Bashe ataka uwekezaji katika vifungashio

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Muktasari:
- Wakati biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine zikiendelea kupigiwa chapuo huku utafutaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini yakizidi kutafutwa, wenye mitaji wameitwa kuwekeza katika uzalishaji wa vifungashio
Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amewaita watu kuwekeza katika uzalishaji wa vifungashio kwa ajili ya kuchochea uuzaji wa bidhaa za ndani na nje ya nchi.
Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza kuwa kufunguliwa kwa uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kunaisukuma Tanzania kuhakikisha inatimiza vigezo vinavyotakiwa kuanzia namna bidhaa zinavyofungashwa.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 12, 2023 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam kuelezea faida zilizopatikana katika Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini India.
"Kuna fursa kubwa sana katika uzalishaji wa vifungashio vya maboksi kwa ajili ya mazao ya mbogamboga na matunda, ni fursa kubwa sana katika nchi yetu ambayo sehemu kubwa ya vifungashio hivyo tunaingiza kutoka Kenya na maeneo mengine, ni eneo muhimu," amesema Bashe.
Amesema kuna wakati unaweza kununua kifungashio cha Korosho ambacho chini kimeandikwa 'Made in China' jambo ambalo kwa haraka mtu akiangalia anaweza kudhani korosho imetoka China.
Amesema kufuatia suala hilo, wizara ya Viwanda inafanyia kazi ili kuhakikisha wanatangaza uwekezaji katika vifungashio hususan eneo la kilimo kwani linahitaji uwekezaji na limetangazwa sana kwa sekta binafsi.
"Miezi miwili mitatu ijayo katika tovuti ya wizara ya kilimo mtaona takwimu ambazo zitaonyesha mahitaji ya vifungashio kwa mwaka kwa sekta aina na thamani gani ili kusaidia wawekezaji kujua kiwango cha niashara kilichopo," amesema Bashe.