Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baba wa Joshua Mollel awasili Israel, amuaga mwanaye

Baba mzazi wa Mtanzania aliyeuawa huko Israel, Joshua Mollel

Dar es Salaam. Baba mzazi wa Mtanzania aliyeuawa huko Israel, Joshua Mollel yuko nchini humo kwa mwaliko wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ambapo akiwa huko alishiriki hafla ya kutoa heshima kwa Watanzania wawili waliouawa kwenye mapigano kati ya Israel na Hamas huko Gaza.

Desemba 14, 2023, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, January Makamba alieleza kwamba walipokea taarifa kutoka Serikali ya Israel ikiwajulisha kwamba Joshua aliuawa na Hamas tangu Oktoba 7, 2023.

Makamba aliandika taarifa hiyo katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter) akieleza kuwa Serikali imejulishwa na Serikali ya Israel kuwa Mollel aliyekuwa anasoma nchini humo aliuawa mara tu baada ya kutekwa na kundi la Hamas.

Joshua (21) alibainika kuwa Mtanzania wa pili kuuawa baada ya taarifa za awali kueleza kwamba Clemence Mtenga (22) kuuawa nchini humo na mwili wake kurejeshwa nchini Novemnba 27, 2023 na maziko kufanyika Novemba 28, 2023 wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Desemba 27, 2023, Naibu Balozi wa Israel katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda, Dvora Dorsman Yarkoni amesema Loitu Mollel ambaye ni baba mzazi wa Joshua Mollel yuko Israel alikokwenda kwa mwaliko wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi hiyo.

Amesema katika ziara yake, Mollel ameshiriki hafla ya kutoa heshima kwa Watanzania wawili waliouawa na kikundi cha Hamas huko Gaza (Clemence Mtenga na Joshua Mollel), hafla iliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Eli Cohen.

 “Mwili wa Joshua unashikiliwa na Hamas huko Gaza sambamba na mateka 129 wa Israel waliobaki mikononi mwa Hamas. Kati ya hao 21 wanajulikana kwamba wamekufa na miili yao bado inashikiliwa.

“Moja ya malengo yetu ya vita ni kuwaokoa mateka wote ukiwemo mwili wa Joshua. Hamas wamekataa kutoa taarifa kuhusu mahali ulipo mwili wa Joshua au kuuachia, kama walivyokataa pia kutoa taarifa kuhusu Waisraeli waliowateka,” amesema Balozi huyo.

Tangu vita ya Hamas na Israel ianze mamia ya raia wa nchi mbalimbali walitekwa nyara na kupelekea baadhi ya nchi kuwarudisha raia wao kwa sababu za usalama ikiwemo Tanzania.

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Israel ilianza juhudi za kuwatafuta raia wake ambapo miongoni mwao wanafunzi walikuwa 260.

Mbali na Watanzania hao, takribani watu 21,000 wameuawa huko Gaza ndani ya siku 81 ya mapigano hayo.