Babu wa Loliondo kuzikwa Samunge Jumatano

Babu wa Loliondo kuzikwa Samunge Jumatano

Muktasari:

  • DC wa Ngorongoro Raymond Mwangwala amesema baada ya kikao cha watoto wa mchungaji huyo na ndugu na majirani wamekubaliana kazishi kuwa Samunge.

Arusha. Mchungaji Ambilikile Mwasapile (86) aliyefariki Julai 30 anatarajiwa kuzikwa Jumatano Agosti 5 katika Kijiji cha Samunge, wilaya ya Ngorongoro mkoa wa Arusha sehemu ambayo alikuwa akitoa tiba ya mitidawa maarufu kama kikombe cha Babu.

Mwasapile aliugua nimonia kali ambayo ilimsababisha  kupata changamoto ya upumuaji na alifariki akiwa anakimbizwa kituo cha Afya cha Digodigo wilayani humo baada ya kuzidiwa.


Akizugumza na Mwananchi leo Agosti 2, 2021 Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mwangwala amesema baada ya kikao cha watoto wa mchungaji huyo na ndugu na majirani wamekubaliana kazishi kuwa Samunge.


"Tumekaa kikao na kufikia makubaliano mazishi kufanyika Samunge," amesema DC Mwangwala.
Amesema viongozi kadhaa kadhaa wa Serikali watashiriki na orodha itatolewa.


Amesema taarifa za awali za daktari wa kituo cha afya cha Digodigo kuwa Mchungaji Mwasapile alikuwa na dalili za nimonia.


Hata hivyo amesema katika msiba kutakuwa na tahadhari zote dhidi ya ugonjwa wa Corona.


"Nimeagiza msibani watu kuvaa barakoa, kuwa na maji tiririka na kufuata miongozo yote ya wataalam wa Afya na serikali," amesema.


Mmoja wa wasaidizi wa Babu wa Loliondo, Julius Peter anasema hadi anafariki Babu wa Loliondo alikuwa anasema watu watakuja Samunge maelfu kupata Tiba na alipata eneo kubwa ambalo alikuwa analiendeleza.


Mchungaji Mwasapile pia alikuwa akipokea wagonjwa wakiwepo wa Corona ili kuwapa kikombe hadi kifo kinamkuta.


Mchungaji ameacha watoto watatu, kwani mkewe wake alishafariki mwaka 2012 na kuzikwa Babati mkoani Manyara.