Balozi Maulidah: Kiswahili kitumike kama nyenzo ya biashara, uwekezaji
Muktasari:
- Hafla hiyo pia, iliambatana na mdahalo uliowashirikisha Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa Kanga Project Zanzibar, Muna Ally, Profesa Ibrahim Bakri Al Noor na mwanahistoria Riadh Al Busaidi.
Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Oman, Maulidah Hassan, amesema ni wakati kwa lugha ya Kiswahili kutumika kama nyenzo ya kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Oman na nchi za Afrika Mashariki.
Amesema Kiswahili kimebeba fursa za maendeleo kuliko ilivyowahi kufikiriwa awali, akidokeza Oman ina nafasi ya kipekee katika historia ya lugha hiyo, kwa kuwa ndiyo nchi yenye watu wanaoizungumza zaidi nje ya Afrika.
Ujumbe huo umetolewa, jijini Muscat nchini Oman, katika maadhimisho ya Kiswahili, yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman na kuwakutanisha wanadiplomasia, wasomi na wadau wa utamaduni.
Maadhimisho hayo yamefanyika miaka mitano tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) litangaze rasmi Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.
Akifungua maadhimisho hayo, Balozi Maulidah, amesema Unesco ilipoitambua lugha ya Kiswahili ilithibitisha kile ambacho mamilioni ya watu duniani walikuwa tayari wanakifahamu kuhusu nafasi ya lugha hiyo katika jamii.
Amesema Kiswahili si lugha ya mawasiliano pekee, bali imebeba amani, utambulisho, mshikamano na historia ya watu waliounganishwa kwa karne nyingi kupitia Bahari ya Hindi.
Balozi Maulidah, amesema Oman ina nafasi ya kipekee katika historia ya Kiswahili kwa sababu ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wazungumzaji wa lugha hiyo nje ya Bara la Afrika.
“Kiswahili si lugha ngeni inayofundishwa darasani tu, bali ni sehemu ya maisha ya kila siku na urithi unaopitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine,” amesema.
Kwa muda mrefu, amesema Kiswahili kimekuwa lugha ya kumbukumbu kwa Wa-Oman wengi wanaotambua asili ya familia zao na mahusiano ya kihistoria na watu wa Afrika Mashariki.
“Kwa Wa-Oman wengi, kuzungumza Kiswahili ni njia ya kuendelea kuwasiliana na historia yao, ndugu zao na urithi wao ulioko upande mwingine wa Bahari ya Hindi,” amesema.
Hata hivyo, balozi huyo amesema wakati umefika wa Kiswahili kutazamwa kwa jicho jipya, si kama lugha ya historia pekee, bali kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi.
Amesema wafanyabiashara wa Oman wanaozungumza Kiswahili wana faida ya kipekee wanapoingia katika soko la Afrika Mashariki lenye mamilioni ya watu kwa sababu tayari wanashiriki lugha moja na washirika wao wa biashara.
Amesema maneno mengi yanayotumika katika shughuli za biashara yanaeleweka kwa urahisi katika pande zote mbili na hivyo kujenga mazingira ya kuaminiana.
Ameeleza uwezo wa kuwasiliana kwa lugha moja huondoa vikwazo vinavyochelewesha biashara na uwekezaji, jambo linalochochea zaidi ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania, Oman na ukanda wa Afrika Mashariki.
Ametaja baadhi ya vyakula vinavyoendana kitamaduni kati ya Afrika Mashariki na Oman ni pilau, maandazi, chapati na maharage ya nazi.
Kwa upande wa mavazi, ametaja baibui, kanzu na khanjar yanaendelea kuwa vielelezo vya namna tamaduni hizo zilivyoshirikiana.
Kuhusu muziki, amesema ala na midundo inayopatikana katika maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki na Oman inaonesha wazi mizizi ya historia iliyodumu kwa karne nyingi.
“Tunafanana katika chakula, mavazi na hata muziki. Haya yote yanaonesha kuwa mahusiano yetu ni makubwa zaidi kuliko yale yanayoonekana katika vitabu vya historia,” amesema.
Balozi Maulidah, amesema historia ya Oman na Tanzania ilijengwa na upepo wa Kaskazi na Kusi uliokuwa ukisukuma majahazi yaliyovuka Bahari ya Hindi karne nyingi zilizopita.
Amesema majahazi hayo hayakusafirisha viungo, vitambaa na bidhaa pekee, pia yalibeba familia, urafiki, imani na utamaduni ulioendelea kuunganisha watu.
Kwa sababu hiyo, amesema jukumu la kizazi cha sasa ni kutumia urithi huo wa kihistoria kujenga sura mpya ya ushirikiano inayozingatia diplomasia ya uchumi, uwekezaji, utalii, usafirishaji, kilimo na uchumi wa buluu.
“Tunapaswa kufufua mahusiano hayo ya kihistoria na kuyatumia kujenga mustakabali wenye manufaa zaidi kwa wananchi wa Tanzania na Oman,” amesema.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa burudani ya taarab, maonyesho ya utamaduni na vyakula vya asili vya Kiswahili.
Hafla hiyo pia, iliambatana na mdahalo uliowashirikisha Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa Kanga Project Zanzibar, Muna Ally, Profesa Ibrahim Bakri Al Noor na mwanahistoria Riadh Al Busaidi.
Akizungumza katika tukio hilo, Muna amesema khanga imekuwa sehemu ya maisha ya watu wa mwambao wa Bahari ya Hindi kwa karne nyingi na imeendelea kubeba utambulisho wa jamii hizo.
Amesema katika baadhi ya maeneo ya Oman na Mombasa, vazi hilo bado linajulikana kwa jina la leso, lenye asili ya Kireno lililoendelea kutumika kwa miaka mingi.
Kwa upande wa Tanzania, amesema jina la kanga limeendelea kutawala na kuwa sehemu ya utambulisho wa mwanamke wa Kiswahili na jamii nyingi za Afrika Mashariki.
Mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman, Dk Mohammed Al Balushi, huku wawakilishi wa Unesco, Chuo Kikuu cha Nizwa na Kituo cha Utamaduni cha Russia wakishiriki pia.
Vyombo mbalimbali vya habari vya Oman vikiwemo Muscat Daily, Oman Observer, Oman TV na Gazeti la Kiarabu la Oman vilifuatilia maadhimisho hayo na kuripoti matukio mbalimbali yaliyofanyika.