Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baruti zauzwa jirani na Ikulu Dar

Ikulu ya Tanzania

Muktasari:

“Mimi ni msemaji wa taifa kwa jumla, sasa naomba masuala hayo ya kuuzwa kwa baruti, zinazotumika katika  uvuvi haramu katika soko hilo mumuulize Kamanda Kova, yeye ndiye anaweza kulizungumzia suala hilo,”alisema Senso.

BARUTI zilizotengenezwa maalumu kwa ajili ya kulipua miamba, sasa zimezagaa katika Soko la Samaki la Kimataifa, lililopo Feri jijini Dar es Salaam, jirani na Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete, zikiuzwa kwa ajili ya kutekeleza uvuvi haramu wa samaki katika Bahari ya Hindi.

Biashara hiyo inadaiwa kufanywa na baadhi ya askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wanaowatumia mawakala, ambao huziuza kwa watu wanaofanya uvuvi haramu sokoni hapo na kutoka maeneo mengine.

Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa biashara hiyo haramu imekuwa ikifanyika zaidi nyakati za usiku na alfajiri kwa takriban mwaka mmoja sasa.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, baruti hizo huuzwa kati ya Sh20,000 hadi 30,000 pamoja na nyaya zake, ambazo huuzwa Sh5,000.

Gazeti hili lilifika katika soko hilo mwishoni mwa wiki iliyopita na kufanikiwa kununua baruti tano kwa Sh50,000.

Kitaalamu baruti hutumika katika miradi ya ujenzi wa barabara, migodi ya madini pamoja na jeshini kwa ajili ya kulipulia miamba ya mawe.

Akizungumza na gazeti hili, mfanyabiashara wa soko hilo ambaye alisita kutaja jina lake, alisema kuwa baruti hizo mara nyingi hupatikana asubuhi kwa kuwa usiku wahusika wanakuwa wameondoka.

“Kaka unataka baruti, usijali hiyo kitu umepata, lakini unaweza kuja asubuhi ili kufanikisha dili hilo,” alisema mtu huyo na kuongeza:

“Sikiliza nikwambie, sisi tunauza kwa siri kubwa, ukiona hapa baruti hazipatikani, unatakiwa uende eneo linaloitwa Mjimwema (Kigamboni) na  ukienda huko ujipange vizuri (uje na fedha ya kutosha).”

Kauli ya JWTZ
Akizungumzia madai ya askari wa jeshi hilo kujihusisha katika biashara hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa ni vyema watu hao kama wanafanya hivyo wakawekewa mtego na Jeshi la Polisi ili wakamatwe kwani ni kinyume cha sheria.

Alisema kwamba hawezi kusema kama wanajeshi hawahusiki kufanya biashara hiyo, lakini ni vyema Jeshi la Polisi likaweka mitego ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa, kwani biashara hiyo ni kinyume cha sheria na hairuhusiwi kufanywa.

“Sisi kama wanajeshi, silaha aina ya baruti siyo ambayo tunaitumia sana, lakini, kwa wanajeshi kufanya biashara hiyo ni kinyume cha sheria, hata kama wanazo. Tunaomba kama kuna wanajeshi wanafanya hivyo, polisi waweke mtego ili wakamatwe na wao waache kufanya hivyo,” alisema Mgawe na kuongeza:

“Siwezi kukataa moja kwa moja kama hawawezi kufanya hivyo, sasa ili kukomesha vitendo hivyo, lazima polisi waweke mitego wawakamate, waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.”

Kauli ya Waziri
Akizungumzia suala hilo Waziri wa  Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo alisema kwamba anachofahamu yeye ni kuwapo kwa watu wanaovua samaki kwa kutumia baruti, lakini biashara hiyo haitambui.

Alisema kuwa kama biashara hiyo inafanyika ni vyema akapata ushirikiano kutoka kwa gazeti hili ili aweze kuwakamata watu hao ili kukomesha biashara hiyo.

“Mimi ninachokifahamu ni kwamba, kuna baadhi ya watu wasio waaminifu wanavua samaki kwa kutumia baruti kitu ambacho hakikubaliki. Lakini kuhusu kuwepo kwa biashara ya baruti katika soko hilo, mimi sifahamu,”alisema Mathayo na kuongeza:

“Naomba tushirikiane kwa pamoja ndugu yangu, ili twende wote tukawakamate watu hao, ambao wanavunja sheria kwa kufanya biashara haramu.”

Polisi wanasemaje?
Gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Advera Senso ili kupata maelezo yake kuhusu suala hilo ambapo alimshauri mwandishi amtafute Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu  ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ili alizungumzie.

“Mimi ni msemaji wa taifa kwa jumla, sasa naomba masuala hayo ya kuuzwa kwa baruti, zinazotumika katika  uvuvi haramu katika soko hilo mumuulize Kamanda Kova, yeye ndiye anaweza kulizungumzia suala hilo,”alisema Senso.

Hata hivyo, Kamanda Kova alipotafutwa alisema kuwa anayestahili kuulizwa suala hilo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieth Mnangi kwa kuwa eneo hilo ni sehemu yake ya kazi.
“Ndugu yangu  naomba umtafute Kamanda wa Ilala, yeye anaweza kukupa majibu sahihi ya suala hilo,” alisema Kova.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieth Mnangi alipotafutwa alisema kuwa hana taarifa ya kufanyika  kwa biashara hiyo katika soko hilo.
“Unataka nikujibu nini, mimi sina taarifa za kuwepo kwa biashara hiyo kama unavyo sema, ila tutalifanyia uchunguzi kisha tutatoa majibu,” alisema Mnangi.

Uongozi wa soko
Kiongozi wa soko hilo Rajab Ramadhan alisema kuwa walibaini kuwepo baadhi ya watu wanaovua samaki kwa kutumia baruti, ambapo wamekuwa wakitoa  taarifa mara kwa mara kwa Jeshi la Polisi, lakini tatizo hilo limeendelea  kuwa sugu.

“Hutujapata taarifa rasmi kama kuna biashara ya baruti hapa sokoni, lakini suala la uvuvi kwa kutumia baruti tunalitambua. Kwamba kuna watu wanaofanya hivyo ingawa ni kinyume cha sheria,”alisema Ramadhani na kuongeza:

“Kutokana na hali hiyo tumeshatoa taarifa polisi na kuna doria za mara kwa mara, lakini sisi kama uongozi tunaona kuna mtandao unaohusisha vyombo vyenye uwezo wa kudhibiti hali hiyo kwa sababu tatizo la uvuvi wa kutumia baruti lipo kwa kiasi kikubwa katika soko la feri.”