RC Makalla aagiza miundombinu ya Tanesco, Auwsa kuondolewa kupisha ujenzi
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, akimsikiliza Kaimu Meneja wa Tanroads mkoa wa Arusha, Mhandisi Christopher Saul, alipofanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara za jiji la Arusha eneo la Mbauda unaoendelea leo Jumatatu Juni 22, 2026. Picha na Filbert Rweyemamu.
Muktasari:
- Hatua ya kuondoa miundombinu ya Tanesco na Auwsa katika hifadhi ya barabara itawezesha ujenzi wa barabara ya Mbauda–Tanganyika Packers hadi Losinyai kwa kiwango cha lami, ambayo inaunganishwa na barabara ya mchepuo ya East Africa Bypass.
Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla ameziagiza taasisi zote zilizo na miundombinu ndani ya hifadhi za barabara kuiondoa mara moja ili kumwezesha mkandarasi anayejenga barabara za njia nne kutekeleza kazi yake kwa kasi na kwa wakati uliopangwa.
Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Juni 22, 2026, wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa barabara ya Mbauda–Tanganyika Packers hadi Losinyai kwa kiwango cha lami, ambayo inaunganishwa na barabara ya mchepuo ya East Africa Bypass, mradi unaotarajiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma na miundombinu kuelekea na kutoka katika uwanja wa michezo wa Afcon.
Amesema uondoaji wa haraka wa miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (Auwsa), utaondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha ujenzi wa barabara hizo muhimu, hasa katika kipindi hiki cha maandalizi ya michuano ya Afcon na matumizi ya baadaye ya miundombinu hiyo.
“Natoa maagizo kwa taasisi zote za umma na nyingine kuhamisha miundombinu yao haraka ili kumwezesha mkandarasi kutimiza majukumu yake kwa wakati. Hatutaki awe na kisingizio cha kushindwa kutekeleza mradi huu kwa sababu ya miundombinu ya taasisi za umma,” amesema Makalla.
Aidha, amesisitiza kuwa barabara hizo ni muhimu kwa maendeleo ya Jiji la Arusha na kumtaka mkandarasi, kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), kuendelea na kazi kwa kasi, akibainisha kuwa tayari imelipwa malipo ya awali ya Shilingi bilioni 17.
Ameitaka kampuni hiyo kuzingatia ratiba ya kukamilisha mradi huo ifikapo Juni 2027, ili barabara hizo ziweze kupitika wakati wa michuano ya Afcon itakayofanyika Agosti mwaka huo.
Mradi huo wa barabara unaogharimu Sh221 bilioni utaendelea kutekelezwa katika maeneo mengine baada ya vipande vya kipaumbele kukamilika.
“Nimekuja kuwasukuma muendelee na kasi ileile mliyokuwa nayo kwenye miradi mingine mliyotekeleza katika mikoa mbalimbali. Hapa Arusha nataka muonyeshe ubora wa hali ya juu. Barabara zote zinazoelekea uwanja wa Afcon zikamilike kwa wakati uliopangwa,” amesema Makalla.
Amezitaja barabara za kipaumbele kuwa ni Arusha hadi Kisongo inayojengwa kwa njia nne, Kisongo hadi uwanja wa Afcon, Mbauda hadi East Africa Bypass na Kona ya Kiseriani, huku akibainisha kuwa maeneo mengine ya mradi yenye urefu wa kilometa 70 yataendelea baadaye.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Arusha (Tanroads), Mhandisi Christopher Saul, amesema mkandarasi ameeleza kuwa kipande cha kilometa 13 ndani ya Jiji la Arusha kimepewa kipaumbele kwa kuwa ni sehemu muhimu ya njia za kuelekea uwanja wa Afcon 2027.
Amesema Tanroads imepokea maelekezo yote ya Mkuu wa Mkoa na itashirikiana na taasisi za Tanesco na Auwsa kuhakikisha miundombinu ya maji na umeme inahamishwa ili kuwezesha ujenzi kukamilika ifikapo Juni 2027 kama ilivyopangwa.
Naye Meneja Mradi wa kampuni ya CCECC, Mhandisi Liu Nanjing, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati, akisema kampuni yake ina uzoefu wa kutekeleza miradi mikubwa kwa ubora unaokubalika kimataifa.
Amesema ujio wa Mkuu wa Mkoa umewapa motisha ya kuongeza kasi ya kazi, akibainisha kuwa kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali nchini na kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania, wakiwemo wa Mkoa wa Arusha, sambamba na kuzingatia masharti ya kimkataba, ikiwemo masuala ya mazingira na ushirikishwaji wa kijinsia katika ajira.