Barabara zote zaelekea Dodoma
Muktasari:
Wajumbe waanza safari, wapambe Arusha wakodi mabasi matatu, polisi watoa tamko
Dodoma. Wakati vikao vya juu vya CCM vikikaribia kuanza mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho, mji wa Dodoma umeanza kupokea wageni kutoka maeneo mbalimbali .
Mkoa wa Dodoma ndiyo sehemu ambayo CCM humpata mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar baada ya kumalizika kwa vikao hivyo vitatu vya juu- Kamati Kuu itakayokutana Julai 9, Halmashauri Kuu (Julai 10) na Mkutano Mkuu (Julai 11-12) - ambavyo hutanguliwa na Kamati ya Maadili na Sekretarieti.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye maeneo ya katikati ya mji wa Dodoma hadi jana, umebaini kuwa tayari nyumba nyingi za kulala wageni na hoteli zimeshajaa.
Hoteli maarufu mjini hapa, St Gasper na Dodoma, ambazo zinatarajiwa kuwa malazi ya vigogo, zimeshajaa. Sehemu hizo zinatarajiwa kuchukua viongozi mashuhuri wa chama hicho wapatao 600, wakati wajumbe wengine wapatao 2,448 wataishi maeneo mengine.
Mbali ya hoteli hizo, mji huu mkuu wa Tanzania una nyumba nyingi za wageni na hosteli, ambazo hutumiwa na wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.
Meneja wa Hoteli ya Royal Village, Zuberi Mpendakazi alisema nafasi kwenye eneo lake haitapatikana kuanzia Julai 6 hadi 12, wakati meneja wa Dodoma Hotel, Wellingstone Maleya alisema vyumba vimejaa kuanzia Julai 6 hadi 13.
Baadhi ya wajumbe wa vikao hivyo ni wabunge ambao tayari wako mjini hapa wakiendelea na Bunge ambalo litavunjwa Julai 9. Wengine waliosalia ni wapambe wa makada waliokuja mjini hapa kurejesha fomu za kuwania urais ambao hawajaondoka.
Baadhi ya mameneja wa hoteli hizo walisema watu hao wataondolewa kuanzia Julai 6 iwapo hawatakuwa miongoni mwa waliopangiwa vyumba.
Uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya wenyeji wameanza kukarabati nyumba zao kwa ajili ya kupangisha wageni mbalimbali.
Polisi watoa onyo
Wakati maandalizi yakiendelea kwenye hoteli, nyumba za wageni, hosteli na maeneo ya biashara, kamanda wa polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime amewahakikishia wageni kuwa jeshi lake limejiandaa vizuri kwa ugeni huo mkubwa utakapoingia, kuishi na hadi kuondoka.
“Natoa onyo kwa mtu yoyote mwenye nia ovu ama kutaka kufanya kitendo chochote cha kuhatarisha usalama, atashughulikiwa kwa nguvu zote za kisheria,” alisema kamanda huyo.
Alisema wajumbe wa mikutano ya CCM, wageni na wananchi watambue kuwa usalama unaanza kwa kila mtu.
“Mtu yoyote atakayeona jambo lolote linaloashiria uhalifu ama si la kawaida, atoe taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua zichukuliwe,” alisema.
Ukarabati wa mwisho
Mwananchi ilishuhudia ukarabati wa ofisi za makao makuu ya CCM ukiwa katika hatua za mwisho na mafundi walikuwa wakipaka rangi nyeupe jengo hilo, maarufu kwa jina la White House, ambako utafanyika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu.
Kikao hicho kitakuwa na kazi ya kuwachuja wagombea 38 waliochukua na kurudisha fomu kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Kwa upande wa mgombea urais wa Zanzibar, Kamati ya Usalama na Maadili ya Zanzibar, itafanya kikao chake leo Julai 4, ikifuatiwa na Kamati Maalumu kesho Jumamosi Julai 5.
Wajumbe waanza safari
Wakati Dodoma ikijiandaa kupokea ugeni ambao unaweza kutoa kutoa Rais wa Tanzania, wajumbe wa vikao hivyo wako katika maandalizi ya mwisho ya safari za kuelekea Dodoma.
Kutoka visiwani, Zanzibar itapeleka kwa mafungu wajumbe 334 kwenye mkutano huo.
Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakary Jabu alisema wajumbe 121 wataondoka Julai 9 kwa ajili ya Halmashauri Kuu na watafuatiwa na wajumbe 213 watakaoondoka Julai 10.
Mkoani Tabora, wajumbe 91 wanatarajia kuondoka Julai 9, kwa mujibu wa katibu wa CCM mkoa, Janeth Kayanda.
Mkoa wa Simiyu utapeleka wajumbe 68 kwenye mkutano huo. Katibu wa CCM, Hilda Kapaya alisema maandalizi ya safari ndiyo yanayofanyika kwa sasa.
Mkoani Kigoma, katibu msaidizi mkoa, Godwin Chacha alisema wajumbe 93 wanajiandaa kwa safari, lakini alisema hajui wajumbe wataondoka lini kwa vile bado wanasubiri fedha kutoka makao makuu ya CCM.
Mkoani Arusha, licha ya kuwa na wajumbe 60, mabasi manne yamekodiwa kupeleka watu hao mjini Dodoma na wapambe zaidi ya 200.
Hadi jana jioni, mabasi manne ya kampuni za Shabiby, Arusha Express na Champion yanayosafiri kati ya jiji la Arusha na Dodoma yalikuwa yameshajaa nafasi za Julai 6 na 7.
“Magari yetu yote manne yanayosafiri kati ya Arusha na Dodoma yamefanyiwa ‘booking’ ya tarehe sita... hatuna nafasi kabisa labda mpaka baada ya tarehe saba,” alisema mmoja wa watumishi wa kampuni ya Shabiby jijini Arusha.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Arusha, Feruzi Bano alisema mkoa huo utapeleka wajumbe 60 katika mkutano huo.
Mkoani Mara, katibu wa CCM wa mkoa, Adamu Ngalawa alisema wajumbe 91 wataondoka kwa mabasi mawili wakiwemo wapambe na wapiga debe wa baadhi ya wagombea.
Hali ni kama hiyo mkoani Tanga ambako katibu wa chama hicho wa mkoa, Shija Othmani alisema wanatarajia kuwa na msafara wa wajumbe 120 wanaoziwakilisha wilaya tisa.
“Tumeandaa usafiri wa mabasi mawili ya Ratco kwa ajili ya kupeleka wajumbe wetu Dodoma... Maandalizi yote yamekamilika na wanatarajiwa kuwasili huko Julai 10,” alisema.
Mjini Morogoro, katibu wa CCM wa mkoa, Rojas Ramuli alisema watapeleka wajumbe 96 kwenye mkutano huo na wataanza kuondoka Julai 10.
“Kwa sasa tunahangaikia usafiri wa wajumbe wetu, tunachotaka tuhakikishe wote wanakuwa Dodoma,” alisema.
Mkoa wa Pwani umepanga kupeleka wajumbe 99 katika mkutano huo huku wajumbe wa Halmashauri Kuu wakiwa wanne na Mkutano Mkuu ni 95.
Akizungumza kwa niaba ya katibu, mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Maulid Bundala alisema kuwa kwa sasa wanasubiri sekretarieti ya Kamati Kuu ndipo wataondoka.
Katibu wa itikadi na uenezi wa mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi alisema wajumbe 90 wa mkoa huo watakwenda Dodoma Julai 10.
Wajumbe 70 kutoka Mkoa wa Mtwara wanatarajia kuondoka kuanzia Julai 9 kupitia Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Katibu wa mkoa huo, Shaibu Akwilombe alisema: “Mimi ninachotakiwa kuhakikisha ni wajumbe wangu 70 wanafikaje Dodoma. Nitakodi basi moja tu ili wajumbe hao waweze kufika huko na kushiriki mkutano huo,” alisema.
Mkoani Manyara, katibu wa CCM, Ndengaso Ndekubali alisema wajumbe 86 wameshakamilisha maandalizi tayari kwa mkutano na wataondoka Julai 9 kwenda Dodoma.
Mkoa wa Rukwa umepanga kutuma wajumbe 60, kwa mujibu wa katibu wa itikadi na uenezi wa mkoa, Clement Bakuli.
Mkoani Geita, katibu wa chama hicho, Gustavu Muba alisema wamepanga kupeleka wajumbe 69.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake, Muba alisema kuwa wamekodi basi moja kwa ajili ya wajumbe wote na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu walishaanza kutangulia.
Mkoa wa Kagera unatarajia kupeleka ujumbe wa watu 105, kwa mujibu wa katibu wa CCM, Idd Ali Ame.
Katibu huyo alisema kuwa wajumbe wote watakutana Julai 8 mjini Bukoba na kuanza safari siku ya pili.
Sharon Sauwa, Mussa Mwangoka, Peter Saramba, Esther Mwimbula, Sylivester Mkombe, Burhani Yakub, Mary Sanyiwa, Joseph Lyimo, Jackline Masinde, Phinias Bashaya, Florence Focus, Robert Kakwesi, Joyce Joliga, Mwinyi Sadallah, Faustine Fabian na Anthony Kayanda.
mwisho