Bajeti yawakuna wazalishaji wa vinywaji vikali

Muktasari:

Akiwasilisha bungeni mapendekezo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/19 wiki iliyopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali inapendekeza kuanzisha mfumo mpya wa stempu za kodi za kielektroniki utakaoanza kutumika Septemba Mosi.

Dodoma. Wazalishaji wa vinywaji vikali nchini wameeleza kufurahishwa na bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2018/19 kwa kuwa na mapendekezo ambayo wanaamini yatamaliza tatizo la uwapo wa bidhaa bandia sokoni.

Akiwasilisha bungeni mapendekezo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/19 wiki iliyopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali inapendekeza kuanzisha mfumo mpya wa stempu za kodi za kielektroniki utakaoanza kutumika Septemba Mosi.

“Mfumo mpya wa stempu za kodi za kielektroniki utaiwezesha Serikali kutumia teknolojia ya kisasa kupata taarifa sahihi za uzalishaji viwandani na kwa wakati zinazotumika kupanga mipango ya maendeleo ya Taifa,” alisema Dk Mpango.

Alisema mfumo huo mpya pia utaiwezesha Serikali kudhibiti uvujaji wa mapato na kutambua mapema kiasi cha kodi ya ushuru wa bidhaa; kodi ya mapato; na Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) itakayolipwa.

Dk Mpango alisema mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki utadhibiti tatizo la uwapo wa stempu za karatasi za kughushi ambalo linachangia kuwapo bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na zinazoweza kuathiri afya za binadamu.

Wazalishaji wa vinywaji vikali wanaamini soko la bidhaa hizo linachafuliwa na uwapo wa bidhaa zenye stempu za kodi ambazo ni bandia, hivyo kuikosesha Serikali mapato stahiki.

Wanaamini pia kuwa bidhaa hizo bandia husababisha hasara kwa wazalishaji wenye sifa na wanaofuata sheria, ambao huuza bidhaa kwa bei ya juu ikilinganishwa na zile zenye stempu za bandia.

“Hii ni habari njema kwetu, inadhihirisha kuwa Serikali imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda. Hatua hii itasaidia kuondoa stempu za bandia za kodi, hivyo kuisaidia Serikali kuongeza mapato yake,” alisema ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Nyati Spiritz Limited, Rupa Suchak jana.

Wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ya mwaka wa fedha 2018/19, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Suleiman Sadiq alisema kumekuwapo bidhaa bandia za vinywaji vikali na kuna wazalishaji wanaotoa taarifa za uongo kwa Serikali.

“Kamati inaamini Serikali hupoteza matrilioni ya shilingi kutokana na uwapo wa bidhaa za vinywaji vikali zenye stempu bandia za kodi. Serikali inatakiwa ichukue hatua,” alisema Sadiq.

Waziri Mpango Alhamisi iliyopita aliliambia Bunge kuwa mfumo huo unatumika kwa mafanikio makubwa katika nchi za Kenya, Morocco, Uturuki, Malaysia na Uswisi