Binti aomba msaada aendelee na masomo kidato cha tano

Amina Abdul binti anayeomba msaada wa vifaa, mahitaji na nauli ya kwenda shule Ukerewe alikochaguliwa kujiunga na kidato cha tano. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Msichana huyo amefaulu masomo yake ya kidato cha nne kwa kupata daraja la kwanza, anaomba msaada wa vifaa vya shule na mahitaji mengine muhimu ili aweze kwenda shule aliyochaguliwa.

Morogoro. Binti mmoja mkazi wa Mafisa, manispaa ya Morogoro, Amina Abdul amewaomba wadau wa elimu, viongozi pamoja na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kumsaidia kupata vifaa na mahitaji mbalimbali ili aweze kwenda shule ambako amechaguliwa kujiunga na kidato cha tano.

Amina ambaye amemaliza kidato cha nne mwaka 2023 katika shule ya Sekondari Kihonda iliyopo manispaa ya Morogoro na kufaulu kwa daraja la kwanza katika mchepuo wa biashara, amechaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule ya Sekondari Bukongo iliyopo wilaya ya Ukerewe jijini Mwanza.

Namba ya kutoa msaada inayopatikana 0782976551 au 0715185912 mama yake mzazi.

Hata hivyo, kutokana na hali duni ya maisha ya wazazi wake, ameshindwa kununua vifaa na mahitaji muhimu ya shule yaliyoorodheshwa kwenye fomu ya kujiunga na shule hiyo.

Mbali ya kuomba msaada huo, Amina ameomba pia kubadilishiwa shule ili aweze kusoma mkoani Morogoro ambako ataweza kuwa karibu na wazazi wake ambapo baba yake anaugua kwa muda mrefu.

“Baba yangu anaumwa kwa muda mrefu, babu yangu mzaa mama amepofuka macho kutokana na ugonjwa wa presha ya macho, mhudumiaji mkubwa kwenye familia yetu ni mama. Kwa hiyo, hana uwezo wa kumudu gharama za mahitaji yanayohitajika,” amesema Amina.

Msichana huyo amesema katika kipindi chote alichokuwa anasoma, alikuwa akilazimika kufanya biashara ndogondogo siku za mwisho wa wiki ili aweze kupata mahitaji mbalimbali yakiwemo madaftari, sabuni, sare za shule na nauli ya kwenda shule na kurudi nyumbani.

“Nilikuwa nauza karanga na biashara nyingine ili niweze kumsaidia mama kupata mahitaji yangu ya shule, kiumweli nimesoma katika mazingira magumu sana. Hata hivyo, nashukuru nilifaulu vizuri na hatimaye nimechaguliwa kujiunga na kidato cha tano,” amesema.

Amina amesema kuwa bidii yake aliyoweka kwenye masomo ya biashara anatamani kuwa mhasibu, anamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kumsaidia kwa kumpatia ufadhili ili aweze kusoma.

Akizungumza na Mwananchi, baba mzazi wa binti huyo, Abdul Salum amesema huyo ndiyo mtoto ambaye anaamini atakuwa na msaada kwake kwa kuwa ana moyo wa kusoma na amekuwa mtoto mtiifu na mtulivu.

“Nina watoto wawili, mmoja alipewa ujauzito akiwa kidato cha pili na wa pili ndiyo huyu ambaye namuona ana moyo wa kusoma, hivyo naiomba Serikali inisaidie kumpatia vifaa na mahitaji yaliyoorodheshwa kwenye fomu aweze kutimiza ndoto zake.

“Mimi hapa nilipo ni masikini sina hata cha kuuza Ili nimpeleke mwanangu shule na akikaa hapa mtaani ndoto zake zitapotea,” amesema Abdul.

Amesema anaamini kuwa binti yake huyo akisoma anaweza akapata kazi na atakuwa mkombozi na msaada kwake kama mzazi na familia kwa ujumla.

Mzazi huyo amesema kama atatokea mdau au kiongozi atakayeguswa kumsaidia binti yake anaweza kuwasiliana naye kwa namba ya simu – 0782976551 au 0715185912