Biden aweka historia mpya Marekani, Trump amkwepa

Biden aweka historia mpya Marekani, Trump amkwepa

Muktasari:

  • Licha ya vuguvugu la wafuasi wa Donald Trump kujaribu kupinga matokeo ikiwemo kufanya vurugu, lakini Biden ameapa kuwa rais mpya wa Taifa hilo kubwa duniani.

Marekani. Joe Biden ameapishwa kuwa Rais wa 46 wa Marekani wakati Taifa hilo likiwa limegawanyika kisiasa na kukabiliwa na janga la corona ambalo limeua maelfu ya watu na wengine mamilioni wakiambukizwa.

Biden,78, anakuwa Rais wa Marekani mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya Taifa hilo.

Jana, aliapa mbele ya Jaji Mkuu wa Marekani, John Roberts majira ya saa 11 jioni kwa saa za Marekani, akiwa ameshika Bibilia ambayo familia yake imekuwa ikiimiliki kwa zaidi ya nusu karne sasa.

Biden aweka historia mpya Marekani, Trump amkwepa

Hata hivyo, hafla ya kuapishwa kwake ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu 1,000 walioalikwa kutoka watu 200,000 ambao wamekuwa wakihudhuria katika sherehe zilizopita za aina hiyo.

Pia, sherehe hiyo haikuwa na shamrashamra kama za watangulizi wake kutokana na janga la Covid-19 na hofu za kiusalama kutoka kwa wafuasi wa Rais Donald Trump aliyeshindwa.

Biden aweka historia mpya Marekani, Trump amkwepa

Wageni mashuhuri waliothibitisha kuhudhuria sherehe hiyo ni pamoja na marais wastaafu, Barack Obama, George W. Bush na Bill Clinton. Makamu wa Rais, Mike Pence naye pia alithibitisha kuhudhuria hafla hiyo sambamba na mkewe, Karen.

Hata hivyo, Trump hakuhudhuria sherehe hizo kama alivyosema kupitia ukurasa wake wa Twitter mapema mwezi huu. Ratiba ya awali ilionyesha kwamba Trump angeondoka Ikulu kwa ndege ya Air Force One saa 1 jioni kwenda mapumzikoni, Mar-A-Lago huko Florida.

Trump amekuwa Rais wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya karne moja kutoshiriki sherehe za kuapishwa kwa mrithi wake. Ni marais watatu pekee huko nyuma ndiyo walisusia sherehe hizo, wa mwisho alikuwa Andrew Johnson, mwaka 1869.

Biden alianza mbio za urais wa Marekani mwaka 1987 kupitia chama chake cha Democrats. Hata hivyo, aliondolewa kwenye kura za maoni baada ya kubainika kwamba, alitumia maneno yasiyokuwa yake kwenye hotuba aliyoitoa.

Mwaka 2007, Biden alitangaza tena kugombea nafasi hiyo. Licha ya uzoefu wake katika Bunge la Seneti, Biden hakufua dafu katika kampeni hizo. Barack Obama alichaguliwa kuwa Rais, naye akamteua Biden kuwa Makamu wa Rais. Ushindi wa Biden unatarajiwa kuwa na tija kwa mataifa ya Afrika hasa katika utoaji wa misaada ambayo utawala wa Trump uliiondoa. Pia, utaimarisha ushirikiano baina ya Marekani na mataifa mengine duniani.


Maisha ya familia

Maisha ya kifamilia ya Biden yamekumbana na majonzi mengi baada ya kufiwa na mke na watoto wake wawili kwa nyakati tofauti. Hata hivyo, anapata ujasiri wa kuwa baba bora kutoka kwa watoto wake wengine pamoja na mkewe, Jill Biden.

Biden alifunga ndoa na Neilia Hunter mwaka 1966 na kufanikiwa kupata watoto watatu ambao ni Beau, Hunter na Naomi Christina Biden.

Biden aweka historia mpya Marekani, Trump amkwepa

Hata hivyo, Biden hatasahau tukio la Disemba 18, 1972 ambalo ni ajali ya gari iliyochukua maisha ya mkewe pamoja na binti yao, Naomi ambaye wakati huo alikuwa na mwaka mmoja tu.

Neilia na Naomi walipoteza maisha kwenye ajali hiyo lakini watoto wengine, Beau na Hunter waliishia kujeruhiwa vibaya.

Furaha ya Biden kushinda uchaguzi na kuwa Seneta wa Delaware iliingia doa baada ya kumpoteza mkewe na binti yake. Lakini, alisimama imara na kuwalea watoto wake mpaka walipopona kabisa majeraha yao.

Mwaka 1977, Biden alifunga ndoa ya pili na Jill ambaye ndiyo mkewe mpaka sasa. Wawili hao wamejaliwa kupata mtoto mmoja, Ashley Biden.

Hata hivyo, mwaka 2015, Biden alimpoteza mtoto wake wa kwanza, Beau, ambaye alikuwa na uvimbe kwenye ubongo. Hilo lilikuwa ni pigo jingine kwa mwanasiasa huyo, ambaye amekuwa akipambana katika maisha yake.

Beau alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuja kufuata nyayo za baba yake kwenye anga za kisiasa na kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwa Biden, ambaye hata hivyo alisimama imara na kuendeleza harakati zake za kisiasa na jana ametimiza adhma yake.