Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bibi aliyeporwa ardhi alipwa Sh107 milioni

Arusha. Bibi Nasi Muruo (98), mkazi wa Sinoni, Arusha, amepokea malipo ya fidia ya ardhi yake Sh107 milioni kati ya Sh519.3 anazotakiwa kulipwa na kaya 110 ifikapo Novemba 28 mwaka huu na kaya zitakazokaidi, zitaondolewa.

Bibi huyo analipwa fidia hiyo katika eneo hilo la ekari nane baada ya Rais John Magufuli kuingilia kati mgogoro wa madai ya kurejeshewa ardhi yake aliyonyang’anywa tangu mwaka 1977 na baadaye kushinda kesi ya kurejeshewa ardhi hiyo mwaka 1979, lakini ikashindikana.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi Agosti 28 mwaka huu, alizipa miezi mitatu kaya 110 zilizojenga kwenye ardhi ya bibi huyo kumlipa Sh519.3 milioni, kulingana na ukubwa wa ardhi kwa kila kaya, la sivyo nyumba zao zinabomolewa na bibi huyo kukabidhiwa ardhi yake.

Akizungumza jana, Bibi Muruo alisema hadi juzi, karibu robo tatu ya kaya zilikuwa hazijakamilisha malipo lakini anaamini siku chache zilizobaki watamlipa.

Alisema anashukuru kaya zilizoanza kumlipa na ana imani mwisho mwa mwezi Novemba kaya nyingi zitakuwa zimemlipa huku akimshukuru Rais John Magufuli na Waziri Lukuvi akidai ameanza kupata haki yake aliyoisaka kwa miaka 42.

Bibi Muruo alisema baada ya malipo kukamilika anatarajia kukamilisha ndoto zake za kujengewa nyumba, kununua mashamba, kuanzisha biashara ya duka na kununua treka kwa ajili ya kilimo.

Mjukuu wa bibi huyo, Obedi Saiteru alisema wanakamilisha nyumba ya muda ya kukaa bibi huyo ili ahame nyumba ya kupanga eneo la sokoni.

“Watu wanalipa kidogo kidogo hasa kaya zenye maeneo madogo lakini zenye maeneo makubwa ukiondoa Kanisa la Evengalistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) bado hazijaanza kulipa, pamoja na kaya ya marehemu Edward Lenjeshi ambayo inadaiwa ndiyo iliyompokora bibi huyo ardhi yake na kuuza kwa kaya mbalimbali,” alisema Saiteru.

Katibu Mkuu wa EAGT, Askofu Dk Leonard Mwizarubi ndiye aliyekuwa wa kwanza, kulipa Sh69 milioni kwa bibi huyo kutokana na kuwa na eneo la mita za mraba 3,458.

Maagizo ya Serikali

Waziri Lukuvi alisema ndani ya miezi mitatu, kila kaya itatakiwa kulipa fedha hizo, kulingana na eneo lake, kila mita ya mraba watapaswa kulipia Sh20,000.

Alisema Serikali imechukua uamuzi huo kwa kutambua familia nyingi zilizouziwa eneo hilo ni maskini kwani ingeweza kuamua kutekeleza hukumu ya mahakama kuwabomolea wote.

“Hizi ni huruma za Rais wenu John Magufuli, baada ya kupokea malalamiko ya Bibi Muruo alinituma kuja hapa kumaliza mgogoro huu na sintarudi tena baada ya maamuzi haya,” alisema.

Bibi Muruo, kwa miaka 42 amekuwa akihangaika kudai ardhi yake na licha ya kushinda kesi na kutakiwa kurejeshewa ardhi hiyo tangu Mei 22, 1979 katika baraza la usuluhishi la ardhi na baadaye Mahakama Kuu lakini hakufanikiwa hadi Agosti mwaka huu.