Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balozi Suleiman aeleza ‘unga’ unavyowagharimu Watanzania China

Balozi wa Tanzania nchini China, Suleiman Haji Suleiman akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Balozi wa Tanzania nchini China, Dk Suleiman Haji Suleiman amesema ubalozi umekutana na visa vingi vya Watanzania waliokamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya na sasa wanatumikia adhabu katika magereza ya China.

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini China, Dk Suleiman Haji Suleiman amesema dawa za kulevya zinaendelea kuwagharimu Watanzania wanaokwenda China na kuwa baadhi yao wamehukumiwa vifungo vya miongo kadhaa huku familia zao nchini zikipoteza mawasiliano nao na kudhani wamefariki dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), jijini Dar es Salaam, leo Julai 14, 2026, Dk Suleiman amesema ubalozi umekutana na visa vingi vya Watanzania waliokamatwa kwa makosa hayo na sasa wanatumikia adhabu katika magereza ya China.

Ametoa mfano wa mama mmoja aliyefika kwenye banda la Ubalozi wa Tanzania wakati wa Maonesho ya Sabasaba akieleza kuwa aliarifiwa mwanaye aliyekuwa China amefariki akiwa gerezani.

“Baada ya kuchukua taarifa zake na kuzifuatilia, tulibaini kijana huyo yupo hai na anaendelea kutumikia kifungo chake. Anatarajiwa kumaliza adhabu mwaka 2031,” amesema.

Katika tukio jingine, amesema ubalozi ulifuatilia taarifa za mwanamke mmoja aliyekamatwa nchini China mwaka 2015 akiwa na dawa za kulevya akahukumiwa mwaka 2019 na anatarajiwa kumaliza kifungo chake mwaka 2045.

Balozi wa Tanzania nchini China, Suleiman Haji Suleiman akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Amesema kwa kipindi chote hicho, familia yake iliyopo hapa Tanzania ilikuwa imekata tamaa na kuamini amefariki baada ya kupoteza mawasiliano naye alipokuwa akifanya biashara ya vitenge kati ya Tanzania na China.

“Nawapa picha ndugu zangu kuwa suala la dawa ya kulevya si la kuchezea,” amesema Balozi huyo.

Ameongeza kuwa wanawake wanaonekana kwa wingi kuwa miongoni mwa Watanzania wanaokamatwa kwa makosa hayo, akieleza kuwa wengi huingia kwenye mtandao huo baada ya kuanza safari za kawaida za biashara.

“Atabeba vitambaa mara ya kwanza na ya pili, baadaye anashawishiwa kubeba ‘unga’. Lakini China wana mifumo imara ya ukaguzi. Ukijaribu kupitisha dawa hizo watakukamata tu,” amesema.

Ameonya kuwa sheria za China dhidi ya dawa za kulevya ni kali na hazitoi nafasi kwa anayebainika kufanya kosa hilo, hivyo amewasihi Watanzania wanaokwenda nchini humo kuwa waangalifu na kutokubali kubeba mizigo wasiyoifahamu kwa ahadi za kupata fedha.

“Sisi kama ubalozi tunaendelea kutoa elimu, lakini niwasihi vijana wajilinde. Wapo ndugu zetu wengi wanaendelea kuteseka magerezani kwa sababu ya dawa za kulevya. Wachina hawana mchezo kwenye suala hili,” amesema.