Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Barabara ya Ubungo –Kimara mwisho yaanza upanuzi

Shughuli ya upanuzi wa kipande cha Barabara ya Morogoro kutoka Ubungo hadi Kimara mwisho ikiendelea. Picha na Tuzo Mapunda

Muktasari:

  • Mradi wa upanuzi wa kipande cha Barabara ya Morogoro kutoka Ubungo hadi Kimara mwisho waanza, Tanroad yaeleza shughuli hiyo itadumu kwa kipindi cha miezi 18

Dar es Salaam. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam umesema mradi wa upanuzi wa kipande cha Barabara ya Morogoro kutoka Ubungo hadi Kimara mwisho kufikia njia nane umeanza kutekelezwa.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa na Kampuni ya Kichina ya Sichuan Road and Bridge Group (SRBG) tangu Novemba 2023, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18, lengo likiwa ni kukamilisha kipande hicho chenye njia sita kilichobakia kufikia barabara nane hadi Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Akizungumzia mradi huo, Mkuu wa Kitengo cha miradi kutoka Tanroad, Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Mwanaisha Rajabu amesema katika upanuzi huo kutakuwa na barabara ya huduma kwa maana ya 'Service road' na njia za watembea kwa miguu kila upande.

"Tuna mradi unaoendelea eneo wa upanuzi wa barabara ya Ubungo hadi Kimara inapanuliwa kuwa na njia nane kwa maana tatu za magari ya mchanganyiko (kawaida), moja kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka na upande wa pili itakuwa hivyohivyo," amesema Mhandisi Mwanaisha.

Mwanaisha amesema matarajio yao mradi utakamilika ndani ya miezi 18 yaani Mei 2025.

"Tayari mkandarasi ameweka kambi maeneo ya Ubungo karibu na kituo cha mabasi yaendayo haraka upande wa kushoto na kulia.”

"Hata baada ya Kimara kwa sehemu ya mbele maeneo ya Stop Over upande wa kushoto kuna sehemu kumezungushwa mabati nako ni sehemu ya mkandarasi anayefanya kazi," amesema  Mhandisi Mwanaisha.

Amesema baada ya ujenzi huo kukamilika barabara ya Ubungo hadi Kimara itakuwa na njia nane kama ilivyo Kimara kwenda Kibaha, pia  kutakuwa na njia za huduma na watembea kwa  miguu kwa kiwango cha lami.

"Kuanzia kimara hadi ubungo Mkandarasi tayari ameanza kusafisha eneo la ujenzi na kuanza kujaza kifusi sehemu zinazohitajika," amesema

Walivyojipanga

Mhandisi Mwanaisha amesema ujenzi huo  hautaathiri kwa kiwango kikubwa shughuli za usafirishaji katika kipande hicho.

 "Tumejipanga kutovuruga na bahati nzuri barabara yetu ina njia sita na ongezeko ni njia mbili yaani moja kila upande na njia za huduma na kwa kiasi kikubwa.”

"Eneo linalojengwa halina njia kwa sasa kwa hiyo barabara zilizopo zitaendelea kutumika na zitaathirika kidogo tu, hasa pale zitakapoguswa kama kuondoa sehemu za mfereji kuwa sehemu ya njia ya watembea kwa miguu,” amesema.

Matarajio Tanroads

Mhandisi Mwanaisha amesema baada ya kumaliza upanuzi huo ndani ya kipindi hicho wanatarajia kuondoa msongamano wa foleni ya magari inayojitokeza eneo la Ubungo hadi Kimara.

Mhandisi Mwanaisha amesema hata katika barabara sita zinazotumika sasa kuna sehemu hazina njia za huduma za watembea kwa miguu.

"Mathalani eneo la kutokea Kimara mwisho hadi Korogwe hakuna barabara ya watembea kwa miguu watu wanatumia barabara mbili za magari mchanganyiko.

"Tukipanua kuweka barabara tatu ikiwemo ya watoa huduma foleni itapungua kwa kiasi kikubwa," amesema.