Bashungwa awaasa vijana kuepuka tamaduni za kigeni
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashunga akiangalia mojawapo ya miundombinu ya skimu ya umwagiliaji ya Kikosi cha Jeshi 837 Chita Kilichopo Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Muktasari:
- Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa akitembelea shamba la Mngeta pamoja na Kikosi cha Jeshi cha 837 ambapo amewaasa vijana kuepuka tamaduni na desturi za kigeni zisizoendana na maadili.
Morogoro. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amewaasa vijana kuepukana na mila na desturi za kigeni zisizoendana na maadili ya kitanzania.
Bashungwa ameyasema hayo leo Alhamis Machi 9, 2023 wakati alipotembelea shamba la Mngeta lililopo chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Kikosi cha JKT 837 Chita mkoani Morogoro.
Amesema wakati JKT inaelekea kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, limefanya kazi kubwa ya kuendelea kufundisha uzalendo kwa vijana na kuwasaidia kuwapa ujuzi mbalimbali utakaowasaidia kwenye maisha yao.
“Lazima kuyaendeleza kama majukumu ya msingi na kama mnavyofahamu dunia inapitia changamoto mbalimbali na vijana wamekuwa ni waathirika wa changamoto hizi,”amesema na kuongeza.
“Kwa hiyo kupitia JKT lazima elimu ya uzalendo na hata Mwalimu Julius aliwahi kueleza kuwa Taifa lililopoteza uzalendo, mila zake na desturi ni Taifa,”amesema.
Amesema kupitia jeshi hilo, vijana wanaweza kuendelea kukumbushwa kwamba hayo ni mambo ya kigeni ambayo hayakuwepo wakati wa mababu na wazazi.
Amehoji kwanini utandawazi uwapeleke vijana katika huko na kuwaasa vijana kuwa watambulika kama Watanzania kwa mila na desturi za kitanzania.
Akizungumzia kuhusu kilimo mkakati, Bashungwa amesema wanaenda kujipanga kuhakikisha kuwa ekari 12,000 zilizopangwa kwa ajili ya kilimo mkakati zinalimwa.
Amesema kwa kufanya hivyo, wataendelea kuhakikisha suala la usalama wa chakula na kuwapa fursa vijana wanaohitimu Jeshi la Kujenga Taifa kujifunza.
Naye Mkuu wa JKT, Meja Jenerali, Rajabu Mabele amesema kikosi cha 837 ni miongoni mwa vikosi vya kimkakati kuhakikisha kuwa itakapofika mwaka 2024/2025, JKT linajitegemea kwa chakula.
“Kama inavyofahamika jukumu kubwa la JKT ni malezi ya vijana tunazalisha mali lakini vile vile kama sehemu ya Jeshi Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ), linafanya ulinzi,”amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi hicho, Luteni Kanali Emmanuel Kukula alisema katika utekelezaji wa kilimo mkakati wameanza na ekari 2,500 ambayo ikimalizika inatarajiwa kutumia Sh8.6 bilioni.
Alisema awamu hiyo ya kwanza ambayo ni kati ya ekari 12,000 ambazo zinalengwa katika skimu ya umwagiliaji, ujenzi wake umefikia asilimia 66.
“JKT imeanza kuzalisha mbegu za mpunga na kwa mwaka huu tunatarajia kuzalisha ekari 500 za mpunga wa mbegu na tayari tumeshaanza kuzilima na tumeshapandikiza kwa ekari 94,”alisema.
Luteni Kanali Kukula alisema katika kutekeleza mpango wa kilimo mkakati kwenye msimu huu wa kilimo wanatarajia kulima ekari 3500 za mpunga ambapo 3,000 ni mpunga wa chakula na mbegu ekari 500.