kumuoa," alidai jirani mwingine.

Alidai baba huyo amekuwa akiwazuia watoto wake kujihusisha na jamii inayowazunguka kwa maelezo kuwa watapewa maneno yatakayoharibu mahusiano ya kifamilia.

Jirani mwingine anasema ndugu wa baba huyo walipojaribu kuingilia kati waliishia kugombana na aliwafukuza nyumbani kwake kwa kudai wana vitendo vya hovyo.


Kauli ya awali ya RPC

Awali, Kamanda Mutayoba alipotafutwa na Mwananchi alisema matukio hayo hayajaripotiwa kituo cha polisi na kama yatatolewa taarifa, watafanya uchunguzi na kubaini ukweli wake.

Kamishna wa Ustawi wa Jamii, katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Nandera Mhando, alisema tuhuma hizo hugusa pande zote na ikithibitishwa kosa mtuhumiwa hufikishwa mahakamani.

Alisema mtoto atahitaji msaada wa kisaikolojia iwapo tukio hilo litathibitishwa na ni lazima ataondolewa kwa kuwa hawawezi kuachwa waendelee kuishi pamoja kama mke na mume.

Alisema kipimo cha vinasaba (DNA) ndicho suluhisho kwenye kesi za namna hiyo.


Mwingine aozeshwa

Binti mwingine wa familia hiyo mwenye umri wa miaka 16 ameozeshwa na mahari ilipokewa na baba yake.

Akizungumzia hilo, Mhando alisema endapo hayuko shuleni sheria inaruhusu mzazi kumuozesha.

Hata hivyo, alisema wanapigania mabadiliko ya sheria inayoruhusu ndoa ya mtoto wa miaka 15 kwa ruhusa ya mzazi.

Ofisa huyo alisema mapitio ya sheria yanafanyika na tayari Wizara ya Sheria na Katiba imekaribisha maoni kwa ajili ya kubadili sheria hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele alisema, "Tabia hii tunaipinga na haikubaliki kwa sababu huo umri ni wa mtoto kuwa shule. Pia kitendo cha kuzaa na mtoto wa kumzaa haikubaliki na ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.”

Mbali ya tukio hilo, alisema hivi karibuni huko Utete kuna mzee alianzisha mahusiano na binti yake wa darasa la sita, taarifa zilipowafikia walimchukulia hatua za kisheria.

"Tulimchukua binti na kumpeleka hospitali kupimwa, alikutwa mjamzito tukamfikisha baba mahakamani na alikiri kufanya kitendo hicho, hivyo sheria ikafuata mkondo wake," alisema.


Viongozi wa kijiji, dini

Balozi wa eneo hilo, Mohamed Mtupa anadai baba huyo hajawahi kuchangia chochote kuhusu shule kwa madai kuwa haoni umuhimu wa watoto kusoma.

Kuhusu tuhuma za kuzaa na binti yake, anadai kila jambo linaposemwa lina sababu na haiwezekani kijiji kizima wakamjadili mtu mmoja.

Mtupa anadai kinachoibua zaidi hisia ni mtoto aliyeolewa kuendelea kukaa nyumbani kwao na akiendelea kupata ujauzito.

"Hakuna mwanamume anaweza kukubali atoe mahari yake, tena ng'ombe kwa wenzetu wafugaji halafu mkewe aendelee kukaa kwao na yeye akae mbali, ni ngumu, ndipo watu walipotilia shaka uhusiano wa baba na mtoto," anasema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mbunju-Mvuleni, Fadhili Hwai anasema kwa familia za kifugaji kutopeleka watoto shule na kuozeshana wenyewe amelisikia ila hajawahi kushuhudia.

Hwai anasema wakati mwingine wanashindwa kuchukua sheria kutokana na mila, hivyo wanabaki kushangaa kwa kuwa tamaduni za Tanzania hazikubaliani kwenye hilo na hata wanapokwenda mahakamani, mtoto hatoi ushirikiano.

Askofu William Mwamalanga ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maaskofu na masheikh ya maadili, amani na haki za binadamu, anasema mtoto kuzaa na baba yake ni laana.

Akinukuu maneno ya Biblia alisema, “Amelaaniwa mtu anayefanya ngono na dada yake, binti ya baba yake au binti ya mama yake. Amelaaniwa mtu anayefanya ngono na mama mkwe wake."

Kwa upande wake, Sheikh Hamidu Sadalla, anayeishi Kinyerezi anasema kitendo hicho ni laana ya familia na hakikubaliki kidini na kisheria.