Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DCEA yakamata tani 22.6 za dawa za kulevya

Mirungi inayodaiwa kukamatwa katika opareshi iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) katika mikoa mbalimbali katika kipindi cha mwezi Mei na Juni, 2026.

Muktasari:

  • Pia magari sita likiwamo fuso lililokuwa limebeba shehena ya mirungi iliyohifadhiwa kwa matenga ya nyanya yamekamatwa

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata tani 22.6 za dawa za kulevya na lita 30.5 za vinywaji vya kuongeza nguvu nyenye viambata vya dawa za kulevya pamoja na kilo 19.94 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Pia, watu 188 wamekamatwa katika opereshi iliyofanywa na DCEA mikoa mbalimbali nchini kuanzia Mei hadi Juni 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Julai 2, 2026, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema mtuhumiwa mmoja alikutwa na kilo 106.04 za dawa za kulevya aina ya mirungi zilizokuwa zikisafirishwa kwa kutumia gari aina ya Toyota Premio.

Katika operesheni hiyo, Lyimo amesema wamekamata pia magari sita likiwamo fuso lililokuwa limebeba shehena ya mirungi iliyohifadhiwa kwa matenga ya nyanya.

Pia, amesema wamekamata bajaji mbili na pikipiki 33 zikihusishwa na mtandao wa biashara hiyo haramu na kuteketeza ekari 228.5 za mashamba ya bangi na mirungi.

Aidha, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), amesema walifanya ukaguzi na uchunguzi wa bidhaa katika duka la bidhaa la village supermarket la jijini Dar es Salaam na kubaini uwepo wa vinywaji vya kuongeza nguvu vyenye viambata vya kemikali ya THC ambayo hupatikana kwenye dawa za kulevya aina ya bangi.

"‎Katika operesheni hiyo, jumla ya makopo 122 yenye ujazo wa millitita ‎250 kila moja, sawa na lita 30.5 zenye chapa ya ‘TRIP’ yalikamatwa na watuhumiwa ni Syed Abdul Bast (43) raia wa Pakistan na Dhirendra Kumar Gorodhan (45), Mtanzania mwenye asili ya Asia ambao wamekamatwa katika tukio hili," amesema Lyimo.

‎‎"THC ni kemikali inayopatikana kwenye dawa za kulevya aina ya bangi ambayo ina madhara mbalimbali kwa mtumiaji ikiwamo, kuamsha magonjwa ya akili, kubadili utendaji kazi wa mfumo wa fahamu kuchochea vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi, unyang`anyi, ukatili na kuchochea matumizi ya dawa nyingine za kulevya," amesema.

Kamishna huyo amesema katika eneo la mizigo inayosafirishwa nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere( JNIA), walikamata kilo 19.9 za bidhaa zilizoandikwa ni virutubisho vya lishe aina ya AFA CELL (Moringa Extract) na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa maabara imebainika bidhaa hizo zilikuwa na kiambata cha Prazepam.

Amesema bidhaa hizo ziliingizwa nchini kutoka Malaysia na kuandaliwa kusafirishwa kwenda Barbados katika visiwa vya Karibiani.

Amesema watuhumiwa ni Agustino Ismaely (30), mkazi ‎wa Kimara; Zamia Upunda (23), mkazi wa Bungoni, llala na Habiba Ally Mziga (54), mkazi wa ‎Mbezi Makonde wamekamatwa kwa ajili ya uchungzi.

‎Akifafanua zaidi, amesema ‎Prazepam ni dawa tiba yenye asili ya kulevya iliyopo katika kundi la benzodiazepine inayotumika kutibu ‎magonjwa mbalimbali ikiwamo wasiwasi, msongo wa mawazo na kukosa usingizi.

"Endapo dawa hizi zitatumika kiholela au bila maelekezo ya daktari zinaweza kusababisha uraibu, kuharibu mfumo wa fahamu, mfumo wa upumuaji, kupoteza fahamu na hata kifo," amesema Lyimo.

Vilevile amesema ukamataji ulifanyika katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na maeneo mengine ya nchi, huku tani 19.5 za bangi, tani 2.6 za mirungi, kilogramu 40 za skanka na kiasi cha heroin zilinaswa.

Lyimo amesema mashamba ya bangi yaliyokuwa Dodoma, Lindi, Geita na Sengerema pia yaliteketezwa katika operesheni hizo.

Katika hatua nyingine, amesema mamlaka hiyo imeongeza ushirikiano na mamlaka za Eswatini, Afrika Kusini, Msumbiji na Zambia kufuatilia Watanzania wanaodaiwa kuhusika na mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya waliokimbilia katika nchi hizo.

"Mpaka sasa Watanzania 28 wamekamatwa katika nchi hizo na walipohojiwa wameelezwa kuwa, wamekimbia nchini kwako na kwenda huko kutokana na sheria kali zilizopo hapa nchini, hata hivyo tunaendelea na ushirikiano kuona ni namna gani watu hao tuwalete ili tuwafungulie mashtaka," amesema.

Hata hivyo, amesema operesheni za pamoja zitaendelea sambamba na ukaguzi wa bidhaa, dawa na virutubisho ili kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia na kulinda afya za wananchi na amani.

Emmanuel Mkiligi ni Meneja wa Ukaguzi na Kudhibiti wa Dawa TMDA, amesema bidhaa hiyo na vinywaji hivyo ni hatari kwa afya, hivyo wataendelea kushirikiana kwa pamoja na taasisi nyingine ili kubaini makundi hatarishi na kuimarisha afya na hali ya usalama wa nchi

Meneja Ukaguzi na Utekelezaji wa Sheria TBS, Nuru Mwasulama amesema bidhaa zilizokamatwa katika operesheni hiyo hazikuwa na ithibati ya ubora inayotokewa na shirika hilo, hivyo bidhaa hizo hazikusajiliwa.