Baba atuhumiwa kumbaka mwanawe wa kumzaa

Baba atuhumiwa kumbaka mwanawe wa kumzaa

What you need to know:

  • Mtuhumiwa Ikwabe Gibogo alikamatwa Januari 23 usiku baada ya polisi kupata taarifa toka kwa wasamaria wema kwa madai kwamba amekuwa na tabia ya kumwingilia kimwili mtoto wake wa miaka 11.

Serengeti. Polisi wilaya ya Serengeti inamshikilia mkazi wa kitongoji cha Chamoto, Ikwabe Gibogo (58) kwa tuhuma za kumwingilia kimwili mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka (11).

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 23 usiku baada ya polisi kupata taarifa toka kwa wasamaria wema na kumkuta amelala chini pamoja na mtoto huyo wote wakiwa hawajavaa nguo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Daniel Shillah leo Januari 25 amezungumza na Mwananchi kwa njia ya simu na kuthibitisha kuwa mtuhumiwa amekamatwa na wanaendelea na uchunguzi kubaini undani wake.

“Tukio lipo na mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa nami nafuatilia mara kwa mara, taarifa ikikamilika nitatoa kwa undani zaidi,” amesema.

Mmoja wa majirani amesema mtoto huyo ameingiliwa kwa muda mrefu na baada ya kujiridhisha waliamua kutoa taarifa kwa kiongozi wa kitongoji na polisi walipofika waliwapa ushirikiano.

“Huyo mtoto hajaanza shule mpaka sasa, mama yao aliachana na baba yao baada ya kubaini anamuingilia mtoto wake mkubwa. Aliondoka na watoto wadogo kwenda Simiyu, hata hivyo, alifariki ndipo mtuhumiwa akafuata watoto na kuja kuishi nao,” amesema jirani huyo kwa sharti la kutotajwa jina.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Chacha Nyambuche amekiri mtuhumiwa kukamatwa nyumbani kwake akiwa amelala na mwanae huyo.