Balozi Bana: Samia ataendelea alipoishia mtangulizi wake

Balozi Bana: Samia ataendelea alipoishia mtangulizi wake

Muktasari:

  • Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk  Benson Bana amesema mambo yaliyofanywa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano,   John Magufuli ni makubwa yasiyo na mfano lakini ana amini Rais Samia Suluhu ataendeleza zaidi pale alipoishia mtangulizi wake.

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk  Benson Bana amesema mambo yaliyofanywa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano,   John Magufuli ni makubwa yasiyo na mfano lakini ana amini Rais Samia Suluhu ataendeleza zaidi pale alipoishia mtangulizi wake.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC, Dk Bana ambaye kabla ya kuwa balozi alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) amesema, “Hayati Magufuli Mungu alimleta duniani ili kuwatumikia Watanzania, ilikuwa ni zawadi ya mwenyezi Mungu kwa Watanzania. Mambo makubwa aliyoyatimiza hapa duniani  wakati wa uongozi wake ni makubwa mno, hayana mfano.”

Bana amesema hakuwahi kufanya kazi binafsi na Rais Magufuli hata alipomchagua alijiuliza kwa nini yeye, “niliwahi tu kupokea simu yake mara moja akinidokeza kuwa anataka kunipa kazi nyingine ya kufanya na hakuitaja nilijua tu kusikia tu baadaye kwa watu waliosikiliza redioni.”

Kuhusu Rais Samia amesema ni kiongozi mahiri na mama mwenye uchungu na nchi, mwenye uzoefu wa kutosha mwadilifu ambaye ameshiriki kikamilifu kuinadi ilani ya CCM na kwamba hana wasiwasi atalivusha Taifa vyema akifuata nyayo za mtangulizi wake.

Akizungumzia uteuzi wa waziri wapya wa mambo ya nje, Dk Bana amesema ni mahiri katika uwanja wa kidiplomasia kwani amekaa wizarani akiwa ofisa, balozi, mkuu wa idara, katibu mkuu na mwanazuoni katika diplomasia.

Kuhusu mahusiano ya Tanzania na nchi za Afrika Magharibi ambako yeye ndiye mwakilishi wa nchi katika mataifa hayo, “kwa upande wa Nigeria sisi kazi yetu kubwa ni kushirikisha watu wa Nigeria wenye mitaji kuweza kuwekeza katika Taifa letu, kwa hiyo kazi yetu kubwa ni kutafuta wawekezaji. Tangu nimefika Nigeria nimekutana na jumuiya ya wafanyabiashara ya Abuja, Legos, jimbo la Kano na jimbo la Kaduna.”

Amesema kwa sasa kuna kampuni kubwa tano ya Nigeria ambazo yaliyowekeza Tanzania ikiwemo kampuni ya Dangote.