Bei vifurushi vya intaneti yaleta maumivu

Bei vifurushi vya intaneti yaleta maumivu

Muktasari:

  • Wakati sakata la kupanda kwa gharama za vifurushi vya intanenti likiendelea kutikisa, wadau wameanisha mambo sita yanayoifanya huduma hiyo kuwa lulu kwa sasa.

Dar es Salaam. Wakati sakata la kupanda kwa gharama za vifurushi vya intanenti likiendelea kutikisa, wadau wameanisha mambo sita yanayoifanya huduma hiyo kuwa lulu kwa sasa.

Kwa muda mrefu, kulikuwa na kilio kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano wakilalamikia bei ya vifurushi vinavyotolewa na kampuni za simu kuwa haviendani na thamani ya fedha wanayolipa.

Kutokana na kilio hicho, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliahidi kuyashughulikia. Mwishoni mwa mwaka jana ilitoa siku 90 za kuleta suluhu kwa kero zilizokuwapo.

Tofauti na matarajio ya wengi, Aprili 2 bei mpya ya vifurushi vya intaneti ilitangazwa ambayo ilikuwa kubwa maradufu ya ile ya mwanzo ambapo GB moja iliuzwa kwa wastani wa Sh3,000 kutoka Sh1,000 ya awali.

Malalamiko hayo yaliifanya Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha bei hizo mpya na kuelekeza gharama za zamani zirudishwe hadi itakapoelekezwa vinginevyo.

Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile alionyesha nia ya kuwasaidia wananchi kwa kuzielekeza kampuni za simu na TCRA kutafuta ufumbuzi.

Lakini ya kuyafanyia kazi malalamiko yaliyokuwapo, kilicholetwa kinaonekana kuwa mwiba zaidi ikizingatiwa matumizi ya intaneti nchini yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku hivyo kupandishwa kwa gharama zake kuyaathiri makundi tofauti ya jamii wakiwamo watumiaji wa kawaida, wafanyabiashara, wafanyakazi hata taasisi na mashirika.

Taarifa za TCRA zinaonyesha hadi Disemba 2020 kulikuwa na watumiaji milioni 28.5 wa intaneti nchini kutoka milioni 17.2 waliokuwapo Disemba 2015. Wateja hao, kati ya Oktoba na Disemba mwaka jana walitumia jumla ya GB 92.7 milioni jambo linalodhihirisha umuhimu wa huduma za intaneti nchini.

Biashara na matangazo ya mtandaoni ni baadhi ya shughuli zinazochangia kuongezeka kwa matumizi ya intaneti ambazo zinajumuisha huduma za benki, vikao na mikutano inayofanyika mitandaoni kwa kutumia mtandao wa Zoom ni mingine na mitandao ya kijamii iliyorahisisha mawasiliano.

Kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi zinauza bidhaa zake mtandaoni na kutokana na maendeleo ya tekinolojia, na Watanzania uwa miongoni mwa wanaozichangamkia fursa za biashara hizo.

Mtaalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Sospeter Mkasanga alisema teknolojia ndiyo kichocheo cha uchumi wa kidigitali ambao Serikali inalenga kuufikia hivyo huduma nyingi zitaendelea kuhamia mtandaoni zaidi ya ilivyo sasa.

Alisema Serikali mtandao na huduma nyingine zinazotolewa kupitia majukwaa ya kiteknolojia yataongeza mahitaji ya intaneti huku wafanyabiashara wengi wakiitumia kutafuta taarifa, kunadi biashara zao na kufanya mauzo kununua bidhaa kwa ajili ya maduka yao.

Hata kipindi cha majanga mfano mlipuko wa ugonjwa wa corona alisema umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza matumizi ya intaneti kutokana na kubadilika kwa mwenendo wa shughuli duniani kote.

Tofauti na ilivyokuwa hapo awali, sasa hivi watu hawakutani tena kwenye mikutano kwani vikao vingi vinafanyika kwa njia ya mtandao. Hata upigaji simu, mwingi ni ule wa mtandaoni unaowaruhusu wazungumzaji kuonana kwa njia ya video kuliko simu ya kawaida au ujumbe mfupi.

Kando na hilo, mawasiliano kwa njia ya mitandao ya kijamii yameongezeka miongoni mwa jamii, kukwepa kukutana mara kwa mara ili kujikinga na ugonjwa huo unaoambukizwa kwa njia ya hewa. Hili nalo limechangia watu wengi kuhakikisha wana vifurushi vya intaneti ili waweze kuwasiliana.

Kutokana na maendeleo hayo, wafanyabishara wadogo nao wamegeukia kwenye mitandao ya kijamii kusaka wateja wa biashara zao na nyingi zinafanyika huko ambako intaneti hutumika kuwakutanisha na wanunuzi.

Akizungumzia hilo, Wakili Bashir Yakub alisema idadi ya wanaotumia huduma hiyo nchini inaendelea kuongezeka siku hadi siku hali inayoashiria wateja wake wanakua zaidi kuliko huduma nyingine.

Wakili huyo ambaye amekuwa akipiga kelele kuhusu dosari zilizopo kwenye huduma za mawasiliano alisema kwa msingi huo kuligusa eneo hili ni kuyafikia maisha ya wengi hivyo kuwa rahisi kuibua malalamiko yao.

Yakub alisema umuhimu wa intaneti kw awananchi unaongezeka na matumizi yake yanakua ambapo watu wengi wanaitumia kutafuta taarifa mbalimbali.

“Umoja wa Mataifa umeishatambua huduma ya intaneti kama haki ya msingi ya binadamu kupitia `IRPC Internet Rights & Principles Coalition, the Charter of Human Right and Principle for the Internet’ (mikataba ya kimataifa ya matumizi ya intaneti ulimwenguni). Kwa hiyo gharama zote za miamala ya fedha, data na maongezi lazima ziwe chini kwasababu sio starehe bali haki na msingi wa binadamu,” alisema.

Katika kuhakikisha zinawafikia wateja wengi zaidi nchini, benki za biashara nazo zimejielekeza mtandaoni na sasa malipo mengi yanafanyika kielektroniki, intaneti ikihitajika zaidi.

Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania inaonyesha mwaka 2019 miamala iliyopita kwa njia ya benki mtandao ilikuwa Sh50 trilioni kati ya Sh99 trilioni ambayo ni jumla ya miamala yote iliyofanyika mwaka huo.


Wasanii watakavyoathirika

Mtangazaji na mmiliki wa chaneli ya Youtube, Frederick Bundala anasema mtandao huo hulipa kwa mfumo wa Cost per Mile ambao kwa lugha rahisi ni sawa na kusema, malipo kwa idadi ya watazamaji 1,000.

“Kwa mfano, kwa hapa Tanzania, kwa kila watazamaji 1,000 msanii au mmiliki wa akaunti ya Youtube hulipwa dola 1.7 za Marekani (takriban Sh3,900) ingawa kiwango hicho hubadilika mara kwa mara. Na Youtube hawaweki wazi sababu za kubadilisha,” alisema.

Miongoni mwa wasanii wanaonufaika na mtandao huu ni Diamond Platnumz kupitia kazi zake mbalimbali zikiwamo nyimbo zake mfano Waaah uliofikisha zaidi ya watazamaji milioni nne siku uliopandishwa.

Hii inamaanisha Watazamaji ambao ndio watumiaji wa intaneti wana mchango mkubwa katika kumuingizia fedha msanii yeyote anayeweka video yake mtandaoni hivyo kupanda kwa vifurushi vya intaneti itakuwa mwiba kwa wasanii.

Akizungumza na Mwananchi, mwanamuziki Amin Mwinyimkuu almaarufu kama Aman alisema gharama kubwa ya virushi vya intaneti itachangia kuzorotesha soko la wasanii kwa kuwa muziki kwa sasa umehamia mtandaoni.

“Tunatamani Serikali ikae vizuri na kampuni za simu kurudisha gharama za zamani. Hivi vifurushi vipya ni gharama kubwa bado Watanzania hatujafika huko, hofu kwetu wasanii kazi zetu zitakwenda kuzorota.

“Itakuwa ngumu mtu anunue GB yake moja halafu aende kuangalia wimbo youtube, hata wasanii wapya itakuwa ngumu kutoka maana haitakuwa rahisi kumshawishi mtu kufungua link hasa ya msanii asiyemfahamu,” alisema Amin.