Blandina Nyoni afunguka alivyotaka kukataa uteuzi wa Rais

Muktasari:

  • Blandina Nyoni amezungumzia changamoto anayoiona kwenye mfumo wa kodi hivi sasa, huku akieleza matukio mbalimbali kwenye maisha yake, ikiwemo namna alivyotaka kukataa uteuzi wa Rais kutokana na hofu.

Dar es Salaam. Unamkumbuka Blandina Nyoni? Mwanamama huyu mhasibu kitaaluma na mmoja wa waanzilishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA amezungumzia changamoto anayoiona kwenye mfumo wa kodi hivi sasa, huku akieleza matukio mbalimbali kwenye maisha yake, ikiwemo namna alivyotaka kukataa uteuzi wa Rais kutokana na hofu.

Nyoni aliyeteuliwa kuwa Naibu Kamishna mwaka 1996 na Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamini Mkapa, aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi aliyoyafanya hivi karibuni.

Anasema mifumo ya kodi imeendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka, tangu kuanzishwa kwa TRA mwaka 1996 ikilinganishwa na sasa, pia viwango na wigo wa kodi navyo umeendelea kuboreshwa.

“Ukiniuliza ni maeneo gani yana viwango vikubwa vya kodi nitasema sekta ya utalii, ukubwa huo unawafanya wanaofanya shughuli za utalii au biashara katika sekta hiyo iwe vigumu kuwavutia watu wengi kuja,” anasema.


Blandina Nyoni akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi wa Mwananchi Herieth Makwetta. Picha na Geofrey Mlwilo


Nyoni, ambaye safari yake ilianza kama mkufunzi msaidizi kwenye Chuo cha Maendeleo cha Mzumbe (DMI) mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, anasema kwenye sekta nyingi zisizo rasmi na rasmi, kuna haja ya kuendelea kuboreshwa kwa mazingira ya kikodi ili kuwezesha watu kutoka katika sekta isiyo rasmi kuwa sekta rasmi.

Nyoni alihamia TRA akitokea Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) alikohudumu hadi mwaka 1995 kabla ya kukutana na Rais Mkapa aliyemrejesha kwenye utumishi wa umma.

Akizungumza namna alivyokutana na Mkapa, Nyoni anasema wakati wa utumishi wake ndani ya shirika la USAID alipata fursa ya kufanya mafunzo nchini Marekani katika Jimbo la Washington, akiwa huko Rais Mkapa alifanya ziara naye akapata nafasi ya kufanya mazungumzo naye kwa muda mfupi katika Ubalozi wa Tanzania nchini humo.

“Mara nyingi nilipokuwa nikienda Marekani, nikifika tu nilikwenda ubalozini na kuripoti kuwa nipo hapo kikazi, kwa hiyo katika safari hiyo nikawa nimekwenda ubalozini na baada ya siku kama tatu aliyekuwa balozi alinipigia simu kuwa Rais anakuja, hivyo anatukaribisha Watanzania wote nyumbani kwake, akitutaka akinamama twende mapema ili tumsaidie mkewe kutayarisha chakula cha pamoja,” anasema.

Anasema hakuchelewa, aliomba ruhusa na kwenda nyumbani kwa balozi kusaidiana na kinamama waliokuwepo na jioni walikusanyika katika tafrija na Rais, yeye akiwa miongoni mwa waliokuwa wakikaribisha wageni.

“Siku hiyo nikapata bahati ya kuzungumza na Rais, ambaye aliniuliza ninafanya nini huku? Nikamweleza akaniambia hapana, rudi nyumbani uko vizuri waweza kulisaidia Taifa, nikamwambia niko huku kwa mafunzo.

Hii ilikuwa mwaka 1995, baada ya kumaliza mafunzo nilirudi nyumbani na akanihamasisha niombe kazi TRA maana ndiyo ilikuwa inaanzishwa,” anasema Nyoni.

Nyoni anasema Rais Mkapa alimweleza kuwa angependa kumuona akifanya kazi TRA ambayo ndiyo ilikuwa kwenye mchakato wa kuanzishwa. “Nilitafakari sana, yaani mtu mdogo kama mimi halafu Rais anakwambia ‘wewe unafanya vizuri kwa nini usije kujenga Taifa lako?’ kwa hiyo niliporudi mara moja nikafuatilia na kwenda TRA, nikaelezwa nafasi zilizopo, hivyo nikaamua kuomba kuwa naibu kamishna. Kwa hiyo niliitwa kwenye usaili, tulikuwa wanane baadaye niliandikiwa barua kuwa nimeteuliwa kuwa naibu kamishna wa matumizi nikiangalia fedha za ndani, basi ndipo safari yangu ilipoanzia serikalini nikiwa umri wa miaka 24,” aliongeza.

Anasema Julai mosi, 1996 TRA ilipoanza rasmi na yeye alikuwa mmojawapo wa waanzilishi akiwa naibu kamishna na mwaka mmoja na nusu baadaye aliteuliwa kuwa kamishna wa kwanza wa fedha wa TRA, walipoanzisha Idara ya Fedha.


Ateuliwa mhasibu mkuu wa Serikali

Nyoni ambaye ni mama wa watoto wawili wa kiume, anasema alifanya kazi TRA mpaka mwaka 2000.

“Rais alipoapishwa kwa awamu yake wa pili, alipotoka kuapishwa uwanjani usiku wake alitangaza uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge. Baada ya hapo, siku iliyofuata tangazo lingine la kapishwa alikuwa yeye kuwa Mhasibu Mkuu wa Serikali, nafasi ambayo hakuitegemea.

“Nilijiuliza sana, lakini kwa kuwa mimi ni mhasibu na nimesoma nilijiambia nitaweza. Ilinichukua muda sana, lakini nilishauriwa na baadhi ya watu akiwemo aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Malkizedeck Sanare, ambaye aliniambia nimeshauteuliwa na Rais napaswa kwenda, sitakiwi kukataa nikamletea matatizo.

“Nilikuwa nikijichelewesha nikifikiria namna ya kuyavaa majukumu hayo makubwa, hadi katibu mkuu wa wizara akanipigia simu nikamwomba anipe wiki moja nifanye makabidhiano ya ofisi, akasema hapana, njoo uripoti kwanza, akampigia tena kamishna Sanare akamtaka aniruhusu...

Nyoni anaongeza kuwa “nilimpigia hata aliyekuwa msaidizi wa Rais wakati huo nikamuuliza hivi naweza kukataa? Akaniambia ‘Rais amekuteua halafu ukatae, hivi unajipenda?’ Nikamweleza woga wangu, nisije nikaenda halafu kazi nisije kuifanya vizuri, maana sijawahi kabisa kuwa na nafasi ya juu hivyo…

“Akaniambia usiogope na akaenda akamwambia Rais, akasema ‘huyu ndiye ninayemtaka, maana ukiona mtu anayekataa unapomteua huyo ndiye anayefaa’,” anasimulia.

Anasema si kwamba alikuwa hataki kazi, bali alikuwa akiangalia ukubwa wa hiyo nafasi, mhasibu wa Serikali nzima ya Tanzania, baadaye akajiambia ‘nitaweza’.

Nyoni anasema wakati huo ulikuwa wa mageuzi makubwa ya sekta ya fedha ambapo hata kuanzishwa kwa TRA ilikuwa ni sehemu ya mageuzi ya kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kwa hiyo akaona ni vema awe sehemu ya mageuzi hayo.

Anasema alikwenda kuanza kazi katika nafasi hiyo mpya na wakati wake alishiriki kuweka mifumo ya usimamizi wa fedha na mapato ya Serikali, hivyo kuwa mmoja wa watu waliofanya kazi usiku na mchana kuweka mifumo ya kihasibu na kuhakikisha mapato na matumizi ya Serikali yanadhibitiwa ipasavyo.

Anasema ni wakati huo akiwa mhasibu mkuu wa Serikali, Sheria ya Fedha inayotumika hadi sasa ilipotungwa pamoja na kanuni zake lakini pia sheria ya manunuzi na kanuni zake, walifanya kazi na wahisani wote ikiwemo Benki ya Dunia (WB), Shirika la fedha duniani (IMF) na wengine walikuwa wakiiunga mkono Serikali kwenye mageuzi waliyokuwa wanayafanya kwenye sekta ya fedha.

Hata hivyo, Nyoni anasema sheria ya manunuzi ambayo alitumia kipindi kirefu kuitengeneza na jopo lake, iliwahi kumuumiza yeye mwenyewe alipokuwa Wizara ya Afya baada ya kusaini nyaraka ambazo hazikuwa na mkataba.

“Viongozi wengi wanaingizwa mkenge usipokuwa makini, lakini mimi nilikuwa sisaini nyaraka mpaka nimeikagua. Nyaraka husika nilikagua vizuri tu, nikaisaini, mwanasheria wa wizara ameniletea. Lakini baadaye ikaja kugundulika mtu amelipwa lakini mikataba hakuna. Mafaili yalitafutwa na kutafutwa mikataba haikuonekana,” anasema.


Ugumu kwenye uhasibu

Nyoni anasema alipofika alikuta kuna hoja nyingi za ukaguzi na hasa kwenye manunuzi ambazo zilikuwa nzito.

Anasema alikuta watu wanafanya kazi kwenye karatasi na udhibiti ulikuwa mdogo, hakukuwa na kumbukumbu za kutosha, hivyo hata kama kitu kimefanyika sawasawa, mwisho wa siku mkaguzi asipopata nyaraka atasema hesabu haziko sahihi.

“Kwa hiyo tulianza kuweka mifumo ya kompyuta ili kuondoka kwenye ulimwengu wa karatasi na kuingia kwenye mfumo mpya. Kulikuwa na vitu viwili, tulianza matumizi ya kompyuta lakini tukajikuta kwamba tunaendelea pia na matumizi ya karatasi kwenye kuhifadhi kumbukumbu.

Ilikuwa ni kazi kubwa ya kuwahamisha wahasibu kutoka kwenye karatasi kuingia kwenye mfumo mpya, nikaanza kufuta rejesta na kuwalazimisha wote kuingia kwenye mfumo mpya,” anasema Nyoni, msomi wa CPA.

Anaongeza kuwa “watu niliowakuta walikuwa na ujuzi lakini walihitaji kunolewa zaidi, utunzaji wa kumbukumbu ulikuwa ni dhaifu ilihitajika mhusika uwepo, maana ilikuwa inawezekana kabisa mtu umefanya malipo na umeandika kwenye karatasi lakini baada ya muda karatasi huioni”

Akisimuliwa anasema waliboresha mfumo wa kuhifadhi, namna ya ulipaji na pia ufanisi katika ulipaji, ambapo wakati huo watu walijaa sana Hazina, hivyo walikuwa wanaboresha mifumo ya ulipaji ili kulipa haki za watu hasa wastaafu kwa wakati.

“Ninachokumbuka nikiwa mhasibu mkuu wa Serikali, hakuna siku nilirudi nyumbani kabla ya saa sita usiku na nakumbuka mwaka 2001 Desemba, Krismasi yote tulisherehekea tukiwa ofisini, sikukuu zote, hadi mwaka mpya hadi tarehe mbili, ukija saa nane usiku pale kwetu ilikuwa ni kama mchana,” anasimulia.

Japokuwa yeye ni Mkristo anasema kwa kipindi hicho alisahau hata kwenda kanisani kwa sababu kuna majukumu ambayo yaliwekea ukomo.

“Nilipofika, wahasibu wengi walikuwa nyuma kitaaluma, nilihakikisha naweka maandiko ya kuomba fedha ili kuinua taaluma na hadhi ya wahasibu Serikalini, ambapo tuliweka programu kubwa ya mafunzo ya miaka mitano kuhakikisha wahasibu wote wanajua kompyuta na wapate CPA na hata kuwalazimisha wengine kusoma. Hadi niliandikwa magazetini,” anasema.

Anasema kwa wakati huo ni kweli ilikuwa ni suala zito kulazimisha watu kusoma, lakini aliweka ukomo kwamba kufikia miaka mitatu kila mhasibu awe na diploma, asiyepata itabidi kumbadilisha kitengo au tumrudishe utumishi, kwa sababu hatuwezi kuwa na wahasibu ambao hawajui wanachofanya.


Kwingine alikoongoza

Mwaka 2007, Nyoni aliteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii baadaye ilihamishiwa Wizara ya Afya mwaka 2009.

Anasema alipokuwa Maliasili, Uvuvi na Utalii ilikuwa ni kipindi kigumu pia kwa sababu ni wakati ambao majangili walitamalaki katika hifadhi za Taifa, uwindaji haramu na uharamia wa nyara za Serikali na alitakiwa kuweka woga kando na kwenda mstari wa mbele kupambana na wahalifu hao.

“Kuna wakati kulikuwa na magogo tunakamata bandarini, ilibidi niwe thabiti, nilikuwa nikipigiwa simu hata saa nane ya usiku, niliwasha gari yangu, Toyota Rav4 na kutoka ninaenda kwenye tukio kisha tunampa waziri taarifa,” anasema,


Changamoto TRA

Nyoni anaeleza kuwa katika nafasi alizopita, alipokuwa TRA ilikuwa wakati mgumu kwa sababu alifika akawakuta watu waliokuwa wakifanya idara za zamani, mtihani ulikuwa ni kuanzisha kitengo, akiwa hana karatasi wala rejea, hivyo kulazimika kulala na karatasi ili akikumbuka kitu anaandika ili asisahau.

“Ilikuwa ni wakati ambapo kila mtu alikuwa anatakiwa awe mbunifu na alitaka kuonyesha uwezo wake, lakini kikwazo vilikuwa vitendea kazi duni, ambapo kwa wakati huo nilitokea USAID ambapo nilikuwa mtu wa kwanza kuwa na kompyuta mpakato, ambayo walinipa. Kutoka kuzoea kufikiri nakutumia kompyuta, unarudi kufikiri na kutumia karatasi, ilikuwa kazi ngumu.

“Fikiria ulishazoea kule ilikuwa kama unatafuta taarifa ukiingia tu kwenye kompyuta unaipata moja kwa moja, haichukui hata dakika, unakuja sehemu ambayo umekalia meza ukiangalia ulipotoka, huku ukarabati unaendelea halafu lazima ufanye kazi, ni wakati ambao niliona ni kukubali mazingira na kuwa mbunifu, ilikuwa changamoto kubwa,” anaelezea.


Ahudumu bodi kibao

Tangu alipostaafu mwaka 2015, Nyoni ameendelea kutumika katika bodi kadhaa. Amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Mwenyekiti wa kwanza wa bodi ya Dawasco wakati Edward Lowassa akiwa Waziri wa Maji akisema wakati huo alipewa siku 100 maji yawe yanatiririka Dar es Salaam.

Kadhalika, nyoni amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la nyumba (NHC) na kuhudumu katika bodi za Benki ya NBC, Bodi ya usimamizi wa madini, Bodi ya NBAA, bodi ya NMB, Bodi ya National Bureu de Change, Bodi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye Kanseli ya chuo hicho, ametumika pia kama makamu mwenyekiti wa Kanseli ya Chuo Kikuu cha Mzumbe ambapo alikuwa akiingia kutokana na nafasi zake alizokuwa nazo.

“Nilikuwa naingia kwenye bodi ikiwemo Bodi ya Chuo Kikuu cha Muhimbili, pia Bodi ya Chuo cha Utalii nikiwa Maliasili, nikiwa Wizara ya Afya niliingia bodi ya NHIF na baadaye nilimteua mkurugenzi awakilishe.

Bodi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilimtaka Katibu Mkuu lakini baadaye niliteua mwakilishi, kuna bodi ya hospitali ya milembe nilikuwa naenda mwenyewe kwa sababu ilizungumzia wagonjwa ambao ni wahalifu ambao walikuwa wanatakiwa kupewa msamaha, kutokana na uzito wake nilikwenda mwenyewe,” anasema.

Nyoni amehudumu pia kwenye bodi ya Shirikisho la Wahasibu wa Serikali Kusini mwa Afrika akiwa mmoja wa waanzilishi lakini pia akawa mwenyekiti wa Bodi ya shirikisho hilo.

Vilevile amekuwa kwenye Bodi ya wataalamu wa Fedha yenye makao makuu yake Marekani, pia kwenye Shirikisho la Fedha Duniani (IFAC), ambapo waliendeleza kanuni za kihasibu kwenye nchi zinazoendelea, alikuwa Bodi ya Global Fund ambapo alikuwa makamu mwenyekiti na mwenyekiti wa kamati.

Kadhalika amekuwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Salma Kikwete na kwa sasa anamalizia muda wake wa miaka 10 kwenye Bodi ya Benjamin Mkapa Foundation na ana bodi nyingine ambazo nyingi anahudumu kama mjumbe wa bodi na pia kama mwenyekiti wa fedha na ukaguzi.