Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Barabara mto wa Mbu-Loliondo kugharimu Sh24 bilioni, mkandarasi aonywa

Meneja wa Wakala wa barabara(Tanroads)mkoa wa Arusha,Mhandisi Regnald Massawe(kushoto) na Afisa Mkuu wa kampuni ya ujenzi ya China,China Wu Yi Co.Ltd, Li Wen Lan wakionesha mikataba ya ujenzi wa barabara kilometa 10 leo,wanaoshuhudia ni Mkuu wa mkoa wa Arusha,Paul Makonda na Katibu Tawala mkoa, Missalie Musa.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemwagiza mkandarasi kukamilisha ujenzi ndani ya muda ulioelekezwa kwenye mkataba ili kutekeleza mkakati wa Serikali kuwaunganisha wananchi na barabara za lami.

Arusha. Wakala wa Barabara Mkoa wa Arusha (Tanroads) na kampuni ya ujenzi ya China Wu Yi Co.Ltd wamesaini mkataba wa ujenzi wa barabara kwa awamu ya pili ya kilomita 10 kutoka mji mdogo wa Wasso hadi Loliondo kwa gharama ya Sh24 bilioni.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akizungumza kwenye hafla hiyo leo Jumatatu Juni 9, 2025, amemtaka mkandarasi kuheshimu masharti ya mkataba na kuutekeleza ndani ya muda aliopewa.

Makonda amesema Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zikiwamo za miundombinu ya barabara, hivyo utekelezaji wake unapaswa kuendana na mikataba inavyoelekeza.

Amesema uboreshaji wa miundombinu ya barabara unarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji, hivyo kuchangia kukua kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo husika.

“Nimeona muda wa utekelezaji wa mradi huu kwenye mkataba ni miezi 12, sitarajii kuona unatoa sababu za kushindwa kutekeleza ndani ya muda tuliokubaliana, naamini itakua chachu muhimu kupewa kazi zaidi. Serikali imejizatiti kuona miundombinu inakua kichocheo cha kukua kwa uchumi wetu,” amesema Makonda.

Katika kuhakikisha miundombinu inaendelea kuimarishwa, mkuu huyo wa mkoa amesema Serikali imetenga Sh11 bilioni kutengeneza upya madaraja mbalimbali yanayoelemewa na maji kipindi cha mvua.

Amesema madaraja hayo ni yale yaliyopo kati ya barabara ya Arusha na Mkoa wa Kilimanjaro kuelekea nchini Kenya.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Mhandisi Regnald Massawe amesema  ujenzi huo wa barabara ya Mto wa Mbu hadi Loliondo yenye urefu wa kilomita 217, katika awamu ya kwanza zilijengwa kilomita 49 kutoka Wasso hadi Kijiji cha Sale  kwa  kiwango cha lami na ulikamilika  mwaka 2022 kwa gharama ya Sh87 bilioni.

Mhandisi Massawe amesema  kukamilika kwa mradi huo  kutachochea maendeleo kwa wakazi wanaoishi katika wilaya ya Ngorongoro hasa vijiji vya Wasso, Sale pamoja na mji wa Loliondo sambamba na ukuaji wa vijiji ambavyo barabara hiyo inapita.

Amesema kabla ya ujenzi wa kilomita 49 haujakamilika, muda kutoka Arusha hadi Loliondo ilikua ni saa 12 lakini sasa ni saa saba pekee na mradi wote utakapokamilika umbali huo utachukua muda saa tatu.

Aidha, ameongeza kuwa umuhimu wa barabara hiyo ni mkubwa kutokana na eneo hilo kuwa na vivutio vya utalii kuelekea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Oldonyo Lengai, Ziwa Natron na Engaruka lenye magadi soda ambalo Serikali inakusudia kujenga kiwanda kikubwa.