Biashara ya ukahaba yashamiri-2

Biashara ya ukahaba yashamiri-2

Muktasari:

  • Timu ya waandishi wa Mwananchi imefika katika maeneo na kuzungumza na watu mbalimbali, wakiwemo wahusika ambao wameeleza masaibu wanayokutana nayo.

Jana tulianza kuchapisha makala maalumu kuhusu kushamiri kwa biashara ya ukahaba kwenye maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, katika uchunguzi huo imebainika kuwa, kuna kushamiri zaidi kwa watoto wadogo chini ya miaka 18 kujiingiza kwenye biashara hiyo haramu.

Timu ya waandishi wa Mwananchi imefika katika maeneo na kuzungumza na watu mbalimbali, wakiwemo wahusika ambao wameeleza masaibu wanayokutana nayo. Endelea


Ushuhuda wa wahusika

Mmoja wa makahaba wanaojiuza kwenye baa moja maarufu maeneo ya Manzese akijitambulisha kwa jina la Jack (28), alizungumza na gazeti hili na kubainisha kuwepo kwa makahaba walio na umri chini ya miaka 18, lakini akasema ni vigumu kuwabaini kwa sababu ya muonekano wa maumbile yao kufanana na watu wazima.

Anasema makahaba wanaoonekana wadogo huwa wanafukuzwa wanapojaribu kuingia katika baa hiyo, lakini wenye maumbo makubwa wanaruhusiwa kuingia.

“Ni vigumu kujua kama huyu ana umri chini ya miaka 18, lakini wale ambao wanaonekana wadogo huwa wanafukuzwa hapa. Wakiondoka unakuta wanarudi tena na kuendelea na biashara kama wengine,” alisema Jack.

Kahaba huyo anaeleza kwamba anafanya biashara hiyo kwa sababu hana shughuli nyingine ya kumwingizia kipato cha kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

Anasema wale wateja wa haraka (short time) wanalipia Sh7,000 hadi Sh10,000 ambapo Sh2,000 wanalipia chumba kwa kila anapoingiza mwanamume na kwa siku za wikiendi anaweza kuwahudumia wanaume kati ya 15 hadi 20. “Siku za kawaida hakuna watu wengi, naweza kupata Sh40,000 hadi Sh50,000 lakini siku za wikiendi nafikisha Sh100,000 mpaka Sh150,000,” anasimulia kahaba huyo ambaye alianza biashara hiyo miaka miwili iliyopita.

Ndani ya baa hiyo (jina linahifadhiwa) kuna vyumba vya kulala takribani vinane ambavyo ndani yake kuna kitanda kwenye kila chumba na kapu la taka. Vyumba hivyo ndiyo vinatumiwa na makahaba hao kwa huduma za haraka, lakini pia kuna vyumba maalumu (VIP) ambavyo viko sehemu tofauti ndani ya baa hiyo na bei yake ni tofauti.

Majirani katika maeneo ambayo biashara hizo zinafanyika wanasema makahaba hao wanawaharibu kimaadili watoto wao kwa sababu wanaona wanachofanya na wao wanaiga, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.

Kwa upande wake, mkazi wa mtaa wa Mnazi Mmoja, Kuluthum Mrisho alisema wanaishi nao hivyo hivyo kwa sababu nyumba yao ipo katika eneo hilo na hawana sehemu nyingine ya kwenda.

“Sisi tulishawazoea, kila mtu na maisha yake. Tutafanya nini, tutakwenda wapi baba yangu,” anasema mwanamke huyo.


Mwananyamala ‘Kwa Wahaya’

Mkazi wa Mwananyamala, Ramadhani Juma anasema eneo la Mwananyama maarufu kama “Kwa Wahaya” ni la muda mrefu na lilianza miaka ya 1980 walipohamia hapo kutoka Kisutu.

Anasema wanawake hao hawakuanza biashara hiyo hivi karibuni, bali walianza zamani kwa kuwafurahisha wanajeshi wa jeshi la kikoloni wakati huo.

“Hawa wanawake walihamia hapa miaka ya 1980 wakitokea mjini karibu na soko la Kisutu, hawa walikuwa pale kwa ajili ya kuwafurahisha wanajeshi wa kikoloni, siku zilivyozidi kwenda walihamia maeneo mengine,” alisema Ramadhani.

Alisema hadi eneo hilo linaanzishwa ni kwa sababu wapangaji walikuwa wanasumbua kulipa kodi, lakini kwa hawa makahaba, mwenye nyumba anakuwa na uhakika wa kulipwa bila usumbufu. “Wapangaji hawa hawasumbui katika suala la kodi, kama ni kwa mwezi au miezi sita uhakika wa kulipa upo tofauti na wengine inapofika wakati wa kulipa wanasumbua,” alisema.

“Binafsi namfahamu rafiki yangu alikuwa na nyumba ya kawaida yenye vyumba vitano, kutokana na kusumbuliwa na wapangaji aliamua kugeuza vyumba vidogo vidogo na kuwapangisha makahaba hao.

“Hii biashara ilianza kwa nyumba moja, kadri siku zilivyozidi kwenda watu wengine walinunua nyumba na kuzifanya hivyo, lengo ni kuachana na usumbufu wa kodi, kwani hawa wana uhakika wa kulipa,” alisema.

Juma alibainisha kuwa wanaofanya biashara hiyo wamekuwa wakipanga vyumba hivyo na umri unapokwenda wamekuwa wanawapangisha watu wengine.


Viongozi wa dini wazungumza

Viongozi wa dini nchini wameitaka Serikali kuingilia kati suala la kuongezeka kwa madanguro katika jamii ili kupunguza maambukizi ya magonjwa, ikiwemo Covid-19.

Wito huo wa viongozi wa dini umekuja baada ya gazeti hili kubaini kushamiri kwa biashara ya ukahaba kwenye madanguro ambayo yapo katikati ya makazi ya watu.

Baadhi ya viongozi, akiwemo aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda waliwahi kujaribu kukomesha biashara hiyo kwa kuwakamata makahaba, hata hivyo, jitihada hizo hazikuzaa matunda.

Mwananchi limebaini kuwa bado kuna madanguro mengi jijini Dar es Salaam, ambapo wanawake wenye umri kati ya miaka 14 - 40 wanajihusisha na ukahaba. Viongozi wa dini wamelaani biashara hiyo haramu na kutoa wito kwa Serikali, hasa zile za mitaa kutokomeza biashara hiyo katika makazi yao ili kuinusuru jamii dhidi ya maradhi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binaadamu kwa Jamii ya Viongozi wa Dini, Askofu Wiliam Mwamalanga anasema viongozi wa Serikali za Mitaa wapewe maelekezo ya kukabiliana na jambo hilo.

Anasema bado Serikali haijafanya jitihada za kutosha kukomesha biashara hiyo, ndiyo maana imeendelea kuwepo kila mwaka na jamii imeanza kuona ni jambo la kawaida.

“Serikali za mitaa zichukue hatua kukabiliana na madanguro kwa sababu yapo kwenye mitaa yao wanayoishi. “Nina uhakika viongozi hao wakifanya kazi yao ipasavyo, madanguro yote yatafungwa. Wenyeviti wa Serikali za Mitaa waelimishwe, wanaweza kabisa kuondoa tatizo hili,” anasema Askofu Mwamalanga.

Kiongozi huyo wa dini anasema amefuatilia suala hilo na kubaini kwamba sababu zinazowafanya wanawake kujiingiza kwenye biashara hiyo ni ugumu wa maisha unaotokana na ukosefu wa ajira.

Hata hivyo, anasema ukahaba siyo ajira ya staha kwa sababu licha ya kuhatarisha maisha yao, inawatenganisha na Mungu na pia jamii inayowazunguka.

“Hatari ninayoiona ni kwamba watoto wa shule za msingi na sekondari nao wamo kwenye madanguro hayo. Tunatengeneza jamii ya namna gani?

“Serikali kupitia wizara ya afya isilifumbie macho jambo hili, tena wakati huu tunapambana na ugonjwa wa corona, ni hatari zaidi. Wasipodhibitiwa watakuwa wanaeneza maambukizi kwa wengine,” anasema askofu huyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema biashara hiyo ni kitendo kiovu katika jamii kinachosababisha matatizo mengi, yakiwemo maradhi.

Anasema biashara hiyo haikubaliki katika jamii kwa sababu imekuwa chanzo cha matatizo mengi, ikiwemo kuongezeka kwa watoto wa mitaani pamoja na yatima.

“Serikali inapaswa kuchukua hatua, kwa sababu biashara hiyo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa maradhi, hasa Ukimwi, ongezeko la watoto wa mitaani na wanaoishi katika mazingira magumu,” anasema Sheikh Mataka.

Anabainisha kuwa wao kama viongozi wa dini wamekuwa wakijitahidi kutoa mafundisho, lakini vitendo hivyo vya uvunjifu wa maadili vimekuwa vikiendelea, jambo ambalo anasema ni dhambi na havikubaliki kwenye jamii.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima anasema ni kweli amri za Mungu zinavunjwa, lakini kama viongozi wa dini wanalo jukumu la kufundisha ili maadili yafuatwe.

“Kwa upande wangu siwezi kulizungumzia kwa kuwa sina takwimu wala ushahidi, niseme tu kwamba tunajua amri za Mungu zinavunjwa,” alisema Padri Kitima.

Mchungaji wa Kanisa la PCT lililopo Segerea, Didas Msonga anasema kuongezeka kwa vitendo vya ukahaba ni ishara ya hofu ya Mungu kupungua katika jamii, ndiyo maana wanaume na wanawake wanajihusisha na mambo ya ukahaba.

Anasema kwa kuwa ni jambo ambalo halikubaliki katika jamii, serikali ina wajibu wa kuchukua hatua ili kuwalinda wananchi wake, hasa wasichana wadogo wanaoingia kwenye ukahaba kwa sababu ya hali ngumu ya maisha katika familia zao. “Sisi kama viongozi wa dini tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuwataka waumini wamwabudu Mungu wao lakini serikali nayo iweke mikakati ya kukomesha madanguro huko mitaani,” anasema mchungaji huyo.

Mratibu wa huduma za makundi maalumu kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Danieli Sendoro anasema kushamiri kwa vitendo hivyo ni tatizo la mmomonyoko wa maadili na kukata tamaa kwa mabinti.

Anasema kwenye mambo ya maadili kuna vitu viwili ambavyo kundi moja linafanya vitendo hivyo kwa sababu wamechagua kama mfumo wa kuwawezesha kuishi na hii ni kutokana na wao kushindwa kudhibiti uendeshaji wa maisha kwa njia nyingine na kufanya vitendo vya ukahaba ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

“Kundi lingine ni mfadhaiko katika mabadiliko ya dunia, huletwa na kundi ambalo huhangaika kufanya maisha ili yawe kama wao wanavyotaka, ikiwemo kuuza miili yao na sio kwaajili ya kupata kipato, kwao imekuwa kama utamaduni,” anasema Mchungaji Sendoro.

Inaendelea kesho ambapo tutaangazia zaidi simulizi za wasichana wenye umiri chini ya miaka 18 walivyojiingiza kwenye biashara hii na masaibu waliyokutana nayo mpaka sasa.