Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bei ya tumbaku yazidi kupaa mahitaji yakiongezeka

Muktasari:

  • Ripoti ya Benki Kuu ya Oktoba 2025 inayoangazia tathmini ya hali ya uchumi ya kila mwezi inaonyesha kuwa tani moja ya tumbaku imefikia dola za Marekani 5,907.15 (Sh14.506 milioni) Septemba 25 mwaka huu ikiwa imeongezeka kutoka dola za Marekani 4,146.96 (Sh10.183 milioni) kwa kipindi kama hicho mwaka 2022.

Dar es Salaam. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita bei ya tumbaku katika Soko la Dunia imeongezeka kwa asilimia 42.44 kati ya mwaka 2022 na 2025, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza.

Ripoti hiyo inayoangazia tathmini ya hali ya uchumi ya kila mwezi inaonyesha kuwa tani moja ya tumbaku imefikia dola za Marekani 5,907.15 (Sh14.506 milioni) Septemba 25 mwaka huu ikiwa imeongezeka kutoka dola za Marekani 4,146.96 (Sh10.183 milioni) kwa kipindi kama hicho mwaka 2022.

Hali hii ilitajwa kuchangiwa na ongezeko la mahitaji yake ya bidhaa z tumbaku duniani na hivyo nchi wazalishaji kunufaika na neema hiyo kwa kuongeza kiwango cha mauzo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zilitumia vizuri ongezeko hilo la bei na kutumiwa vizuri na wakulima kwa kuwa hata mauzo ya zao hilo katika masoko ya nje nayo yameongezeka.

Ripoti hiyo ya BoT inaonyesha kuwa katika mwaka ulioishia Septemba mwaka huu, Tanzania ilipata Sh1.027 trilioni kutokana na mauzo ya tumbaku, zikiwa zimeongezeka kutoka Sh413.78 bilioni mwaka 2022.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa wakulima wa tumbaku kutoka mkoani Tabora, Kiswaga Matheo amesema ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi na soko hilo, huduma za ugani ziendelee kuimarishwa na wataalamu kuwafikia kwa wakati.

“Kama ni pembejeo zije kwa wakati na kiwango kinachotakiwa, kuna baadhi hawafikiwi kikamilifu au unakuta mtu unahitaji mifuko 50 ya mbolea lakini hupati yote,” amesema Matheo.

Maneno yake yaliungwa mkono na Antony Mayunga mkulima kutoka Shinyanga, aliyetaka kuainishwa maeneo zaidi yanayoweza kustawisha tumbaku ili watu waweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa.

“Kama kuna teknolojia wangetwambia, hata aina ya tumbaku inayostawi katika eneo husika kuelezwe, kwani bila kufanya hivyo watu wataendelea kulima kwa kubashiri au kwa mazoea,” amesema.

Hayo yanasemwa wakati bajeti ya Kilimo ya mwaka 2025/2026 inaonyesha kuwa uzalishaji wa tumbaku uliongezeka kutoka tani 58,508 msimu wa 2020/2021 hadi tani 160,000 msimu wa 2024/2025 na kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji wa pili Afrika.

Na ili kuongeza uzalishaji wa tumbaku Bodi ya Tumbaku imesambaza kwa wakulima tani 124,771.05 za mbolea, viuatilifu lita 72,418, chupa 1,627,839, pakiti 772,913, vyenye thamani ya Sh7.69 bilioni.

Pia imesambaza vifungashio ikijumuisha magunia 1,242,126 na Jute Twine kilo 383,220 na nyuzi kilo 84,301.5, vyenye thamani ya Sh13.3 bilioni kwa mpango wa ruzuku lengo likiwa ni kuzalisha tani 250,000 katika mwaka 2025/2026.

“Wizara kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania itaendelea kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa tumbaku kufikia tani 250,000 mwaka 2025/2026. Ili kufikia lengo hilo, Bodi itahamasisha na kutoa mafunzo kuhusu kanuni za kilimo bora cha zao la tumbaku kwa wakulima 5,000 na maofisa ugani 200 katika maeneo ya uzalishaji,” amesema.

Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Lutengano Mwinuka amesema Tanzania ina maeneo mengi yanayofaa kwa ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali lakini hayajatumika kikamilifu.

Amesema ili kutumia maeneo hayo kikamilifu ni vyema wizara ikaja na mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuweka wazi mazao yanayofaa katika maeneo mbalimbali ili wananchi wayajue,  sambamba na kufanya tathmini za mwenendo wa masoko.

 “Uelekeo ni mzuri lakini taarifa za mara kwa mara ni muhimu kuwajulisha wananchi namna mambo yanavyokwenda, bei za masoko, hali ya soko na tumbaku huwa inanunuliwa kwa dola, hivyo ina tija kuliko bidhaa nyingi za Kitanzania ambazo zinanunuliwa kwa shilingi,” amesema Dk Mwinuka.


Tahadhari yatolewa

Hata hivyo, Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema wakati nchi ikisherehekea ukuaji wa mauzo ya tumbaku ni vyema pia kuangalia athari zinazoweza kusababishwa na zao hilo.

Alitolea mfano wa baadhi ya athari na mojawapo ni ile inayofanya mazao mengine yashindwe kustawi katika eneo ambalo tumbaku imewahi kulimwa na ili kufanya hivyo, labda mtu asioteshe mazao kwa misimu kadhaa na ametoa angalizo la kuwatumia watoto katika uzalishaji.

“Tunapoangazia faida zinazotokana na tumbaku ni vyema zitumike kuondoa hasara zinazopatikana huko. Ili tuseme hiki kitu ni kizuri lazima kuangalia matokeo hasi na chanya kwa pamoja,” amesema.