Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Biteko awaasa viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani

Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko (aliyevaa suti) akiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu wa kanisa la Moravian baada ya kuwekewa Wakfu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Jimbo la Kusini Magharibi,  Robert Pangani leo Juni 2,2024  jijini Mbeya.

Muktasari:

  • Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko  amewaasa viongozi wa dini kuhubiri amani kama ambavyo Biblia imeelekeza.

Mbeya. Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amewataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani na kukemea wanaohubiri udini na ukabila.

Dk Biteko ameyasema hayo leo Juni 2, 2024 wakati wa kuwekewa Wakfu Askofu Mkuu wa Kanisa la Moraviani Kanda ya Kusini Magharibi, Askofu Robert Pangani.

Amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan  ameshaweka njia ya maridhiano, hivyo viongozi wa dini wahubiri amani na mshikamano ili Tanzania iendelee kuwa kimbilio, huku  akieleza kuwa hata Biblia imetaja neno amani mara 429.

"Msiangalie itikadi za vyama, ukabila na udini bali onyesheni upendo na kuhubiri amani kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kwa kuweka maridhiano," amesema na kuongeza;

"Serikali tutaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi za dini, lakini tunakupongeza Askofu Pangani kwa hatua hii, tunaamini utafanya vizuri kuwaongoza vyema waamini, Serikali iko pamoja na wewe na Moraviani kwa ujumla," amesema Biteko.

Pia  amewaomba waamini kumheshimu, kumtii na kumsikiliza Askofu huyo akieleza kuwa na yeye ni binadamu pale itakapoonekana amekata tamaa avumiliwe na kutiwa moyo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo,  Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema utulivu na amani iliyopo mkoani humo ni kutokana na ushirikiano wa viongozi wa Serikali na dini.

Amesema Serikali ya mkoa huo inaamini Askofu huyo ataongoza vema na kumuomba kufuata ushauri wa watangulizi wake ili kufika mbali zaidi.

"Lakini nikuombe Naibu Waziri Mkuu kuna mgogoro wao wa kiwanja pale Dodoma umalizike ili wajenge ofisi, Mbeya tumekuwa na amani na utulivu kutokana na ushirikiano wetu," amesema Homera.

Naye Askofu kiongozi wa hilo, Conoradi Sikombe ameishukuru Serikali kwa namna wanavyopata ushirikiano akiahidi kuwa taasisi hiyo itaendelea kuhubiri amani na kushirikiana nayo.

"Tufikishie salamu kwa Rais kwamba tunafurahishwa na uongozi wake, tumekuwa na ushirikiano na Serikali na leo tunaomba kukabidhi tuzo maalumu kutambua mchango wake," amesema kiongozi huyo.

Akizungumza baada ya kuwekwa Wakfu, Askofu Pangani amesema ana deni kubwa kwa Taifa kutokana na ushirikiano mkubwa aliopewa, huku akiwaomba viongozi wenzake kufanya kazi ya Mungu kwa hofu.

Amesema tangu kuwapo kanisa hilo, wamekuwa wakishirikiana kwa ukaribu na Serikali katika kuwafikishia huduma wananchi ikiwamo elimu, afya, nishati na maji.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, lakini wamekutana na changamoto moja katika mfumo mpya wa udahili wa wanafunzi wa vyuo ambao si rafiki kwa sekta binafsi akiomba kuwapo mabadiliko kurejeshwa wa awali.

"Tumesaidia vijana mbalimbali kimaisha katika nafasi mbalimbali zaidi ya 1,000 wakiwamo wa mahitaji maalumu (1,203), vyuo vya ufundi 715 na nafasi nyingine 350, yote ikiwa ni juhudi za makusudi kuwafikishia huduma wananchi, lakini hata kumaliza migogoro ya wafugaji kule Mbarali,” amesema Askofu huyo na kuongeza;

"Niwashukuru wote kwa mchango wenu na ninajua kazi ni ngumu, ila tufanye kwa hofu ya Mungu na tuna imani kubwa na Rais wetu na tutaendelea kushirikiana naye." Amesema.