Balozi Ruhinda azikwa, Jaji Warioba akisema ‘hakuwa chawa’

Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wakiwa wamebeba Jeneza lenye mwili wa Balozi Ferdinand Ruhinda,katika makaburi ya Kondo - Ununio wakati wa mazishi yaliyofanyika leo ,jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Mwili wa Balozi Ferninard Ruhinda (86) umezikwa katika makaburi ya Kondo yaliyopo Ununio, Dar es Salaam huku watu waliomfahamu wakimwelezea kwa mitizamo mbalimbali.

Dar es Salaam. Safari ya maisha ya hapa duniani ya Balozi Ferninard Ruhinda (86) imehitimishwa kwa mwili wake kuzikwa katika makaburi ya Kondo, yaliyopo Ununio, Dar es Salaam huku viongozi mbalimbali wa Serikali na wastaafu wakimwelezea utendaji wake hakujikweza, kutaka vyeo wala kuwa chawa.

Balozi Ruhinda, aliyefariki dunia Juni 14, 2024 akiwa nyumbani kwake Masaki, mwili wake umezikwa leo Jumatatu Juni 17, 2024. Awali mwili ulipelekwa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT), Masaki, kulipofanyika ibada.

Mwanadiplomasia huyo ameelezewa alikuwa mtendaji na mchango wake kwenye tasnia ya habari alichangia kuanzishwa kwa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na enzi za uhai wake alisimamia weledi na kujenga uhusiano mzuri na wafanyakazi wake.

Akihudumu kwenye nafasi ya ubalozi alihakikisha uhusiano baina ya Tanzania na China hauvunjiki, akilieleza Taifa la China kwa nini undugu baina ya mataifa hayo unapaswa kuendelezwa.

Wawakilishi wa Serikali wamemtaja Balozi Ruhinda kama mzalendo aliyepanda mbegu kwa kazi zake.

Ibada ya kuaga mwili wa balozi huyo iliongozwa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Manford Kijalo kwa saa moja na nusu saa 7:24 mchana hadi 8:16 mchana na baada ya mahubiri alikaribisha salamu za rambirambi kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wa Serikali, wastaafu na ndugu, jamaa na marafiki.

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akimwelezea Balozi Ruhinda amesema alikuwa kiongozi aliyesimamia hoja zake.

"Hakuwahi kuwa chawa wa mtu, alisimamia hoja zake, alikuwa na misimamo yake, hakuwa mtu wa kutegemea vyeo na hakupenda siasa za majukwaani, kwa namna alivyojiweka watu walimtafsiri kuwa mtu mwenye dharau, tofauti na uhalisia," amesema. Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Aziz Mhina amesema Balozi Ruhinda alikuwa miongoni mwa wanadiplomasia wachache nchini waliotumia vyombo vya habari kutoa elimu juu ya maendeleo.

"Aliaminiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere kushika nafasi ya ubalozi nchini Canada, China na Sweden na alikuwa miongoni mwa watu waliomshawishi Hayati Rais Benjamin Mkapa kugombea urais mwaka 1995 na alikuwa mwenyekiti wa kampeni," amesema Jaji Warioba.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amemtaja Balozi Ruhinda kama mzalendo ambaye Serikali itaendelea kumkumbuka daima.

"Alikuwa muungwana sana, aliacha kazi zake zijisemee zenyewe, maisha ya balozi wetu ni fundisho kwetu vijana kuipenda na kuijenga nchi yetu," amesema Waziri Nape.

Mwasisi wa MCL

Kuhusu mchango wake kwenye vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema japo hakufanya kazi na Balozi Ruhinda, lakini kwa simulizi alizopatiwa wakati wa uanzishwaji wa Gazeti la Mwananchi alitaka liwe huru, liwe linatoa maendeleo kwa Taifa.

"Msingi huo ndio aliutumia Mzee (Theophil) Makunga kuanzisha Gazeti la Mwananchi, hata Kampuni ya Nation Media Group ya nchini Kenya ilipokuja Tanzania kufanya uwekezaji ilizungumza na kampuni mbalimbali, bahati ikaangukia Kampuni ya Mwananchi kwa sababu misingi yake iliendana na Nation Media Group," amesema.

Machumu amesema kutokana na maelewano aliyokuwa nayo Balozi Ruhinda na Hayati Rais Benjamin Mkapa wakati wa uongozi wake ndio uliofanikisha kuishawishi Kampuni ya Nation Media kuja kuwekeza nchini.

Kwa upande wa magazeti ya Serikali ambayo Balozi Ruhinda nako alihudumu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Aisha Dachi amesema balozi huyo alihakikisha tasnia ya habari inasonga mbele.

"Alisaidia kujenga uweledi kwenye tasnia ya habari, kwa muda aliohudumu alihakikisha weledi wake unakuwa dira," amesema.

Upande wa Magazeti yanayomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), Uhuru na Mzalendo, Mhariri Mtendaji wa Uhuru Publications Limited (UPL), Ramadhani Mkoma amesema Balozi Ruhinda ndiye aliyesaidia wafanyakazi wengi wa kampuni hiyo kwenda masomoni.

"Alijenga mahusiano mazuri na wafanyakazi, alihimiza unadhifu wa wafanyakazi na wakati kampuni inapitia changamoto ya fedha alitoa msaada wa gari kwa kampuni," amesema.

Awali, katika misa ya kuuga mwili wa kiongozi huyo, Mchungaji Kiongozi wa KKKT Msasani Manford Kijalo amesema kupitia msiba huo watu wanapaswa kujitafakari namna wanavyoishi.

"Watu wanapaswa kujitafakari maisha wanavyoishi wanaaminika, maisha aliyopewa mwanadamu na Mungu ni kwa ajili ya watu wengine, tunaishi katika nyakati na majira ya Mungu hakuna mtu anayeweza kujipangia namna ya kuishi,"amesema.


Historia ya Balozi Ruhinda

Akisoma historia ya Hayati Balozi Ruhinda, mmoja wa watoto wa familia hiyo, Pamela Ruhida akitumia dakika saba (saa 07:35 hadi 07:44) mchana, amesema balozi huyo alizaliwa Karagwe mkoani Kagera mwaka 1938.

Amesema Balozi Ruhinda ameanza elimu ya msingi mkoani Kagera na baadaye kujiunga na elimu ya Sekondari ya Bwiru Mkoa wa Mwanza. Masomo ya uandishi wa habari kwa ngazi ya Stashahada nchini Kenya na kuchukuwa mafunzo ya muda mfupi Marekani na China.

Baada ya hapo alipata nafasi ya kuwa Ofisa Maendeleo wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro alikofanya kazi kwa muda na kuelekea Shirika la Habari Tanzani akifanya kazi Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kabla ya kujiunga na Uhuru na baadaye Daily News kama Mhariri Mtendaji wa magazeti ya chama na Serikali miaka ya 1970.

Akiendea utumishi wa nafasi ya ubalozi, Ruhinda aliteuliwa  kuwa Ofisa katika ubalozi wa Tanzania nchini Sweden,  Canada (1983 - 1988)  China (1989 – 1992) na kwenye tasnia ya habari nafasi yake aliyoitumikia ni Mhariri vyombo vya habari nchini na mmoja wa waasisi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na Redio Uhuru.

Amesema marehemu ameacha watoto watatu--- wa kike wawili na wa kiume mmoja na wajukuu wanne.